Zitto Kabwe: Nani anaongoza nchi yetu?

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
NANI ANAONGOZA NCHI YETU?


1. Utangulizi:

Ndugu Wananchi

Katika siku za hivi karibuni suala la afya ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli limekuwa katika mijadala katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, katika mitandao ya kijamii na katika medani nyinginezo.

Kukithiri kwa mijadala hiyo kumesababisha hali ya wasiwasi na taharuki miongoni mwa wananchi. Hali hiyo inatia shaka zaidi na kutokuonekana hadharani kwa Rais mwenyewe kwa takriban siku 16 sasa. Aidha, ukimya wa hali ya juu miongoni mwa viongozi serikalini kumeongeza uzito wa suala hili.

Tunatambua kuwa Waziri Mkuu akiwa msikitini wilayani Njombe, alitamka kuwa amezungumza na Rais na kutaka watanzania wapuuze kauli za kuzua taharuki kuhusu afya ya Rais. Kiukweli Watanzania wanapata shida kuamini kauli hii ya Waziri Mkuu, kwani imezoeleka huko nyuma kwa Rais kuwapigia viongozi wake simu hasa wanapokuwa katika hadhira. Kwa namna tunavyojua utendaji wa Rais, kwa uvumi kuhusu afya yake ulivyoenea hiyo ndio ingekuwa njia angeitumia kumaliza uvumi na uzushi huo, haikuwa hivyo.

Imezoeleka kuwa kila siku ya Jumapili, Rais hujumuika na waumini wengine kwa ibada kanisani na mara nyingi kuzungumza na Taifa, kwa Jumapili ya Juzi tarehe 14 Machi, 2021 hali haikuwa hivyo. Hii inaongeza taharuki na kuongeza uzito wa uvumi unaoshika kasi kuhusu afya ya Rais.

Hata kauli ya Makamu wa Rais jana akiwa njiani kwenda mkoani Tanga haikukidhi haja, imeongeza mshawasha badala ya kuzima tetesi zilizoenea, imeacha maswali mengi zaidi badala ya kujibu maswali yanayoulizwa kuhusu afya ya Rais, imeibua sintofahamu zaidi badala ya kuleta utulivu kwa wananchi.

2. Tathmini Yetu:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana mamlaka makubwa na nafasi nyeti katika ustawi wa Taifa. Katiba ibara ya 33(2) inamtambua Rais kama pia Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Haya ni mamlaka makubwa sana. Hivyo basi, afya ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitakiwi kuwa ni jambo la kudhihakiwa ama linapouliziwa watu kuonekana wabaya.

Afya ya Rais, kwa umuhimu wake, ni jambo lililowekewa utaratibu wa kushughulika nalo inapotetereka. Tunatambua pasi na shaka kwamba Rais anaumwa, tunashangazwa na ukimya unaoendelea kutamalaki katika suala hili. Ni kwa kiasi gani ugonjwa wa Rais unasababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake ni suala lililo katika utaratibu wazi wa kikatiba. Kwa umuhimu wake ninanukuu vipengele vifuatavyo vya Katiba:

Ibara ya 37(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, toleo la 2005 inasema, nanukuu;

“Endapo Baraza la Mawaziri litaona; kuwa Rais hawezi kumudu kazi zake kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili, laweza kuwasilisha kwa Jaji Mkuu azimio la kumwomba Jaji Mkuu athibitishe kwamba Rais, kwa sababu ya maradhi ya mwili au akili, hawezi kumudu kazi zake. Baada ya kupokea azimio kama hilo, Jaji Mkuu atateua Bodi ya Utabibu ya watu wasiopungua watatu atakaowateua kutoka miongoni mwa mabingwa wanaotambuliwa na sheria ya matabibu ya Tanzania, na Bodi hiyo itachunguza suala hilo na kumshauri Jaji Mkuu ipasavyo, naye (Jaji Mkuu) aweza baada ya kutafakari Ushahidi wa kitabibu kuwasilisha kwa Spika hati ya kuthibitisha kwamba Rais,kutokana na maradhi ya mwili au ya akili hamudu kazi zake; na iwapo Jaji Mkuu hatabatilisha tamko hilo ndani ya siku saba kutokana na Rais kupata nafuu na kurejea kazini, basi itahesabiwa kiti cha Rais ki wazi, na yaliyomo katika ibara ndogo ya (5) yatatumika.”

Aidha, Ibara ya 37 (3) ya Katiba nayo pia inatamka yafuatayo kuhusu Rais kushindwa kutekeleza majukumu yake, nanukuu;

“Endapo Rais atakuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano au atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu nyingine yeyote, kazi na shughuli za Rais zitatekelezwa na mmojawapo wa wafuatao kwa kufuata mpangilio ufuatao, yaani –
(a) Makamu wa Rais au kama nafasi yake iwazi au kama naye hayupo au ni mgonjwa; basi;
(b) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano”.

Zaidi, Ibara ya 37 (4) inaeleza;

“Endapo Waziri Mkuu ndiye atatekeleza kazi na shughuli za Rais kutokana na sababu kwamba Makamu wa Rais hayupo basi Waziri Mkuu ataacha kutekeleza kazi na shughuli hizo endapo lolote kati ya mambo yafuatayo litatokea mwanzo –
(a) Rais atakaporejea katika Jamhuri ya Muungano au atakapopata nafuu kutokana na maradhi na kuanza kutekeleza kazi za Rais;
(b) Makamu wa Rais atakaporejea katika Jamhuri ya Muungano”.

Tumenukuu vipengele vyote hivyo vya Katiba kuonesha umuhimu na uzito unaopewa afya ya Rais katika nchi hii. Huu si wakati tena wa kukaa kimya. Huu ni wakati wa Serikali kutoa tamko rasmi la hali halisi kuhusu afya ya Rais. Tunahitaji kujua ni nani hivi sasa anayetekeleza madaraka ya Rais na kwa nyenzo ipi ya Katiba. Ukimya uliopo sasa unasababisha taharuki kubwa isiyo na tija kwa ustawi wa Taifa letu. Tunachelea kuwaza, na Mwenyezi Mungu apishie mbali, hivi leo Taifa letu likivamiwa na wasioitakia mema nchi yetu, ni nani Amiri Jeshi Mkuu? Kutuambia tu tuko salama bila kutuambia yuko wapi Amiri Jeshi Mkuu si jambo linaloleta utulivu.

3. Wito Wetu kwa Serikali:

Kwa kuzingatia uzito wa tuliyoyaeleza, tunatoa wito kwa Serikali, kwanza iwaachie watu wote waliokamatwa na Jeshi la Polisi kwa kuhoji juu ya afya ya Rais, kisha ifanye yafuatayo ili kutuliza mshawasha wa wananchi;

i. Itueleze wananchi hali halisi ya afya ya Rais, itumie pia maelezo hayo kutujibu kwa kina wananchi iwapo Rais bado anao uwezo wa kutekeleza majukumu yake au la.

ii. Iwapo Rais hana uwezo huo au afya yake imetetereka kiasi cha kutia mashaka, basi kifungu cha 37(2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kitekelezwe ili jopo la matabibu litakaloteuliwa na Jaji Mkuu lifanye kazi yake na hali ya afya ya Rais ijulikane wazi kupitia kwa Spika.

iii. Katibu Mkuu Kiongozi atamke rasmi kuwa Makamu wa Rais amekuwa akitekeleza madaraka ya Rais Kwa mujibu wa Katiba na kwamba ni Kaimu Rais Kwa mujibu wa Itifiki zote. Hivyo basi kumtaka Makamu wa Rais atekeleze majukumu uRais Kwa mujibu wa Katiba na atumie nafasi hiyo kulieleza Taifa Hali ya Rais.

iv. Wakuu wa Mashirika ya Umma, na haswa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) watoke kuzima tetesi zinazoenea juu ya yanayoendelea katika taasisi hiyo nyeti kwa uchumi wa Nchi. Ni muhimu rekodi ya Fedha za Kigeni na Akiba ya Dhahabu zilindwe. Wakati huu wa sintofahamu ni vizuri Makamu wa Rais peke yake kama Kaimu Rais ndiye anapaswa kuidhinisha kwa kauli thabiti kinachoitwa ‘maagizo ya Rais’. Wananchi watahitaji Taarifa kuhusu Akiba hizi mara baada ya sintofahamu hii kuisha.

Vile vile Tunatoa wito Kwa Asasi za Kiraia na Bunge kuchukua hatua Kwa;

- kuitaka TLS na AZAKI nyengine za uwajibikaji wapaze Sauti zao katika Suala hili ili kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Itakuwa ni makosa makubwa kwa siku nyengine 16 kuacha Nchi ikiongozwa na watu ambao hawakuchaguliwa (unelected bureaucrats) Wakati Katiba yetu imezingatia mazingira yote ya mwanadamu.

- Kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge watumie nafasi yao kuitaka Serikali itoe tamko kuhusu Afya ya Mhe Rais . Kwa kufanya hivyo ni kulinda kiapo chao cha kuitetea na kuuhifadhi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

4. Hitimisho:

Afya ya Rais sio jambo linalopaswa kuwa siri, yeye ni kiongozi wa Taifa hili. Tumekuwa na marais ambao waliugua huko nyuma, Marehemu Mzee Mkapa alipougua na kukaa muda mrefu nchini Uswizi wananchi walijulishwa na taarifa za mara kwa mara zilitolewa kuhusu maendeleo ya afya yake, halikadhalika Mzee Kikwete alipofanyiwa upasuaji nchini Marekani.

Utoaji huo wa taarifa za hali ya afya ya Kiongozi wa nchi ni jambo la kawaida duniani kote, na husaidia kuondoa taharuki na wasiwasi ambao kwa bahati mbaya ndio vimetamalaki nchini kwa sasa. Ni muhimu Serikali itoe taarifa kuhusu Afya ya Rais ili kumaliza taharuki iliyopo, kwank Watanzania tunayo haki ya kujulishwa hali ya afya ya Rais.


Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Machi 16, 2021
Dar es salaam.
FB_IMG_1615880660548.jpg
 
Nyie wapinzani wapumbavu sana hasa Lissu

Juzi mmesema Rais amelazwa nchini Kenya, mara amepelewa India ,mara amekufa.Pumbafu kabisa.

Leo mmekuja na ngojera Nyengine mara Yuko paralysed one side .Pumbafu sana nyie.hamna akili kabisa.we watch you .nchi Nyengine watu kama nyie mnafuatwa Huko mliko.
 
Back
Top Bottom