Bajeti 2008/09: Mambo Magumu!
2008-06-11 18:01:14
Na Sharon Sauwa, Jijini
Wakati Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi, Mhe. Mustafa Mkulo akitarajiwa kuwasilisha bajeti ya mwaka 2008/09 katika mkutano wa 12 wa Bunge kesho, bei ya vitu imepanda maradufu kulinganisha na kipato na hivyo kuwafanya wananchi wengi kuwa na maisha magumu zaidi.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa gazeti hili katika baadhi ya maeneo Jijini, umebaini kuwa bei ya bidhaa na huduma mbalimbali muhimu zimepanda mno na hivyo Serikali, kupitia kwenye bajeti yake itakayotangazwa kesho, kuwa na changamoto ya kulainisha makali hayo ya maisha kwa wananchi wake ambao yenyewe inataka wawe na maisha bora.
Mwandishi amebaini kuwa mbali na pesa nyingi wanazolipa wakazi wa Jijini kutokana na kupanda kwa gharama za usafiri, pia vyakula, huduma za matibabu, umeme na hata vifaa vya ujenzi vimepanda mno kwa namna inayofanya maisha yawe magumu zaidi.
Wakati nauli ya daladala ikiwa shaghalabaghala na kutozwa kati ya Sh. 250 hadi Sh. 1,000 kulingana na eneo na umbali wa safari yenyewe, katika baadhi ya maeneo mengi Jijini, unga wa mahindi huuzwa kati ya Sh. 700 hadi 800 kwa ujazo wa kilo moja.
Mwandishi wa Alasiri amebaini kuwa mchele huuzwa kati ya Sh. 900 hadi Sh. 1,300, maharage Sh. 1,200 hadi Sh. 1,500 huku kipimo kimoja cha mkaa kikiwa kati ya Sh. 700, 1,000 na hadi Sh. 1,200 kwa maeneo kama ya Kimara Bonyokwa.
Aidha, mwandishi amebaini kuwa bidhaa nyingine zilizo katika bei ya juu ni vitunguu na nyanya ambavyo vyote, huuzwa kwa wastani wa Sh. 100 kwa kimoja, au Sh. 400 kwa fungu lenye nyanya tatu hadi nne au vitunguu vya idadi hiyo huku fungu la bamia likiuzwa kati ya Sh. 100 na 300.
Hata hivyo, bei ya nyama ya kawaida imekuwa kimbilio la wengi kwa sasa, kutokana na ukweli kuwa yenyewe imeendelea kuuzwa kwa wastani wa Sh. 2,800 hadi 3,500, kulingana na eneo.
Sukari nayo huuzwa kwa Sh. 1,000 hadi Sh. 1,200 kwa kilo, mafuta ya kula huuzwa Sh. 150 kwa kipimo kidogo kabisa kwenye maeneo kama ya Tandale na Buguruni huku fungu la bamia ni sh 100.
Mwandishi amebaini vilevile kuwa bei ya samaki imekuwa haishikiki, ingawa hushuka kidogo pale wanapovuliwa kwa wingi wakati bahari inapotulia na giza kutawala usiku.
Bei ya dagaa wanaopendwa zaidi toka Kigoma huuzwa kwa kati ya Sh. 7000 hadi sh 9,000, nanasi Sh.1,000 na 1,500, embe dodo sh. 500 hadi 700 na machungwa Sh.100 hadi 150.
Aidha, bei ya maji yanayouzwa kwenye madumu katika maeneo yenye shida ya maji huuzwa kwa kati ya Sh. 300 hadi Sh. 500 kwa dumu moja la lita 20.
Nayo bei ya mafuta ambayo hutajwa kuwa ni sababu kubwa zaidi ya kupanda kwa maisha imeendelea kupanda siku hadi siku ambapo sasa, katika baadhi ya vituo vya mafuta, dizeli huuzwa kwa Sh. 1,950 kwa lita, Petroli Sh. 1850 na mafuta ya taa Sh. 1,300.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizopo, ni kwamba kupanda kwa bei ya mafuta kunachangiwa pia na bei yake katika soko la dunia.
Kwa mujibu wa mwelekeo wa bajeti ya 2008/2009 uliotolewa na Waziri Mkullo, Serikali haitarajii kuongeza ushuru wa mafuta ya dizeli na petroli.
Walipoulizwa kuhusiana na maoni yao ya kupanda kwa gharama za maisha kusikoendana na kipato, baadhi ya wabunge wamekaririwa na vyombo vya habari wakisema kuwa watashupalia sula hilo baada ya kutangazwa kwa bajeti hiyo kesho.
SOURCE: Alasiri