Itakuwa kutojitendea haki kutokutambua kuwa taifa hili linapita katika hali iliyo tete. Itakuwa ni kukosa uzalendo kuyaona haya na kuyafanyia macho.
Pamoja na yote ni muhimu sana maslahi ya taifa yakawekwa mbele.
Ieleweke kuwa maslahi ya taifa (kama ilivyo kwa wajibu wa kuyalinda), si ya watawala, serikali, Polisi wala taasisi yoyote iwayo yote hapa nchini. Msingi mkuu wa maslahi ya taifa ni uhai na maisha ya mtu mmoja mmoja katika taifa, pasipo na ubaguzi wowote.
Hayupo anayaweza kujimilikisha wajibu wa kuulinda msingi huu wa maslahi ya taifa. Wajibu wa kuyalinda maslahi ya taifa letu ni wetu sote. Hayupi aliye bora, uchungu au dhamana zaidi kuliko mwingine.
Yaliyo mazito zaidi kutufikisha kwenye hali tete hii tulimo yenye kuhatarisha maslahi yetu kama taifa ni:
(a) janga la Corona linaloendelea kutupukutisha kweli kweli,
(b) fukuto lililowiva la kudai katiba mpya.
1. Janga la Corona:
Tunapita katika wakati mgumu sana na ugonjwa huu. Kama alivyosema SSH, ugonjwa huu unatupukutisha vilivyo na kuwa anayebeza madhara ya ugonjwa huu ni vile hajaguswa tu.
Tusiwape nafasi wanaobeza uwepo wa ugonjwa huu, tahadhari na jitihada za kitalaamu kwenye kupambana nao kwa sababu zozote zile.
2. Fukuto la katiba mpya:
Hili limekolezwa zaidi na kukamatwa kwa mheshimiwa Mbowe. Itakuwa ni kujidanganya kwingi kudhani kuwa sababu zilizotolewa za kukamatwa kwake zimekubalika au hata kuaminika.
Siyo siri kuwa kwa tashwishi za ukiukwaji huu wa haki unaoonekana machoni pa wengine, tunakoelekea si kwema. Busara isipotamalaki ni wazi kuwa kitaumana.
#1, Chonde chonde wadau, hili lisigubikwe na harakati za #2. Hadi hapa wadau hongereni sana kwa kuwahimili wajumbe wenu.
Katika hali zote kuliwekea #1 kuwa ni kipaumbele na hasa kuwapa nafasi watu kupokea chanjo bila ya kutatizika, ni jambo lenye thwawabu kubwa.
Kwa hili hadi hapa tulipo, kongole kwenu sana tu wadau.
#2, Chonde chonde serikali, hili lisiwe sababu ya kutufarakanisha na hata kuweka #1 hatarini. Pimeni faida za kumshikilia mheshimiwa Mbowe kwa sababu zisizoaminika dhidi ya kuchagua njia ya salama ya mazungumzo.
Kuna haja gani ya kutiana majaribuni?
Mzaha mzaha hutumbua usaha.
Eeh mola wetu ukawanyooshee vidole vyako vya onyo wote wanaonoa silaha zao na kujipanga kuyahatarisha maslahi ya watu wako katika nchi yao kwa ubinafsi wao.
Ninawasilisha!