Hii ni nchi yenye dola iliyo tayari kujeruhi na kuua raia katika masuala ya kisiasa. Mifano ipo ya kutosha. Ningeshangaa sana kama CHADEMA wangeshikilia msimamo wa kuandamana kesho. Kuna mambo sikubaliani nao LAKINI, hadi sasa, naiona CHADEMA kuwa chama pekee Tanzania chenye watu wenye jeuri dhidi ya utawala wa mabavu wa serikali ya CCM.
Ni dhahiri kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kufikia bei ya watu kama Mbowe, Lissu, Mnyika, Lema, Mdee, Sugu, n.k. CHADEMA inajengwa na watu wasiolingana na "stereotype" ya Watanzania wengi; ya kunyenyekea watawala kupita kiasi kwa ajili ya maslahi binafsi. Inavyoonekana serikali na CCM wanatikiswa sana na harakati za CHADEMA kwani hawajui jinsi ya kuwadhibiti zaidi ya kulilia "tishio dhidi ya amani" na kuamrisha polisi na, sasa, jeshi kujiandaa kupiga/kuua yeyote anayeshiriki harakati za CHADEMA. Kwa mazingira tuliyo nayo, nje ya CHADEMA, tunao mbadala upi wa kuiweka sawa serikali angalau iwe na adabu kidogo?