Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,476
- 39,995
Hakuna namna nyingine ya kumaliza mgogoro wa nidhamu CDM isipokuwa ama kwa uongozi wa Taifa kuwavua uanachama wale wote ambao wanaonekana kuwa ni vyanzo vya migogoro isiyokoma ndani ya chama au kwa wale ambao wanaona hawawezi kuendelea kuwa chini ya uongozi wa taifa (subordination) na wanataka kulazimisha mabadiliko kwa njia nje ya zile za Kikatiba kuamua kujiondoa wenyewe.
Katika mfululizo wangu ule wa mwisho wa mwaka jana kuhusiana na suala la nidhamu nilieleza kwa kirefu juu ya jambo hili. Mgogoro wa CDM ulipofikia sasa sioni njia yoyote nyingine isipokuwa ama watu kuvuliwa uanachama na hivyo kutokuwa na jambo lolote la kufanya kwa chama au wao wenyewe kuamua kujiondoa baada ya kuona kuwa chama hakiendi au hakikubaliani nao kiasi cha kutoweza kuaminika tena. Binafsi siamini kama mahakama itaingilia kati utendaji wa chama cha siasa na hasa haki yake ya Kikatiba kusimamia nidhamu ya wanachama wake na hasa viongozi wake. Tayari tumeshaona precedence za mahakama kuhusu suala hili huko nyuma.
Kwa maoni yangu Zitto hawezi kuendelea kuwa CDM kwa sasa na sijaona dalili za kuweza kupatana hasa baada ya matukio mbalimbali ya mwishoni mwa mwaka jana. Ametengeneza (ametengenezewa) hali ambayo inamfanya iwe vigumu kuwa chini ya viongozi wengine na yawezekana hilo haliwezi kutokea hadi yeye awe ndiyo kiongozi mkuu wa chama. Katika mfululizo wangu ule nilieleza kuwa ni lazima viongozi na wanachama wajifunze kukubali madaraka yaliyo juu yao na kutumia njia za kawaida kuleta mabadiliko hata kama itatumia muda. Kauli za ndugu yetu Zitto za mara kwa mara (kwenye mitandao na kwingine) zinaonesha pasi ya shaka kuwa hana imani na viongozi walio juu yake na hajawa tayari kukubali madaraka yao juu yake na hivyo kutengeneza kile ambacho katika makala yangu nilikiita "parallel leadership". Chama hakiwezi kuwa na sehemu mbili za uongozi - wale halali na wale ambao wanaamini wana uhalali (hata kama hawajapewa nafasi za kufanya hivyo).
CDM ichukue uamuzi wa kusimamia nidhamu katika chama na kuweka taratibu za kuhakikisha kuwa matatizo haya ya mara kwa mara ya baadhi ya viongozi wake wakuu kugongana yanatatuliwa na kuzuia mapema zaidi. Itakuwa ni kujidanganya kudhani kuwa matatizo haya yanatokea kwa bahati mbaya; ni vizuri kujiuliza kwanini yanatokea na ni kitu gani kinafanya kuwepo na potential ya migogoro ya aina hii. Kwenye mfululizo wangu nilitoa mapendekezo kadhaa na nina uhakika wapo wengine wenye mapendekezo ya tofauti. Ni lazima kisimamia nidhamu kwa sababu kama taasisi haiwezi kufanikiwa kama haisimamii nidhamu bila upendeleo, woga, husda au chuki. Kisipepese macho bali kichukue hatua thabiti za kuhakikisha kuwa viongozi wanaoonekana ni vyanzo vya migogoro wanaelewa uzito wa matendo, kauli, na fikra zao dhidi ya chama. Pendekezo langu la kwenye mfululizo kuwa Chama kitoe masharti makali kwa viongozi hawa ili waendelee na uanachama sidhani kama linaweza kukubaliwa nao; linaweza kujaribiwa lakini sioni dalili ya kukubaliwa.
Nje ya hapo viongozi kama Zitto ambao wanaamini wana wapenzi, kundi kubwa la wanachama na wanakubalika sana na wananchi kuamua kujiondoa wao wenyewe bila kusubiri kufukuzwa kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamesimamia dhamira zao zaidi. Nyerere aliwahi kusema CCM siyo mama yake na hili ni kweli kwa CDM pia. Zitto kama anaona hawezi kuwa chini ya uongozi wa sasa na hawezi kuacha kuonekana anashindana na uongozi wa chama chake ni vizuri akaamua kujivua uanachama wa CDM kwa heshima na kuendelea na siasa kwa namna nyingine. Kwa vile wapo watu wanaomfuata au kukubali fikra zake ni wazi kuwa akiingia chama kingine au hata kuanzisha kingine atakuwa na kundi la wafuasi ambao watafuata nyayo zake na yeye anaweza kuwapa ule uongozi ambao hawezi kuutoa CDM bila kuyumbishwa na "wahafidhina" wa CDM.
Ni maoni yangu kuwa njia pekee ya kumaliza mgogoro huu wa kinidhamu ni ama watu kuvuliwa uanachama au wao wenyewe kujivua uanachama. Njia nyingine ambayo sidhani kama inawezekana ni viongozi wenye mgogoro kukubali makosa na kujiweka chini ya uongozi wa juu yao bila masharti (unconditional) ili kurudisha imani. Hili la tatu sidhani kama linawezekana kirahisi.
Mahakama isiingilie migogoro hii ya kinidhamu kwani itafungua mlango mbaya sana katika siasa za Tanzania ambapo watu wanaweza kujikuta kwenye migogoro kwenye vyama vyao na badala ya kukubali madaraka yaliyo juu yao katika vyama watakimbilia mahakamani kutafuta "haki". Mwisho wa siku vyama vinaweza kujikuta vinalazimishwa kuwa na viongozi wanaotokana na mahakama. Ni pale tu ambapo kuna hoja za Kikatiba au za Haki za Binadamu na zile za Kiraia mahakama zinaweza kuangalia kwa uangalifu bila kujikuta vinaingilia maamuzi ya vyama vya siasa kujiendesha na kujisimamia.
Ni matumaini yangu mgogoro huu utaisha punde ili vyama na watu mbalimbali waanze kujipanga vizuri kuelekea chaguzi mbalimbali zinazokuja bila kujikuta zinatumia muda na raslimali nyingi kushughulikia migogoro ambayo ingeweza kumalizwa mapema zaidi kuliko ilivyo sasa.
Heri ya Mwaka Mpya!