Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 20,925
- 30,273
Ilikuwa wakati Nyerere yuko Musoma ndipo John Hatch kutoka Chama cha Labour cha Uingereza alipokuja Tanganyika kama mgeni wa TANU.
TANU ilifanya mkutano mkubwa sana Mnazi Mmoja na Hatch akawahutubia wananchi.
Inakisiwa takriban watu 20,000 walijitokeza kwenye mkutano huo. Ali Mwinyi Tambwe alikuwa mkalimani wa Hatch.
Denis Phombeah pamoja na Katibu mkuu wa TANU, Oscar Kambona vilevile walihutubia halaiki ile.
Hii kutanguliza ‘’Bibi’’ kabla ya jina la Titi mtu wa kwanza kulisema kwa msisitizo alikuwa Oscar Kambona katika mkutano mmoja wa kuwavuta wanawake waiunge mkono TANU.
Hatch akiwa anaunga mkono ukombozi wa watu weusi aligundua kuwa TANU haikuwa na tawi la akina mama.
Katika dhifa ya chai iliyoandaliwa na TANU kwa heshima yake, Hatch alilieleza tatizo hili kwa Schneider Plantan na John Rupia.
Hatch alimwambia Schneider kwamba ili kuwa na chama chenye nguvu TANU isiwaache akina mama nyuma.
Hatch alimwambia Schneider kwamba huko Uingereza Chama cha Labour kilikuwa kimejikita kwa wanawake kama moja ya nguzo yake kuu.
Schneider alimwendea Bibi Tatu binti Mzee akamwomba kuanzisha tawi la akina mama kwa ajili ya TANU.
Bibi Tatu binti Mzee alimpendekeza Bibi Titi Mohamed ndiye afanye kazi hiyo kwa sababu ya tabia yake ya ucheshi na kupenda kuchanganyika na watu na ukweli kwamba toka hapo alikuwa mwanachama wa ‘’Bomba Kusema,’’ chama cha akina mama wa mjini Dar es Salaam.
Scheneider akamfuata mumewe Bibi Titi Bwana Boi Suleiman kumuomba mkewe ajiunge na TANU.
Hivi ndivyo Bibi Titi alivyojiunga na chama cha TANU.
Inasemekana kuwa kama nafasi ile ingempita Bibi Titi basi ingechukuliwa na Bibi Halima bint Khamis ambao wote wawili walikuwa na vipaji sawa katika kushawishi na fasaha ya uzungumzaji.
Mwalimu Nyerere na Bi. Halima Khamis, Dimaond Jubilee Hall, 1990