Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ahojiwa na TAKUKURU

Status
Not open for further replies.

nyamadoke75

Member
Apr 1, 2020
86
280
Mrisho Gambo ambaye ametumbuliwa nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, anahojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), JAMHURI limebaini.

Juni 19, mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Gambo na wenzake wawili - Gabriel Daqaro, na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk. Maulid Madeni.

Wakati akimwapisha mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Rais Magufuli, aligusia sababu za kuondolewa viongozi hao, na miongoni mwa hizo ni undumilakuwili na fitna za Gambo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa siku chache baada ya Gambo kutumbuliwa amehojiwa na TAKUKURU. Tofauti na tuhuma nyingine zinazomkabili, zikiwamo za ufisadi, kuhojiwa kwake kumetokana na tuhuma za kugawa rushwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chamna Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Arusha wanaohusika kupitisha jina la mgombea ubunge.

Kwa muda mrefu amekuwa na matamanio ya kuwania ubunge jijini Arusha, akiwa anapambana kuhakikisha jimbo la sasa la Arusha linagawanywa na kuwa majimbo mawili. Kuna madai kuwa kwa kuamini Jimbo la Arusha litagawanywa, alihakikisha eneo la Muriet anakoishi kunajengwa miundombinu ya barabara, maji na umeme ili kuwavuta wapigakura.

Jimbo la Arusha linaongozwa na Mbunge wa CHADEMA, Godbless Lema kwa miaka 10 sasa.

Hali ilivyokuwa
Hapana shaka kuwa pamoja na sababu nyingine, uamuzi wa Rais Magufuli, kumwondoa Gambo na kisha kuwakemea viongozi wengine wa vyombo vya usalama, umetokana na kitendo cha wao kumtumikia Gambo kwenye harakati zake za kuwania ubunge.

Vyanzo vya habari vya uhakika vimeliambia JAMHURI kuwa Gambo aliwatumia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, na aliyekuwa Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Frida Wikesi, katika kuhakikisha anakutana na wajumbe wa CCM na kuwapa fedha kwa ahadi kuwa hawatakamatwa.

“Kukawapo kauli kwamba pokeeni fedha bila wasiwasi kwa sababu haya ni maelekezo kutoka juu (kwa Rais Magufuli). Tukawa tunaambiwa Rais anamtaka awe mbunge wa Arusha kwa hiyo msiwe na wasiwasi,” amesema mmoja wa watoa taarifa wetu.

Katika tukio moja, Gambo alitumia basi la swahiba wake (namba tunazo), mmoja wa wamiliki wa shule binafsi mkoani Arusha (jina tunalihifadhi kwa sasa), kuwakusanya wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo.

Gari hilo liliwapeleka wajumbe hao katika makazi ya Mkuu wa Mkoa (Ikulu Ndogo) Arusha, na hapo mazungumzo yalifanyika na kisha wajumbe wakagawiwa fedha kwa uangalizi wa polisi mkoa na maofisa wa TAKUKURU.

“Tuligawiwa Sh 50,000 kila mjumbe, tena utashangaa fedha tulikuwa tunapenda na ofisi wa polisi huku TAKUKURU wakishuhudia.

Alishawaaminisha kuwa yeye ana Baraka zote za Rais Magufuli, lakini baada ya kumtumbua tukajua alikuwa anamsingizia Rais wetu,” amesema mmoja wa wanufaika wa tukio hilo.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa hadi anatumbuliwa, Gambo akishakutana na wajumbe wa kata 11 kati ya kata 25 za Jimbo la Arusha. Kata ya mwisho kwenye mkakati wake huo ilikuwa ya Moshono.

Kwa sasa kiongozi huyo hapatikani katika simu za kawaida, isipokuwa kupitia WhatsApp, mmoja wa marafiki zake aliozungumza nao amesema, “Yeye kasema atagombea tu hata kama amefukuzwa ukuu wa mkoa. Anasema atagombea hata kama ni kukatwa, basi akatwe maana tayari ameshaukosa ukuu wa mkoa, anajiamini kweli kweli,” kimesema chanzo chetu.

Lakini taarifa zilizozagaa katika viunga vya CCM Mkoa wa Arusha zinaonyesha kuwa Gambo amekuwa akiwahadaa baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho kwa kuwambia kuwa ameondolewa kwenye ukuu wa mkoa ili agombee ubunge Jimbo la Arusha.

“Anasema ameombwa atoke kwenye ukuu wa mkoa ili agombee ubunge na atakuwa waziri katika serikali ijayo, ndivyo anavyowambiwa wana CCM,” kimesema chanzo chetu.

Kwa muda wote, pamoja na kutumia magari ya rafiki yake kukusanywa wajumbe na kuwapeleka Ikulu Ndogo, Gambo amekuwa na ushirika wa karibu na baadhi ya viongozi waadamizi mkoani Arusha.

Miongoni mwa wanaotajwa ni mbunge mmoja wa viti maalumu, mmiliki wa shule mwenye jina linaloishia herufu ‘N’, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya moja ya kimkakati mkoani Arusha, mmoja wa wabunge mwanaume kijana kutoka wilaya inayosifika kwa migogoro kati ya serikali na wafugaji mkoani Arusha, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) ya moja ya wilaya za kimkakati mkoani Arusha. Majina yao tunayahifadhi kwa sasa kwa sababu za kitaaluma.

Baadhi ya makada na viongozi kadhaa wa CCM wamemtaka Gambo asithubutu kuchukua fomu.

“Ndoto zake za kuwania ubunge Arusha zilishayeyuka tangu alipotumbuliwa ukuu wa mkoa,” anasema mmoja kati ya wanachama maarufu wa CCM, Arusha mjini, Saidi Ndaki.

“Kwa sasa habari yake imekwisha. Hawezi tena kuwashawishi wanachama wamuunge mkono achukue fomu za kugombea ubunge. Wala sidhani, zaidi ya ukuu wa mkoa, kama alikuwa anakubalika ndani ya chama,” anasema.

Kada mwingine wa CCM ambaye kwa nafasi yake ya uongozi ameomba jina lake lisitajwe gazetini, anasema wakati Gambo akiwa madarakani, amesababisha mgawanyiko ndani ya chama.

Viongozi waliowahi kumnyooshea Gambo kidole ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula; Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

“Wala hakuwasikiliza, hapa Arusha kulikuwapo ugomvi wa mara kwa mara kati yake na viongozi wa chama. Yote hayo ilikuwa ni kuweka mazingira ya kuwa Mbunge wa Arusha hata kama hakubaliki.

“Tunamshauri kwa sasa anyamaze, atulie. Hana sababu ya kuja CCM mkoa kwa sasa. Atulie upepo upoe na labda baadaye anaweza kuomba uongozi, si kipindi hiki,” anasema kiongozi huyo wa CCM.

Kigezo cha kauli ya kada huyo ni kwamba kule tu kuondolewa kwenye uongozi na kiongozi wa juu wa nchi na kisha kuweka wazi sababu za kuondolewa kwake, kunamkosesha sifa mbele ya umma.

“Rais ametoa sababu za msingi na za maana kwanini amemtumbua, leo atawaambia au kuwashawishi nini wananchi na wanachama wa CCM Arusha?” anahoji.

Hii si mara ya kwanza kwa Gambo kutumbuliwa. Akiwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, alitumbuliwa na aliyekuwa Rais kwa wakati huo, Jakaya Kikwete.

Pamoja na tuhuma za ufisadi, Gambo analalamikiwa mno kwa vitendo vyake vya uonevu, kiasi cha kuwafanya wananchi kadhaa wateseke katika mahabusu mbalimbali mkoani Arusha.

Pia anatuhumiwa kwa uchonganishi na kutumia vibaya jina la Rais akilitumia kuwatisha watumishi wenzake kufanikisha mipango yake.

“Mara nyingi alikuwa akiwapigia simu au kuwafuata viongozi wa ngazi mbalimbali na kusema ana maagizo ya Rais. Watu wameumizwa sana na wengine wanaendelea kuteseka mahabusu kwa sababu ya fitna na ghiliba zake,” kimesema chanzo chetu.

Kutumbuliwa kwake kumeibua faraja kubwa kutoka kwa watu wa kada mbalimbali, wakiwamo wafanyabiashara ambao aliwabana kwa michango mingi ya fedha.

Mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Meja Jenerali John Mbungo, alisafisha ofisi ya taasisi hiyo mkoani Arusha. Frida Wikes aliyekuwa Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, alirejeshwa Makao Makuu, ilhali James Ruge ambaye alikuwa Ofisa Uchunguzi Mkuu-Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu –Makao Makuu amepelekwa Arusha kuwa Kaimu Mkuu wa TAKUKURU katika mkoa huo.

Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Siha, Deogratius Petera amehamishiwa Arumeru kuchukua nafasi ya Zawadi Ngallo aliyehamishiwa Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Arusha.

Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Monduli, David Shirima, anakuwa Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Siha. Naye, Mariam Mayaya ambaye alikuwa Ofisa Uchunguzi Mkuu Mkoa wa Arusha amehamishiwa Wilaya ya Monduli kuwa Mkuu wa TAKUKURU katika wilaya hiyo.

Rais Magufuli, wakati akiwaapisha viongozi, akiwamo Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Idi Kimanta, alieleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa wakuu wa TAKUKURU na Polisi mkoani humo, lakini akasema amewasamehe. Baada ya hapo Shana alihamishiwa Chuo cha Polisi Moshi.

Vituko vya Gambo
Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika baadhi ya visa vya Gambo vinavyosadikika kusababisha uamuzi wa Rais kumuondoa kwenye nafasi hiyo ilhali imesalia miezi minne tu kabla ya kipindi cha kwanza cha uongozi wa Awamu ya Tano kumalizika.

Gambo akiwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, alipandishwa cheo Agosti 18, 2016 kuchukua nafasi ya Felix Ntibenda. Bado wengi wanaamini kuondolewa kwa Ntibenda kulitokana na ‘fitna’ zilizosukwa na mrithi wake. Pia bado kuna wingu kubwa kuhusu uchomwaji moto wa shule mkoani Arusha, hali inayoelezwa kwamba ilichangia kuondolewa kwa Ntibenda.

Vituko vya Gambo vimeanzia mbali, kwani akiwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kabla ya kutumbuliwa, aliingia kwenye mgogoro na mwanasheria wa Halmashauri hiyo hadi wakafikishana Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Alipohamishiwa Arusha ni kama alikuwa amepania kwenda kuonyesha kiburi cha madaraka na mamlaka aliyokabidhiwa kwani alipofika tu alisikika akiwaeleza baadhi ya watu wake wa karibu wakiwemo waandishi wa habari kuwa amekwenda kuisambaratisha CHADEMA.

Gazeti la RAI la mwishoni mwa mwaka jana, liliandika habari za Gambo, likirejea hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa hospitali ya Mama na Mtoto kwa ufadhili wa taasisi ya Maternity Africa. Gambo na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, waligombana mbele ya wafadhili hao na kuibua aibu kubwa.

Mradi huo ulishakuwa kwenye hatua mbalimbali kabla Gambo hajateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa. Serikali ilitoa vibali vyote vya mradi kufanyika katika eneo ambalo kampuni ya Mawalla ilitoa kwa Shirika la Maendeleo la Arusha (ARDf).

Lema alitoa vilelezo kuthibitisha kuwa ni yeye aliyekuwa na maono ya kujenga hospitali hiyo kwa manufaa ya wananchi wote, ni yeye aliyeomba eneo, ni yeye aliyetafuta wafadhili na pia ni yeye aliyependekeza Gambo awe mgeni rasmi katika uwekaji wa jiwe la msingi na uzinduzi wa ujenzi.

Mgogoro ulianza pale ratiba ilipoonyesha Lema angekuwa miongoni mwa wazungumzaji, lakini Gambo akabadilisha ratiba kwa kuondoa baadhi ya wasemaji katika hafla hiyo akiwamo Lema.

Lema alilipuka na kupinga maelezo ya Gambo akisema yamejaa hila, ghiliba na wivu wenye mwelekeo wa kumnufaisha kisiasa badala ya kuwakilisha msimamo wa serikali kwa faida ya wananchi wote.

Pamoja na mgogoro huo, Gambo alihakikisha Lema anaswekwa rumande kwa muda mrefu kabla ya suala hilo kufikishwa mahakamani.

Mkono wa Gambo fidia ya Sh. Bilioni 1.9

Baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, uongozi wa Jiji la Arusha uliokoa Sh bilioni 1.9 zilizokuwa zitumike kununua eneo la kujenga kituo cha mabasi, huku Gambo akitajwa kusimama kidete fedha zilipwe.

Fedha hizo zilikuwa zitumike kuwalipa fidia wakazi wa Oloresho, Kata ya Olasiti, ili kupisha ujenzi wa kituo hicho.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, kwa wakati huo, Dk. Madeni, aliunda timu maalumu kutafuta eneo mbadala, baada ya kuona fidia hiyo ni kubwa kulinganisha na uhalisia.

Bei ya soko ambayo ingeweza kununuliwa na Jiji ni Sh milioni 40 kwa ekari moja badala ya bei iliyowekwa na wataalamu ya Sh milioni 80 kwa eneo la ukubwa huo.

Dk. Madeni alisema baada ya kupata ukweli kuhusu fidia halali ya eneo hilo, alishangazwa na ufisadi huo.

Alisema baada ya kupata utata wa fidia ya Sh bilioni 1.9 kwa wakazi wa Oloresho, timu yake ilibaini kuwa kiwango halali kilichopaswa kulipwa ni Sh bilioni 1.1.

Alisema kuwa si tu kwamba fidia hiyo ndiyo halali, bali ndiyo waliyokuwa wamekubaliana miaka miwili iliyopita kati yao na mkurugenzi aliyeondoka, Dk. Athuman Kihamia na wauza eneo.

Kukwama kwa mpango huo wa ufisadi kuliibua vita ya maneno kati ya Dk. Madeni na Gambo, kiasi cha kutoleana maneno makali hadharani.

Pia Gambo amehusika katika malumbano ya hadharani na viongozi wa chini yake kama wakurugenzi na wakuu wa wilaya wengi.

=====

Habari hii imekanushwa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Nchini TAKUKURU.

Zaidi, soma;

Arusha: TAKUKURU yakanusha kumshikilia na kumhoji Mrisho Gambo
 
Naendelea kutafakari tu...Maana "pindipo inapokufikia hoja chunguza Kwanza usije ukadhuru wasiokuwa na hatia".....
 
Sijapenda mtoa mada hata hujui uko jukwaa gani humu hakuna kuficha ficha watuhumiwa! umeniboa sana kuna sehemu nyingi unaandika na kuficha ficha majina na wahusika si bora ungeenda kuitisha kikao cha familia uwaeleze majungu yako kwa Gambo? acheni wivu enyi wabongo wenzangu!! hivi Arusha mmekuwaje mmeharibu mji wa wajanja!
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom