Bajeti ya Serikali 2008/09 - Exclusive Thread

jmushi1

jmushi1

JF-Expert Member
22,306
2,000
CCM na ufisadi ndoa yao itadumu milele!

Deus Bugaywa

NI wazi sasa kwamba kile kinachosemwa kuhusu CCM na hatima yake kutokuwa ya kutia matumaini si tena habari za mitaani, ni suala ambalo liko wazi na dhahiri hata kaka wenye chama chao hawataki kuuikiri ukweli huo.
Na zaidi sana kutokiri kwao kwamba mambo si shwari ndani ya chama chao ni moja ya dalili za wazi kwamba huu ni mwanzo wa mwisho wa chama hicho kikongwe katika historia ya siasa ya nchi hii na bara la Afrika.
Ukiangalia kwa makini taarifa zilizotolewa katika vyombo mbalimbali vya habari tangu kuanza kwa kikao kinachoendelea cha Bunge na fununu kwamba kwamba lipo kundi la wanachama wakongwe wa chama hicho waliokuwa na mkakati wa kushawishi wabunge wa chama hicho wawasafishe watuhumiwa wa Richmond.
Pia kuibuka kwa tuhuma za ushirikina bungeni na yaliyojiri kwenye kikao cha NEC ya CCM na wabunge wake, na habari zilizoandikwa kama matokeo ya kikao hicho, haihitaji kuwa Thomaso kujua kwamba uko mkono unaoiandikia CCM ukutani kwamba ‘Mene mene tekeli na peres’ yaani ufalme wake sasa umekwisha.
Baada ya kikao cha NEC na wabunge kila aliyekuwa na shaka na ukali wa wabunge wa CCM wakati wa kujadili ripoti ya kamati ya Mwakyembe sasa amethibitihsa hofu yake hiyo, kwamba hizo zilikuwa ni mbio za sakafuni ambazo mkiambiaji wake hata awe na kasi kama ya mwanga, jeuri yake inaishia ukingoni - haifiki mbali.
Msomaji mmoja wa safu hii aliwahi kuniandikia wakati wa vurugu hilo lililosababisha waziri mkuu wa wakati huo kujiuzulu kwamba ‘ndugu mwandishi hiki kinachosemwa na wabunge wa CCM sasa ni ngoma ya watoto haikeshi, ufisadi siku hizi ndiyo mhimili wa CCM, kujidai wanaupiaga vita ni kama wanajipiga vita wenyewe, wataweza?’ Wakati huo nilimwambia kila kitu lazima kiwe na mwanzo na mapinduzi yanapoanza huwa kuna mstari mwembamba sana katikati ya hali ya zamani iliyozoeleka na hali mpya ya kimapinduzi inayoanza kuzaliwa, kiasi kwamba unaweza usione tofauti, kwa hiyo huo huenda ukawa mwanzo wa CCM kujivua gamba lake.
Kokote aliko msomaji huyu najua wala hakushangaa kusikia matokeo ya kikao cha chama kinaamua kurejea kwenye jadi yake na kuwatakasa watuhumiwa wa ufisadi, kwamba kuitengeanisha CCM na ufisadi unaoendelea nchini ni kazi kubwa.
Tunaambiwa hata wale ambao tuhuma zao wala hazihitaji kuwa mhitimu wa kilichokuwa chuo cha kijasusi cha Patrice Lumumbe huko Urusi, kujua kwamba kulikuwa na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kukiuka maadili ya kawaida kabisa uongozi.
Na hapo ndiyo ule mwisho unapokaribia, kwamba kikao hicho kama vilvyokuwa vilivyotangulia vilivyokuwa na lengo la kuleta mshikamano katika chama, kimesaidia kuongeza uadui miongoni mwa wanachama wake wakongwe na viongozi waandamizi kiasi kwamba nyufa zilizopo sasa sina shaka hata mweyekiti wake, Rais Kikwete, anaweza kuzuia zisiendelee kukua na kupanuka achilia mbali kuziziba kabisa.
Inapofika mahali chama kikongwe chenye viongozi wazoefu, kama viongozi wake wa ngazi ya mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama ya taifa, anamwambia Spika wa Bunge lenye wabunge wengi wa CCM na Spika huyo anatoka CCM, kwamba ni mzushi anaongoza Bunge kizushi, ujue anguko kuu haliko mbali.
Na hizi tunazoziona hadi huku nje ni ishara chache tu kwamba sasa hivi kuna CCM mbili, bila kujali wennyewe wanafunika kombe vipi, hata kama watasingizia kwamba ndio kukomaa kwa demokrasia, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba mambo ndani ya chama hicho yanakwenda msege mnege.
Kama tulivyojuzwa na vyombo mbalimbali vya habari kwamba pamoja na mvutano uliotokea ndani ya kikao hicho cha NEC na wabunge juu ya nini chama kifanye kwa watuhumiwa wa ufisadi, na mwenyekiti kuishia tu kutoa kauli laini ambazo kila kundi linaitafsiri kwamba ilikuwa ni kijembe kwa upande mwingine, si ishara nzuri ya kiuongozi, hii inatoa mwanya kwa watu kuanza kuamini kwamba hata mwenyekityi wake sasa kuna watu au kundi analoliogopa ndani ya chama.
Hakuna ubishi kwamba kusafishwa au (kujisafisha?) kwa watuhumiwa wa kashfa za Richmond na EPA ndani ya CCM, si suala ambalo limekuja kibahati bahati, huo ni makakati ambao umeandaliwa na wahusika siku nyingi, kwa ujuzi mkubwa na gharama kubwa.
Kwa hiyo, ndiyo kusema kwamba CCM mengine ya chama hicho sasa hayategemei sana itikadi yake na mfumo wake wa kutendaji au kimaadili, isipokuwa ujanja wa baadhi ya wanachama wake wanaoweza kufanya ‘maarifa’ na kuwafanya wajumbe wawaunge mkono katika kile wanachokitetea hata kama kinasigana na maadili na miongozo ya chama hicho.
Wanaoshinda kwa ‘mbinu’ na maarifa yao katika hoja moja wanatoa mwanya kwa kundi lililoshindwa nalo kujiandaa na kupanga mikakati ya kuja kuwapiku wengine, ilimradi ni mashindano ya madaraka na kunyemelea nani atakuwa mpangaji anayefuata wa mambo pale Magogoni.
Kwa kufanya hivi viongozi wa chama hiki wamewasahau wananchi, wako bize wanapigana vikumbo vya kuwania ukubwa, katika vikao vyao vingi vya hivi karibuni kwenye kila hoja nyeti, mwananchi na mwanachama hana nafasi ukisikia ametajwa ni katika hali ya kujihami kwamba ‘wananchi wameamka’ kwa hiyo mwaka 2010 chama kinaweza kuwa na kazi kubwa kushinda.
Kusahauliwa huku kwa wananchi ndiko kunakopaswa kutumiwe na Watanzania kuona na kukijua hasa chama hiki kinachoitwa cha mapinduzi, kina sura gani na viongozi wake wana mweleko na malengo gani na watu wa taifa hili.
Kwa kuamua kuwakumbatia mafisadi, CCM inatuma salamu kwa wananchi kwamba chenyewe kinaangalia watu wake kwanza, ikumbukwe CCM ina wenyewe na wenyewe ni wao, na chama hakiko tayari kuwaona ‘wanapata tabu’ hata kama wanatuhumiwa na nini.
Ni jukumu la wananchi kuamua kusuka au kunyoa - chama ndiyo hivyo kimeamua kufunga pingu za maisha na ufisadi, kwa kwamba yaliyounganishwa na NEC, wananchi kwa maana ya Bunge lao lisiyatengue.
Mbele ya CCM hata Bunge si lolote si chochote, kwamba hata kama Bunge limejiridhisha kwamba kweli hawa ni watuhumiwa, lakini kwa kuwa wanachokifanya ni kile kinachoitikadiwa na chama chao, acha Bunge lisema na ‘lizushe linavyoweza kuzusha’, lakini ndoa ya CCM na watu wake hata kama ni watuhumiwa hawana ruksa kuivunja.
Chama (kipande kimoja cha chama) ndiyo hicho kimeamua kuchukua ufisadi, je, kundi la wakereketwa linalodhani mwenendo wa mambo ndani ya chama hicho si wenyewe litakwenda njia ipi? Ni suala la kusubiri na kuona.
Lakini kitu kimoja ni dhahiri kwamba kwa kila kitendo na kila neno wanalosema CCM linashabikia mtu ambaye machoni pa umma anaonekana hana sifa hata za kuwa balozi wa nyumba kumi, kwa kukosa nidhamu na uadilifu wa kiuongozi, ni hatua moja ya taratibu lakini yenye nguvu na ya uhakika kuelekea kwenye kaburi lake.
Mungu ibariki Tanzania!
drbugaywa@yahoo.com
0734 449 421
 
jmushi1

jmushi1

JF-Expert Member
22,306
2,000
Usafi wa Lowassa, uchafu wa CCM

Ansbert Ngurumo

STAILI ambayo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetumia kujisafisha inavutia, inashangaza, inachekesha na kutafakarisha kidogo. Ni staili inayozua maswali yasiyo na majibu au yenye majibu yasiyoridhisha.
Lililo dhahiri ni kwamba, kwa kitendo cha kujisafisha, kwa kutumia kikao cha Halmashauri Kuu (NEC), CCM imekiri kile ilichokuwa inakikataa kwa muda mrefu - kwamba imechafuka.
Lakini staili yake ya kujisafisha inatufanya tuhoji upya: Uchafu ni nini? Umeingiaje CCM? Umeingizwa na akina nani? Umeingia lini? Na unaondolewaje? Labda CCM wangejiuliza maswali haya na kuyatafutia majibu ya kina, wangepiga hatua kidogo.
Majibu ya maswali haya yanatosha kuandika kitabu ambacho kitaandikwa siku moja na kuwa marejeo ya vizazi vijavyo kuhusu historia ya ukombozi wa nchi hii kutoka mikononi mwa wakoloni weusi waliojipa haki ya kutafuna matunda ya uhuru wa Watanzania bila ridhaa yao.
Ikumbukwe kwamba zilipoibuliwa tuhuma dhidi ya CCM, hadi baadhi ya watani wake kisiasa wakakiita Chama Cha Majambazi; Chukua Chako Mapema; Chama Cha Majangili; Chama Cha Mafisadi na kadhalika. Viongozi wakuu wa wanachama walipinga, waling’aka, kuwakebehi na hata wakawatisha waliotoa tuhuma hizo.
Katika hali ya kutapatapa na kukata tamaa, na kama ilivyo kawaida ya CCM kufanya propaganda katika masuala ya msingi, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alitamka hadharani kwamba tuhuma dhidi ya CCM ni kelele za mlango zisizoweza kumzuia yeye (akajiita mwenye nyumba) kulala! Wiki hii ni yeye aliyeongoza kikao cha NEC kujaribu kujisafisha, kwa staili aliyochagua yeye na viongozi wenzake. Viongozi wenzake, naye akiwamo, pamoja na wastaafu, wamefunikwa na kashfa nzito mno kichwani hadi miguuni.
Hawaonekani! Hata waliotishia kwenda mahakamani baada ya kuhusishwa na ufisadi wameshindwa kwenda kwa sababu dhamiri zao zinawaeleza ukweli kwamba hizi si kelele za mlango, bali sauti za wanyonge, wenye mali ya nchi hii, ambao hatimaye wamegundua mnyonyaji wao ni nani.
Watuhumiwa hawa wanaogopa yasifumuke mengine wakiwa kule mahakamani. Na licha ya ushahidi wote uliopatikana hata bila kwenda mahakamani, vyombo vya dola vimeshindwa kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa.
Polisi wetu wameamua (bila shaka kwa maagizo ya kisiasa) kufanya kazi ya kisiasa. Wanakimbizana na vibaka na wezi wakuu mitaani; wanawabambikia kesi wananchi maskini wanaotafuta kwa jasho. Wakati mwingine wanawanyonga ili kuwanyang’anya walicho nacho.
Wanashindwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale wanaotuhimiwa kwa wizi mkubwa unaofilisi hata maisha binafsi ya polisi wenyewe. Maana kama watuhumiwa walishindwa kwenda wenyewe mahakamani kuwashitaki waliowatuhumu, Jeshi la Polisi lingetusaidia kwa kuwakamata watuhumiwa ili haki itendeke.
Kimsingi, hata wanasiasa makini wanaotaka kujisafisha matope ya ufisadi, walio na dhamiri ya kuonyesha kwamba hapa kuna ari mpya, wangepaswa kuchukua hatua za kisheria ili kujisafisha au kuwasafisha watuhumiwa au kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria.
Huo ndiyo ungekuwa usafi wa CCM na serikali yake. Hapo ndipo rais angeanzia kuisafisha na kuwasafisha wenzake. Angechanganya hatua hiyo na zile fursa kadhaa zilizojitokeza, akabadilisha sura na mfumo wa utawala; akaondoa wachafu na kuweka wasafi; akafukuza wazembe na kuingiza wachapakazi.
Angepata pa kuanzia upya; na tungemsikiliza. Mara zote alizobahatika kufanya mabadiliko madogo na makubwa katika Baraza la Mawaziri zilikuwa fursa muhimu za kutuonyesha nia yake ya kusafisha serikali na CCM. Alishindwa kuzitumia.
Akawahamisha mawaziri kutoka wizara moja hadi nyingine; akawapunguza wachache wasio na tuhuma nyingi; akawabakiza wale wanaotuhumiwa kila siku. Ni sawa na mtu anayefagia nyumba yake halafu akakusanya uchafu wote akaulundika chumbani anakolala; kisha akawatangazia wana familia na majirani kwamba nyumba yake ni safi.
Harufu ya uchafu inayowakera hao, inamburudisha yeye, maana yeye na wao wana tafsiri tofauti ya usafi na uchafu. Tusisahau kuwa kabla aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu, rais alikuwa ameunda Tume ya Profesa Rwekaza Mukandala kumsaidia kuwachunguza mawaziri wake na kumpa ushauri juu ya nani mbovu, nani ana nafuu, nani aondolewe na nani abaki.
Kwa bahati mbaya, hakuunda tume kabla ya kuwateua, ili kubaini ubovu wao. Lakini wengi wa wateule wake ni wale ambao yeye na wao wamekuwa pamoja serikalini kwa zaidi ya miaka 17. Haiwezekani kwamba hakuwajua. Wala hakuhitaji ushauri wa tume.
Wananchi wenyewe walionyesha wasiwasi juu ya baadhi yao. Iweje wananchi wajue udhaifu wa mawaziri, yule aliyewateua, tena mwenye vyombo vya kiutawala vya kumsaidia kuwajua, ajidai kwamba hawajui hadi aletewe taarifa na tume ya ‘kisomi’! Ajabu ni kwamba, hata tume ilipoleta majibu, hakuyatumia. Akawateua wale wale, tena wengine wakamkejeli kwenye vyombo vya habari. Andrew Chenge ni mfano hai. Alipoteuliwa kuongoza Wizara ya Miundombinu, wanahabari wakamhoji kwanini amerudi akasema “muulize rais aliyeniteua. Ndiye anajua sababu.” Chenge alikuwa sahihi.
Na hata baadaye alipoondoka kwa kashfa za kuficha nje mabilioni ya shilingi ambazo hazijajulikana alivyozipata, alitoa kauli nyingine kwamba ameondoka ili kumwondolea ugumu rais. Maana yake, kama si kwa ajili ya rais, Chenge asingeondoka.
Lakini maana kubwa zaidi inayopatikana kwenye kauli yake ni kwamba kama asingeondoka, rais asingemfukuza! Kauli kama hii ilitolewa pia na Lowassa alipojiuzulu uwaziri mkuu, akasema amefanya hivyo si kwa kuwa ana mkono kwenye Kampuni ya Richmond, bali kwa kuwa alitaka kulinda heshima ya chama na serikali.
Baadhi yetu tuliandika kumsahihisha Lowassa, tukasema alijiuzulu kulinda heshima ya rais kwa kuwa wote walikuwa washiriki wakuu katika mradi wa Richmond. Kuna jambo lilitokea wakati ule ambalo lipo hadi sasa. Ile heshima ya chama na serikali haikurejea.
Kwa hiyo, kujiuzulu kwa Lowassa hakukusaidia kurejesha heshima ya serikali na CCM. Na sababu mojawapo iliyosababisha heshima hiyo isirejee ni kwamba mafisadi wale wale wameendelea kuwa viongozi wa CCM na serikali.
Wao walitaka tuamini kwamba fisadi ni Lowassa; akiondoka serikali inakuwa safi. Wapi! Sasa NEC ya CCM imekaa na kumsafisha rasmi Lowassa kwa kusisitiza kauli yake ya awali.
Maana yake ni kwamba CCM na serikali hii ya Kikwete inamhitaji sana Lowassa. Na imegundua kwamba inahitaji kumlinda. Inajua, kwamba tunavyojua, kwamba alipokuwa waziri mkuu, Lowassa hakutenda jambo lolote zito kwa uamuzi wake pekee.
Yote aliyatenda kwa idhini na ushauri wa rais. Ndiyo maana yalipomtokea yaliyosababisha ajiuzulu, rais alikuwa wa kwanza kumtetea, akasema amepatwa na ajali ya kisiasa; kwa kuwa Lowassa ni kiongozi mchapakazi, mwadilifu na mzalendo wa kweli.
Aliyasema hayo huku akijua kuwa umma wa Watanzania unamzomea Lowassa na kumwona fisadi wa kutupwa, maana katika sakata hili la Richmond, jina la Lowassa limetajwa mno kuliko hata la wamiliki halisi wa Richmond.
Hili ndilo ambalo CCM imejaribu kupambana nalo. Na kitendo cha NEC kumsafisha Lowassa sasa, ni uthibitisho kwamba CCM imesisitiza kauli ya Rais Kikwete juu ya ‘uadilifu na uzalendo’ wa Lowassa. CCM na Serikali ya Kikwete inamuogopa Lowassa. Na haikuanza leo.
Lakini woga huu uliongezeka pale walipoona Lowassa anawekewa zulia jekundu kwao Monduli! Woga ulizidi walipoanza kusikia akijitetea hadharani. Wakajua wasipofanya kitu, atalipuka na kulipua mambo. Wakaamua kumlipua yeye kwa njia mbili.
Kwanza, wakawa wanamtumia wajumbe wa kumpa pole na kumfariji kwa yaliyompata. Pili, walipogundua bado ana kinyongo na kwa hulka yake atazidi kusema mengine wasiyotaka aseme - maana alishaamua kujitetea asife kibudu - wakaingiza nguvu ya dola. Wakamuonya. Akaufyata! Hadi leo najiuliza. Kuna kitu gani serikali inaogopa kwa Lowassa? Kitu gani waliogopa asiseme? Na hapa walipofikia, inawezekana hatasema tena; maana wamemsafisha. Wamemziba mdomo.
Lakini usafi huu wa Lowassa una maana gani pana? Wamemsafisha Lowassa kumlinda mwingine. Na ulinzi huu ndiyo sababu ya NEC kuwatisha wabunge na kuwawekea ‘gundi’ mdomoni wasijadili masuala ya ufisadi wa EPA bungeni.
Huu ni uchafu ambao wakubwa hawataki kuondokana nao. Uchafu huu ndiyo asili ya nyadhifa zao. Uchafu huu ndiyo ulaji wao. Ukizungumzwa kwa uwazi, ukaanikwa, hakuna mmoja wao atakayebaki. Hakuna atakayemfukuza mwingine. Na ndiyo maana wamekuwa wakilindana na kuogopana hata mambo yanapokuwa yameharibika waziwazi.
Na ndiyo maana wengine tunatilia shaka hizi harakati za CCM na serikali kujisafisha kwa kuwatoa kafara wachache na kuwakumbatia wengi. Wanataka kutumia ‘usafi’ wa Lowassa kuisafisha CCM na serikali. Lakini wanashindwa kuchukua hatua za dhati kwa mafisadi wa EPA.
Hakuna atakayewaelewa. Hata Richmond (sasa Dowans) bado inaendelea kulipwa mamilioni wasiyostahili (sh 152,000,000 kila siku). Matendo haya ya NEC huku serikali ikishindwa kuchukua hatua dhidi ya mafisadi, ni sawa na CCM kujisafisha kwa kunawa matope. Sote tunajua matokeo yake.
Inavutia kufuatilia mchakato wa namna hii; inashangaza CCM wasivyojua maswali ya msingi yanayowakabili; inachekesha kwamba watawala wameamua kufanya maigizo mbele yetu; na inatafakarisha kwamba vita dhidi ya ufisadi inahitaji watawala mbadala na vyombo mbadala. Si hawa tulio nao.

ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com
+447853850425
 
MwanajamiiOne

MwanajamiiOne

Platinum Member
10,476
1,225
Azimio Jipya hongera kwa kulitoa dukuduku lako. Ni kweli kabisa wanatunyanyasa kwa hii misaada yao. Ni wajanja hawa nanatafuta maeneo yale ambayo yanawagusa moj akwa moja ndio wanajidai tuyarekebishe kwanza kabla ya kutupa misaada yao. Wanajitia hawatoi mpaka turekebishe au tuwe na good governance je huko nyuma walipokuwa wanatusaidia tulikuwa na good governance? au wameona nasi tumecharuka tunawadai rushwa mpaka wao na wanaumia ndo maana wanataka tujirekebishe ili wavune ipasavyo?

Mimi hata siku moja simwamini Mzungu na misaada yake, they always come with strings attached ...... si umasikini tena unaotufanya tudhalilishwa na vimisaada vyao bali ni uroho wa baadhi ya viongozi wetu ndo maana tunajikuta tunaingia katika mikataba uchi na hawa mafisadi... hakika wanastahili kuitwa mafisadi weupe shwaiiin
 

Forum statistics


Threads
1,424,986

Messages
35,078,036

Members
538,184
Top Bottom