All about Tanzania life/ Safari zangu kuizunguka Tanzania

Jul 6, 2023
23
28
Kati ya maamuzi magumu zaidi nionayo nimeweza kuyakabili na kuyafanya ni hili la kuweka uhalisia hapa. Habari na heshima kwenu wakuu na wadau wote wa Jamii Forums. Nimekuwa hapa kwa muongo mmoja na miaka miwili sasa. Kila nitakaposherehekea siku yangu ya kuzaliwa nitakumbuka pia siku na mwezi kama huo, miaka 12 iliyopita nilifungua account yangu ya kwanza Jf saa sita usiku baada ya kuifuatilia jamii forums kwa mwaka mmoja nyuma kama mgeni na sio mwanachama halisi.

Ilinigusa sana wakati huo. Nakumbuka nilianza kwa kupenda tu majina ya ajabu ajabu yanayotumiwa humu. Hapa Jf kuna vichekesho sana, nakumbuka Thread yangu ya kwanza kabisa member wa kwanza kabisa kutoa maoni yake (jina kapuni) aliandika hivi "Asubuhi andika fupi fupi, zingatia muda" na hadi leo sijui alikuwa anawahi wapi Ah ah ah wakati mwingine inavunja moyo na wakati mwingine kuujenga moyo wenye ujasiri wa ajabu.

Nimejifunza mengi sana hapa na nimeona mageuzi mengi, simulizi nyingi na habari nyingi ambazo kamwe nisingebahatika kuzisikia maishani mwangu. Kama kijana nashukuru kuyashuhudia haya katika kipindi cha maisha yangu. Ahsante kwa jitihada zenu nyote. Nilifanikiwa kuvunja rekodi yangu ndogo niliyojiwekea hapa. Nyuzi zangu tatu kati ya habari kadhaa nilizowahi kuchapisha naona zinasomwa na kutazamwa zaidi hadi hii leo. Kati ya siku nilizowahi kufurahi zaidi ni pale ndugu member mmoja maarufu sana hapa alipochangia wazo langu kwa kirefu, fikilia niambie kwa hapa JF pekee unaona hakuna watu wenye IQ kubwa Tanzania?

Haukuwa utashi wangu, kila kitu nilijifunza hapa. Thread zote tatu nashukuru zilikuwa matukio ya kweli na ziligusa sana maisha ya watu, na wakati mwingine mimi binafsi nikizipitia nakuta zinanigusa na kunikumbusha mbali, ahsanteni kwa maswali na maoni mengi kule. Naahidi nitazifufua na kuziweka hapa.

Kwasasa nimechoka kufanya sanaa ya uandishi niliojifunza hapa kwa miaka mingi kwa njia ya siri, nitamalizia muda wangu kwa uwazi na kuhamasisha watanzania kufanya utalii wa ndani. Tangu mwanzoni mwa mwaka 2014 sikuwahi kuwa na ndoto hii, miaka yote ya ulevi wa JF sikuwahi kuandika chochote ama kuchangia mawazo yoyote kuhusiana na masuala ya utalii. Zaidi zaidi nilizungumzia ubunifu katika teknolojia na simulizi za kweli za safari na matukio ya kweli mahali pasipojulikana, pia ulevi na starehe kidogo kama vile watu wengi hapa wanavyopenda. Sikuwa mpenzi wa majukwaa ya siasa, utabibu au hata kule Chit chat.

Kwa sasa napenda kuanza safari nyingine mpya na ndoto yangu ni kukutana na watu wote muhimu hapa waliofanikiwa kubadilisha maisha ya watanzania wengi bila wao kujijua. Nimeanza kutembelea sehemu kadhaa ndani ya Tanzania na natumaini nitakuwa natoa mawazo na taarifa ya vipi unaweza kuyafikia maeneo hayo, ni ghalama kiasi gani kumudu kufanya safari kutembelea eneo la ndoto yako na namna ya kuweka pesa ya akiba kwaajiri ya matembezi na utalii wa ndani.

Jiulize hivi kwanini uzaliwe Tanzania kisha uje ufe huku hukuwai hata kuuona mlima Kilimanjaro kwa macho kweli?? Au ushindwe kufika pwani yoyote ya Tanzania na kugusa maji ya bahari ya Hindi?? Utakuwa mtu wa ajabu kukosoa mambo huku ukiwa umekulia sehemu moja hiyo hiyo na sasa unaelekea uzeeni.

Ni jambo la kujivunia kwako ikiwa utayafikia maeneo ya Tanzania japo nusu, kuijua mikoa yake na kukanyaga huko, kutembelea maeneo maarufu na kuona tamaduni mbalimbali kwa macho yako mwenyewe bila utegemezi wowote. Mimi naamini unaweza na inawezekana kwa kila mtanzania kuifahamu nchi yake kona zote.

Ahsanteni na kuwa tayari kwa masimulizi na stori za kweli kabisa kuzunguka Tanzania.
 
Back
Top Bottom