Bibi yangu alikuwa hanipendi nilivyokuwa mdogo, sasa hivi haishi kunipigia simu

ephen_

JF-Expert Member
Oct 28, 2022
3,624
14,801
Habari wana JF! kama uzi unavyojielezea.

Mimi ni binti nilizaliwa miaka kadhaa iliyopita, katika kukua kwangu nilibahatika kulelewa kwa bibi mzaa baba ambapo tulikuwa wajukuu wote wa watoto wake.

Nilienda kuishi hapo sababu mama yangu alikuwa ana maisha magumu kwa wakati huo so ilimlazimu kunipeleka kuishi hapo wakati yeye anazidi kujitafuta, isitoshe baba alikuwa hampi hela ya matumizi sababu hawakuwa wanandoa.

Msemo wa "yatima hadeki" niliuelewa hapa, sio kwamba nilikuwa yatima hapana ila niliishi sehemu ambayo hayupo baba wala mama yangu, siwezi sema walikuwa wananitesa kwa sababu chakula nilikuwa nakula milo yote mitatu ila tu changamoto za hapa na pale ambazo ziliweka vidonda moyoni mwangu mpaka nimekua hivi mtu mzima nakumbuka yote.

Tulipokuwa tunaishi ni Dar tena katikati ya mji kabisa. Bibi yangu alikuwa anapenda sana kuniambia "Wewe sio mtoto wa mwanangu, baba yako ni kinyozi" kauli zile zilikuwa zinaninyima raha sababu mimi nampenda sana baba yangu na isitoshe tumefanana sanaa.

Binamu zangu walikuwa wananitania "kumbe wewe sio mtoto wa mjomba" maneno yake yalikuwa yananiuma na kunifanya niwe mnyonge isitoshe ndo kwanza nina miaka 5.

Baba alikua akija hapo nyumbani namfata namuuliza "baba ety mimi baba yangu ni kinyozi?" Mzee alikuwa anasema "nani kakwambia maneno hayo" namwambia "bibi ndo kanambia" Jibu lake kila siku lilikuwa ni lile lile kwamba Nimzoee bibi, nisisikilize maneno yake.

Bibi yangu alikuwa mkali sanaaa nikikosea kitu kidogo ananiambia ndio mana wewe sio mjukuu wangu😂 ndugu zangu wote walikuwa awaniiti jina langu mara nyingi waliniita jina baya nakumbuka nilienda kwa mama kumuona nikamwambia, mimi kule wananiita banyamrenge kwani ndo nini? Mama angu machozi yalimlenga tu! Akanambia nitaongea nao wasikuite tenaa.

Nakumbuka mama akanirudisha kwa bibi waligombana sana kuhusu hilo jina maneno bibi alimwambia mama ni kwamba " Wewe huyu mtoto sio wa mwanangu, na mtoto umetuletea nuksi vilevile, wewe kwenu sio Tanzania umetokea misituni wanapokaa nyani na watu wafupii" Mama aliondoka akiwa amekasirika na aliniacha pale nikiendelea kusota.

Nilipofikisha umri wa kuanza kusoma nilipelekwa Shule ya msingi, na uzuri darasani nilikuwa vizuri sanaa bibi yangu akawa anasema "Wewe huna lolote hata ukipata maisha mazuri unadhani utatukumbuka basi, Sijui kwanini Mtoto wangu kakung'ang'ania na cha kukwambia tu Baba yako ikitokea amekufa hautorithi hata kijiko"

Mimi nililia sanaa nikaondoka hadi nyumbani kwa mama yangu sababu ilikuwa kwa mguu nafika. Mama akaniuliza kwanini umerudi nikamuelezea kila kitu basi akakubali nibaki kukaa naye japokuwa nilipoingia darasa la pili alikosa hata hela ya kuninunulia madaftari na Mzee hakuwa anatumia hela nikiwa kwa mama.

Maisha yaliendelea nikiwa kwa mama lakini kila nilipopata nafasi nilikuwa naenda kwa bibi kumsalimia, mambo yake ni yaleyale Wewe sio mjukuu wangu baba yako kinyozi, mwanangu akifa hautarithi hata kijiko nikirudi kwa mama namuelezea kila kitu so mama akanikataza kwenda kwa bibi sababu naenda na furaha nikirudi nakuwa na huzuni.

Nilipomaliza primary Mzee akanipeleka shule moja ya bweni hapahapa Dar, Nilisoma vizuri tu likizo narudi kwa mama sababu maisha yalikuwa tayari mazuri upande wake, nilipofika form 2 likizo mzee akasema niende kwa bibi kumsalimia, nilivyoenda Bibi kama kawaida yake alinisema sana kisa tu nilienda nimevaa suruali akanambia nishaanza umalaya😂💔 Hata shule hadhani kama nitafaulu Mwanake amepata hasara kuharibu pesa kunipeleka bweni.

Aisee nilijisikia vibaya mnoo lakini nilivyorudi nyumbani sikumwambia mama tayari nilipata akili za kiutu uzima sikutaka kuwagombanisha matokeo ya form 2 Yalivyotoka nilipasua na Distiction, Mzee alifurahi sanaa! Akalipa ada nikaendelea form 3, Nilipomaliza form 4 shuleni kulikuwa na graduation yangu ndugu zangu walikuja na bibi pia, ukafika wakati wa kutoa vyeti vya heshima Nakumbuka nilipewa vyeti vitatu vya masomo niliyokuwa naongoza.

Muda wa kula ulipofika Bibi akanifata akaniuliza umepewa vyeti vingapi? Nikamjibu "vitatu" basi akabinua midomo Siwezi kusahau hii. Nikamaliza form 4 matokeo yalivyotoka nikawa nimefaulu vizuri! Nikapangiwa shule kwenda Advance. Bibi yangu hakuwa bado ameamini macho yake kama napanda vidato😹🤍 Wajukuu wengine aliokuwa anawathamini wote waliishia form 4. Basi nikamaliza form 6 nikapangiwa kwenda Jeshi.

Nilipokuwa jeshi matokeo yakatoka nimefaulu vizuri kwenda chuo, Bibi yangu alionyesha hasira ya waziwazi tena nilikosa mkopo, akawa anasema nikae nyumbani hadi nipate mkopo, Mama angu alipinga sana hilo jambo la mimi kubaki nyumbani! Alitoa hela yake yote ya mtaji akanilipia ada 1.8M chuo kimoja hapa Dar.

Kabla sijaendelea safari yangu ya chuo naomba nielezea tabia zangu.
Malezi niliyopewa kwa bibi yangu yalinifanya niwe binti nisiyejiamini, furaha kwangu ilikua ni ya kutafuta kwa tochi sababu muda wote napewa Masimango nakumbuka nishawahi kumwambia mama Angu "Mbona wewe hunipendiii"🥺 mama akaniuliza kwanini unasema hivyoo!

Nikamjibu "Wewe hutaki kukaa na mimi, huku nateseka!" Mama akanambia "Mimi nakupenda sana sitaki ukae hapa kwangu sababu sijui utakula nini! Milo mitatu kwangu ni changamoto, lakini kwa bibi yako chakula kipo cha kutosha" Mama akaendelea "Nikipata hela nitakuja kukuchukua mwanangu" Niliridhika na lile jibu.

Yaani mimi hadi sasa ni mtu wa peke yangu peke yangu sio mtu wa marafiki kwa sababu nimezoea kuwa hivyo. Nilikuwa mwembamba sanaaa kwa mawazo. Hadi kipindi fulani watu walikuwa wanasema mbona huyu mtoto hakuii? Nahisi kukosa furaha, mawazo yalifanya nidumae.

Basi mama alinilipia ada nikaanza chuo rasmi! Maisha ya chuo bila mkopo na familia zetu hizi ni changamoto kidogo lakini nashukuru Mungu mimi sio mtu wa tamaa na mama yangu amenifundisha sana kuhusu Mungu so Mambo mengi ya kijinga ambayo yanafanyika chuoni mimi yamenipita kushoto. Muda mwingine unakosa hela ya matumizi lakini sithubutu kufanya mambo mabaya!

Wakati naingia mwaka wa pili Mzee akanambia Kamuone bibi yako, hapo nina kama miaka 4 sijaonana na bibi. Ikafika siku nikaenda yaani alikuwa ameshanisahau kabisa sababu nimenenepa nishakuwa mdada🥺 akaniangaliaa akaniuliza wewe ni...... nikamjibu ndiyo! Akasema mbona umekuwa mkubwa hivyooo, sikutegemea na hivi tunaongeaga tu kwenye simu tungekutana njiani nisingekujua Wallah. Nikamwambia ni mimi bibi.

Nilimuuliza unaendeleaje akasema vizuri ila uzee huu magonjwa yananiandama pressure nikamwambia pole. Lakini mimi ndani ya moyo wangu sina amani muda huoo! Maneno yote yale "wewe sio mtoto wetu" "baba ako akifa hata kijiko hupati" "mtoto una roho mbaya sana wewe" bado yanapita masikioni mwangu.

Masimango manyanyaso yote nayakumbuka. Akanambia mjukuu wangu umekata kabisa mguu kuja hapa yaani mama yako anakufundisha tabia mbaya, wewe mwenyewe unajua katika wajukuu zangu wote! Wewe ndo nakupenda sanaaa!!😹💔Oooh! Kimoyomoyo nilihisi naota, Bibi mjukuu gani unasema unampenda sana kuliko wote? Ina maana huyu mzee kasahau yote aliyonifanyia au!? Sawa nilikuwa nakula kutwa mara 3 kwa bibi yangu msosi ni wa kumwaga lkn hiyo haikutosha katika malezi yangu. Nilihitaji kuona upendo, thamani kutoka kwenu! 😹 hayo niliyasema moyoni lkn!! Sikumwambia kitu muda wote nilikua kimya moyoni ndo naongea mwenyewe.

Nilisimama nikaenda chooni nililia sanaa🥺 huyu mzee vipii ni uzee au kuna kingine, hivi mimi ndo nimepanda thamani kiasi hiki au, hadi aliyekua hanitaki anasema yeye ananipenda sana kuliko wajukuu zake wote!? Amesahau alivyonitumbukiza kwenye mfuko wa takataka nilivyokua mdogo?

(Hii nilihadithiwa na binamu yangu mkubwa alipokuwa ananitania kwamba ndo mana nilitupwa kwenye mfuko wa taka na bibi mama angu alivyoenda kunipeleka nilivyokuwa mdogo sababu bibi alikuwa hanitaki! Kwanini mwanae kazaa na banyamrenge") Lakini mama angu hajawahi kuniambia hili kama nilitupwa kwenye takataka.

Basi nilishinda kwa bibi siku hiyo lakini moyoni sina Amani kabisa sio kwamba simpendi hapana ila tu nikiwa karibu yake nakuwa sipo comfortable. Mida ya saa 10 niliaga kuondoka, tangia hapo simu hazikauki hadi nyingine sipokei, akipiga anauliza utakuja lini kuniona namwambia likizo nitakuja. Juzi hapo alinipigia simu kwamba ananisalimia tu nikamwambia Nashkuru!

Nyuma kidogo kuna siku bibi yangu alimpigia simu mama anamlaumu kwanini ananikataza kwenda kumuona? Mama angu akamjibu simkatazi mtoto kuja kwako ni yeye mwenyewe isitoshe mtoto ni mkubwa sasa ni vyema ukimpigia kuongea nae mwenyewe". Simu ilivyokata nikamuuliza mama kwanini bibi alikua hanipendi? Akanambia "Siwezi kukuambia kila kitu sababu yashapita, ila tu alikua hanipendi na hataki mwanae anioe kisa mimi sio kabila lao. Hivyo niliposhika mimba yako alilaani hicho kitendo ndo mana hata ulipozaliwa alikufanyia yale"

Hapo nikawa nimeelewa kwanini bibi alikua ananichukia. Nimemsamehe lakini naendelea kujifunza kumpenda na kua na furaha ninapokua karibu nae.

Kama nilivyomuhaidi likizo nitaenda kumuona😂 Ijumaa nitaenda nitamfungia mazagazaga nimpelekee bibi yangu mpendwa.

MWISHO.
 
Back
Top Bottom