Serikali sasa kuwajengea Wamachinga jengo la kisasa
. Litawakusanya wote katika sehemu moja
. Litachukua wafanyabiashara zaidi ya 10,000
. Barabara ya Kawawa kupita chini yake
Na Joseph Lugendo
BAADA ya kufanikisha kuhamisha Wamachinga kutoka katika maeneo yasiyoruhusiwa jijini Dar es Salaam, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imekamilisha michoro ya ujenzi wa jengo kubwa la biashara la kisasa kwa ajili ya kuwapangisha wafanyabiashara hao.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bw. Adam Kimbisa wakati alipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia ujenzi huo.
Kwa mujibu wa Bw. Kimbisa, jengo hilo litakuwa na uwezo wa kupangisha Wamachinga zaidi ya 10,000 na kwamba ujenzi wake utagharimu kiasi cha sh. bilioni kumi.
Jengo hilo lenye ghorofa tano, limepewa jina na Business Park na litajengwa katika makutano ya barabara za Lindi na Kawawa nyuma ya Uwanja wa mpira wa Karume, Ilala jijini.
Mchoro wa jengo hilo uliooneshwa jana kwa wanahabari na Bw. Kimbisa, umechorwa na mtaalamu wa michoro wa NSSF Bw. Deo Mponeja na unaonesha kwamba barabara ya Kawawa itapita chini ya jengo hilo.
"Jengo hili litakuwa moja ya vivutio vya utalii, tena litakuwa kimbilio la wateja kwenda kujipatia mahitaji mbalimbali wakiwa Dar es salaam." Alisema Bw. Kimbisa
Alisema kwamba ujenzi huo umepata baraka ya ya Rais Jakaya Kikwete na kwamba Serikali kuu imetoa dhamana kwa Halmashauri hiyo ili iweze kukopa fedha kutoka NSSF kwa ajili ya ujenzi huo.
"Ujenzi utaanza mwishoni mwa Desemba mwaka huu au mwanzoni mwa Januari mwaka ujao na utakamilika baada ya miezi kumi na mbili," alisema Bw. Kimbisa
Alisema kwamba wataalamu wa Halmashauri hiyo akiwemo mchoraji wa jengo hilo, walitembelea katika nchi za China na Malaysia ambapo walikuta Wamachinga wa huko wakifanya biashara zao lakini kwa kufuata utaratibu katika majengo kama hayo.
"Hakuna Serikali ya kidemokrasia duniani ambayo inataka wananchi wake wapate shida ndio maana Serikali ilitoa muda wa miezi sita ili Wamachinga wote waweze kuhama wenyewe kutoka maeneo yote wasiyoruhusiwa," alisema Bw. Kimbisa.
Alisema kwamba shunguli ya kuondoa Wamachinga ilifanyika kwa manufaa yao wenyewe na wananchi kwa ujumla na kwamba kazi ya kufikiria jinsi ya kuwahamisha na kuwawezesha, ilimsababishia vidonda vya tumbo.
Kuhusu kuwezeshwa kwa Wamachinga hao, Bw. Kimbisa alisema kwamba wote wataorodheshwa katika maeneo wanaofanyia biashara na kwamba orodha hiyo ndiyo itakayotumika kuwapangisha vyumba vya biashara kwa bei nafuu mara ujenzi utakapokamilika.
"Huwezi kumkopesha mtu ambaye hana mahali maalumu pa kufanyia biashara tena, hata benki zinaogopa kuwawezesha," alisema Bw. Kimbisa na kuongeza kwamba jengo hilo litakuwa na sehemu maalumu itakayopewa benki itakayoonesha kwamba itawawezesha Wamachinga hao.
Alisema kwamba amezungumza na baadhi ya kampuni za bima ambazo zimemuahidi kuipatia benki hiyo bima kwa ajili ya kulipa fedha ambazo zitapotea kama watashindwa kulipa mikopo wakiwa katika jengo hilo.
Bw. Kimbisa alisema kwamba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo na kuwapangisha Wamachinga, wataendelea na ujenzi wa majengo mengine kama hayo katika kila wilaya ya jiji la Dar es Salaam.
Aidha, Bw. Kimbisa alisema kwamba Wamachinga hao watapewa mafunzo ili waweze kuhitimu kutoka kufanya biashara za kununua na kuuza mali na kuwa wafanyabiashara wanaozalisha na kuuza mali.
Hata hivyo, Bw. Kimbisa aliwaonya wafanyabiashara hao kutojaribu kurudi katika maeneo waliyoondolewa na kusema kwamba sheria kali zitatumika dhidi ya yeyote atakayethubutu kufanya hivyo.
Source: Gazeti la Majira
http://majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=1521