SoC02 Afya ya Mama na Mtoto

Stories of Change - 2022 Competition

Miry Mo

New Member
Jul 18, 2022
1
0
Habari, jina langu ni Miriam, na leo ningependa kuzungumza na wanajamii kuhusu afya ya uzazi kwa wakina Mama na watoto.

Kumekua na wimbi kubwa la wanawake/mabinti wanaopata ujauzito kwa miaka ya hivi karibuni, kutokua na elimu sahihi juu ya makuzi ya mtoto tumboni.

Moja kati ya eneo ningependa kuzungumzia, ni kuhusu swala la dawa ya "Folic acid"

Wamama/mabinti wengi huzipuuzia na kudhani kuwa hakuna ulazima wa kuzitumia, lakini yote haya yanatokea, kwasababu jamii haipatiwi mafunzo kwenye baadhi ya vituo vya afya.

Ningependa kuwakumbusha wataalamu wa afya/wadau mbalimbali walifanyie kazi. Ufahamamu na elimu sahihi ya matumiza ya folic acid humsaidia mtoto asipate madhara kama vile mdomo sungura, mgongo wazi, mtoto kuzaliwa na kichwa kikubwa kuliko kawaida, lakini pia humsaidia mama mjamzito kuongeza damu nk. Ninaimani wamama/mabinti wengi wakipatiwa mafunzo ya namna hii watabadilika na tutapata kizazi salama kwa manufaa ya kesho katika jamii yetu.

Vilevile wataalamu au wadau wa afya wajitahidi kuendelea kutoa elimu ya changamoto mbali mbali zinazowapata/zinazoweza kuwapata wamama kabla na baada ya kujifungua hususani sehemu za vijijini, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuondoa imani za kishirikina zinazohusishwa na changamoto hizo. Mfano kwenye swala la mchakato wa kukua kwa mimba, kuna changamoto kama ya kiumbe kuto-kukua tumboni, hili ni moja kati ya changamoto wanazo kutana nazo wamama wajawazito.

Pia niliwahi kusikia changamoto ya mama mjamzito kupata tatizo la kitovu cha mtoto kua kifupi tumboni (hii kesi yake hutokea mara chache sana) hivyo kwa ajili ya usalama wake na mtoto wakati wa kujifungua inabidi mama afanyiwe upasuaji ili kuokoa maisha yake na ya mtoto.

Kitu pekee kilichonijia baada ya kuyasikia haya, ni dhahiri kuwa, ndugu zetu wa vijijini ambao wao baadhi yao bado hawajifungulii kwenye vituo vya afya, wakikutana na kesi ya namna hii hatutaweza kupata kizazi salama. Hivyo bado napendekeza elimu, pamoja na uboreshwaji wa vifaa tiba, vyakuweza kusaidia kutambua mapema changamoto kama hizi zinapojitokeza, ili kusaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Lakini kuna matatizo mengine pia yanayowapata wakinamama wakati wa kujifungua kama vile kupasuka kwa placenta, hili tatizo hutokea sana, bado nasisitiza ndugu zetu wa vijijini ambao baadhi yao bado hawajifungulii katika vituo vya afya, watawezaje kukabiliana na changamoto za namna hii?

Hivyo basi wadau mbalimbali katika sekta ya Afya wajitahidi kutembelea maeneo ya vijijini ili kuona changamoto zao na kutoa elimu za namna hii ili kupunguza kama sio kumaliza kabisa athari zinazopatikana, ambazo ni vifo vya mama na mtoto, na kutusaidia pia kupata vizazi bora katika taifa letu na jamii kwa ujumla.


Vilevile kwenye swala zima la unyonyeshaji, wataalamu wa afya waendelee kutoa elimu kwa bidii hususani kwa wamama wa kileo, waendelee kuambiwa umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto na athari za mtoto kutokupata maziwa ya mama ndani ya miaka miwili ya ukuaji wa mtoto.

Pia kuna hili swala la wakinamama wajawazito kuambiana/kushauriana kutokuanza clinic mapema, hii ni hatari sana, mwanamke anapojingundua mjamzito mara moja awahi katika kituo cha afya yeye pamoja na mwenza wake, kwa ajili ya vipimo muhimu vya awali kwa ajili ya maendeleo ya makuzi ya mtoto. Kama wazazi watakua na maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile kaswende nk. Kuna uwezekano mkubwa mtoto kuzaliwa na ugonjwa huo kama tu wazazi watachelewa kupata matibabu sahihi tangu mwanzo wa utungwaji wa mimba.

Na pia jamii ipate elimu ya kutosha ya wababa kwenda kwenye clinic za uzazi kwani husaidia kwenye vipimo na kujua namna ya kumlinda mtoto, katika hili kuna kitu kama vile swala la group (grupu) la damu, kuna kitu kinaitwa RHESUS FACTOR hii ni aina ya protini (protein) ambayo hupatikana kwenye chembe nyekundu za damu, ambazo watu wengi wenye grupu la damu lenye chanya(+) huwa nazo, lakini wenye grupu la damu lenye hasi(-) hawana.

Hii ni moja kati ya kitu muhimu sana kutambua magrupu yenu ya damu ili kumlinda mtoto,

Kwa mfano mama akiwa na grupu la damu lenye hasi(negative) halafu baba akiwa na grupu la damu lenye chanya(positive), hapa kitaalamu wataalamu husema mara nyingi mtoto lazima awe na grupu la damu lenye chanya, hivyo ili kumlinda mtoto inabidi ujauzito unapofika umri fulani mama apatiwe sindano ambayo huitwa anti D, hiyo sindano humsaidia kumlinda mtoto asipate changamoto mbalimbali wakati wa kuzaliwa ikiwemo kifo muda mfupi baada ya kuzaliwa kama tu mama hatapatiwa huduma kwa wakati.

Lakini pia kwenye maswala ya makuzi ya mtoto/watoto, hutofautiana katika njia za ukuaji.

Kuna utofauti wa jinsi watoto wanavyo jifunza vitu mbalimbali, wepesi na uelewa wa kupambanua mambo kati ya mtoto mmoja na mwingine hutegemea vitu mbalimbali.

Kwenye swala la watoto wenye uzito kujifunza, kuna tatizo lingine linaweza kuwa ni chanzo kinachoathiri maendeleo ya ukuaji wa mtoto. USONJI ni moja ya tatizo hilo,

Usonji ni tatizo ambalo katika jamii yetu ya kitanzania tulio wengi hatulifahamu na wala hatuna elimu nalo. Hivyo ningependa wataalamu wa Afya pia watoe elimu katika jamii juu ya tatizo hilo hususani kwenye clinic za maendeleo ya mama na mtoto ili iwe rahisi kwa jamii kujua ni kwa namna gani mzazi au mlezi anaweza kutambua tatizo hilo na kulitatua kwa urahisi au kujua namna ya kuishi na mtoto wake bila kumnyima haki zake za msingi.

Mwisho kabisa napenda kumalizia kwa kuwapongeza serikali na wadau wote wa sekta ya afya kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kuboresha huduma za afya. Pia kuomba serikali yetu tukufu pamoja na wadau mbalimbali wazidi kutusaidia kuweza kupata vituo vya afya kwa wingi, hasa maeneo ya vijijini ili elimu za namna hii na nyingi nyingine ziweze kutolewa kwa ufasaha na kwa wingi zaidi ili kukiokoa kizazi chetu cha sasa na cha baadae kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu ili kupata Taifa lenye watu Imara. ASANTE.
 
Back
Top Bottom