Anayedhani Mahakama za Tanzania siyo huru asome hii kesi

comte

JF-Expert Member
Dec 11, 2011
8,226
5,948
Mahakama yatengua makubaliano yaliyorejesha mali ya Ushirika serikalini
Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imetengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyohalalisha mkataba wa makubaliano baina ya Serikali na mfanyabiashara Amos Njile, kuhusu umiliki wa ghala la Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza, Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd (NCU).

Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na rufaa aliyoikata Njile akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Mwanza katika kesi ya ardhi namba 12/2018 iliyobariki makubaliano hayo yaliyoliweka ghala hilo katika umiliki wa Serikali kutoka kwa Njile aliyekuwa amelinunua kwenye mnada.

Ghala hilo lililoko kiwanja namba 104/1 kitalu A, eneo la Viwanda, Igogo jijini Mwanza ni miongoni mwa mali za chama hicho zilizorejeshwa na Serikali kutoka kwa watu mbalimbali waliokuwa wakizimiliki, kwa maelezo zilinunuliwa isivyo halali, vikiwemo viwanda, nyumba za kuishi na viwanja.

Mahakama ya Rufani katika uamuzi uliotolewa na jopo la majaji watatu lililoongozwa na Rehema Mkuye na wenzake, Winfrida Korosso na Othman Makungu, imesema makubaliano hayo yalikuwa na kasoro za kisheria zinazoyafanya yasiwe halali.

Mahakama baada ya kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi hiyo, imeelekeza uamuzi na amri ya Mahakama Kuu katika kesi ya awali aliyoifungua Njile, utekelezwe.

Katika uamuzi wa kesi ya awali ya ardhi namba 58/2015, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilielekeza ufanyike ukaguzi kuonyesha haki ya kila upande na kugawanywa kwa pande zote mbili.

Historia ya mgororo
Mgogoro wa umiliki wa mali za chama hicho likiwemo ghala hilo, unaanzia mwaka 2007.

Januari 7, 2007, Njile alinunua ghala hilo katika mnada wa hadhara ulioendeshwa na dalali wa mahakama, ukiwa ni utekelezaji wa tuzo ya kesi ya madai namba 45 ya mwaka 2003, baada ya kutupilia mbali rufaa aliyokuwa ameikata NCU.

Julai 9, 2013, Njile alipewa hati miliki ya ghala hilo namba 45296 iliyosajiliwa kwa jina lake.

Mwaka 2015 alifungua kesi Mahakama Kuu dhidi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, NCU, Kamishna wa Ardhi, Msajili wa Hati na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) baada ya kupokea taarifa ya kubatilishwa hati ya umiliki wa ghala hilo na Rais.

Katika kesi namba 58/2015, alikuwa akiiomba Mahakama itamke kuwa ndiye mmiliki halali wa ghala hilo.

Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Issa Maige, Novemba 30, 2017, iliifutilia mbali kesi hiyo ikaamuru mali hiyo yenye mgogoro ikaguliwe vizuri na ibainishe haki ya kila upande na kuigawanya kwa pande zote.

Desemba mwaka huohuo, alipata taarifa kuwa hati hiyo ilikuwa imefutwa, lakini alipofuatilia katika mamlaka husika akajiridhisha bado ilikuwa halali.

Baadaye wapangaji waliokuwa wamekodishiwa ghala hilo, walipokea barua kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza ikiwafahamisha ghala hilo halikuwa likimilikiwa na Njile tena bali NCU. Njile alielezwa hati ilikuwa imebatilishwa.

Januari 2018, Njile alialikwa kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu kujadili masuala yaliyokuwa yanahusiana na uuzwaji wa ghala hilo, uliofanyika jijini Dodoma.

Katika mkutano huo hati hiyo ilihojiwa na akaelekezwa kuikabidhi, ambayo wakati huo bado ilikuwa katika himaya ya mahakama iliyosikiliza na kutupilia mbali kesi ya msingi namba 58 ya mwaka 2015.

Pia katika mkutano huo, Njile alisaini hati ya iliyoitwa ‘Makubaliano ya Kurejesha Mali’ yaani ghala hilo, akiridhia kulirejesha katika umiliki wa Serikali bila fidia, huku Serikali ikiahidi kuwa haitamchukulia hatua za kisheria kuhusu uuzwaji wa ghala hilo.

Licha ya kusaini makubaliano hayo yaliyochukuliwa kuwa mkataba wa maridhiano baina ya pande hizo mbili, Njile kwa upande mmoja na Serikali kwa upande wa pili; baadaye alifungua kesi nyingine Mahakama Kuu.

Katika kesi ya ardhi namba 12/2018 aliyoifungua dhidi ya NCU, Donald Kusaya (Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo) na AG, Njile alikuwa anaomba mahakama itamke makubaliano ya mapatano ya Januari 15, 2018 baina yake na Serikali ya Tanzania ni batili tangu mwanzo na hayawezi kutekelezeka.

Pia aliomba amri kuwa yeye ni mmiliki halali wa ghala hilo, malipo ya Sh150 milioni kama fidia ya hasara halisi kwa mwaka kuanzia Januari 2018, malipo ya Sh2 bilioni kama fidia ya madhara ya jumla, fidia ya adhabu, riba ya kufaa na gharama za kesi.

Wadaiwa katika hati ya pamoja ya majibu yao kupinga madai hayo, waliomba Mahakama iitupilie mbali kesi hiyo na walipwe gharama. Pia itamke kuwa makubaliano hayo yalikuwa halali na ya kisheria na kwamba, NCU alikuwa mmiliki halali wa ghala hilo.

Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Agness Mgeyekwa Julai 30, 2019 iliwapa ushindi wadaiwa ikisema mkataba huo ulikuwa halali kwa kuwa pande zote ziliingia kwa hiyari kwa kuwa ulikuwa umesainiwa na pande zote na hapakuwa na ushahidi wa mdai kulazimishwa kusaini.

Pia iliamua kuwa kubatilishwa kwa hati ya mali na Rais, ilikuwa halali na mmiliki halali wa ardhi hiyo alikuwa Rais.

Rufaa Mahakama ya Rufani
Njile alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akiwasilisha sababu tano pamoja na mambo mengine, akidai mahakama ilikosea kuamua kuwa alisaini mkataba huo kwa ridhaa yake, na kwamba mahakama ilishindwa kutathmini ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama.

Wakati wa usikilizwaji rufaa hiyo, Njile aliwakilishwa na wakili Jamhuri Johnson na wajibu rufani waliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Solomon Lwenge akishirikiana na mawakili wa Serikali Sabina Yongo na Felician Daniel.

Wakili Jamhuri alisema kama mahakama ingetathimini mrufani alivyosafiri kwenda Dodoma, mazingira na dhamira nyuma yake, ingebaini hakusaini kwa ridhaa na kwamba hakuwa na shahidi na wakili wake alikataliwa kuhudhuria.

Alidai Njile kutakiwa kutokudai fidia yoyote katika mkataba huo ni kitisho na kwamba, mahakama ilikosea kuhamisha dhima kwa mrufani kuthibitisha kuwa kulikuwa na uhuru wakati wa kusaini makubaliano hayo.

Wakili wa Serikali Lwenge, akijibu hoja hizo pamoja na mambo mengine alidai makubaliano hayo yalikuwa halali.

Pia alidai si takwa la kisheria kuwa na mashahidi kwa kila upande na kwamba, mrufani alishindwa kuthibitisha kuwa hapakuwa na uhuru katika kusaini makubaliano hayo, huku pia akidai mahakama ilitathmini vema ushahidi kwenye kumbukumbu za mahakama.

Uamuzi wa Mahakama ya Rufani
Mahakama ya Rufani imesema haijashawishika kuwa mrufani kusaini tu mkataba bila kuwepo kwa ushahidi mwingine, kunathibitisha kulikuwa na ridhaa huru kwa upande wake.

“Hatujashawishika kuwa mrufani kwa ridhaa yake alikubaliana na masharti yote yaliyomo na kulikuwa na maridhiano kwa watia saini wote kuhusu maudhui na muktadha wa mkataba dhaniwa chini ya kifungu cha 10 na 13 vya Sheria ya Mkataba,” imesema sehemu ya hukumu.

Ikielezea sababu za kutokushawishika, Mahakama imekubaliana na hoja za wakili Jamhuri kuwa ni kutokana na mazingira ya mrufani kuhudhuria mkutano na Waziri Mkuu, Dodoma uliozaa makubaliano hayo na ushahidi wa Njile asiye mwanasheria kunyimwa fursa ya kuwa na wakili wa kumwakilisha katika mkutano huo.

Sababu nyingine imesema ni kutokuwa wazi kwa nini mkataba huo ulitolewa na Serikali wakati suala la umiliki wa mali hizo lilikuwa limeshaamuriwa kupitia hukumu ya Mahakama Kuu katika kesi ya ardhi namba 58/2015.

Vilevile imekubali kuwa mkataba huo unaonyesha ni wa upande mmoja, kwamba mrufani ndiye pekee anayeonekana kutoa au kuahidi na hapati chochote, mbali na kuthibitishiwa tu kutokuchukuliwa hatua za kisheria kwa suala linalohusiana na ununuzi wa mali hizo.

“Kwa hayo, ni msimamo wetu kwamba kama jaji Mahakama Kuu angezingatia kwa kina mazingira yanayaozunguka mchakato wa kusaini mkataba huo unaobishaniwa, kwa heshima na taadhima asingefikia uamuzi kama alivyofanya kwamba kulikuwa na ridhaa huru kwa upande wa mrufani,” imesema hukumu ya majaji.

“Mwisho wa uchambuzi, tunakubali rufaa na gharama kwa kiwango kilichobainishwa. Zaidi tunatengua hukumu na amri za Mahakama Kuu katika kesi namba 12/2018. Kwa kuondoa mashaka, wadaawa wenye masilahi wanaweza kuendelea na utekelezaji wa amri katika kesi ya ardhi namba 58/2015, kama wakipenda,” inaeleza hukumu.
 
Back
Top Bottom