Mimi sijaribu ku-benchmark Performance ya Halima Mdee na wabunge wa CCM; kwanza naona hiyo ni sign mapema ya udhaifu... hauwezi kusema na kusimama jukwaani na kusema kwamba wabunge wa CCM hawafai halafu ukija kuulizwa umefanya nini unaanza kuuliza hao amabao hawafai wamefanya nini.... Wabunge wanaosema wako tofauti na wataleta mabadiliko makubwa lazima waweke Benchmark yao juu zaidi.... hata ukiwa shuleni hauwezi kupata "D" halafu ukasema lakini wenzangu wamepata "F"; sisi tunataka Changes za ukweli natunataka watu wa "A"...... Nimeshasema mimi sina ushabiki wa ki-chama I am merely an innocent observer..... siko upande wa CCM na siko CDM niko upande wa Maendeleo... Kwa mchango wake bungeni juu ya Maslahi ya kitaifa kwa ujumla mimi sina tatizo na Mheshimiwa Mdee, lakini kwa wapiga kura wa Kawe walio mchagua bado naona hajawafanyia lolote la kumsifia....
Please soma makala hii ya Privatus Karugendo halafu naomba comments zako
SWALI langu la msingi katika makala hii ni je, sisi Watanzania tunafahamu kazi za wabunge? Na je, wabunge wetu wanafahamu kazi zao na wajibu wao? Tunapokaribia uchaguzi mkuu, tunafahamu umuhimu wa kazi hii ambayo ni ya gharama kubwa?
Taifa letu linatumia fedha nyingi kuendesha uchaguzi mkuu, je, tunafahamu umuhimu wake? Tunawachagua wabunge kwa sifa zao na uwezo wao au tunachagua wale wanaotununulia pombe na kutupatia sukari?
Tunachagua wabunge wetu kwa kuangalia uzuri wa sera za vyama vyao siasa au tunaangalia madaraka na nguvu za kifedha za vyama vyao?
Tunawachagua wabunge kwa kubaini kwamba wanayatabua na kuyashiriki matatizo yetu na mafanikio yetu au tunawachagua kwa shinikizo na pengine inawezekana hatuwachagui kabisa bali wanatangazwa washindi na mamlaka husika?
Katika pitapita zangu nimekutana na bango linalomnadi mbunge wa sehemu fulani hivi: Baadhi ya misaada mbalimbali niliyotoa kwa wanajimbo langu, Binafsi:
- Nilisaidia upatikanaji wa majeneza pamoja na kusafirisha marehemu kutoka wilaya yangu waliopata ajali ya treni huko Dodoma na kushughulikia majeruhi kwa kuwawahisha hospitali ili kupata matibabu ya haraka.
-Nilifanikisha uletwaji wa mwili wa marehemu Mathias Kasoso kutoka Dar-es Salaam; Nilisaidia sana uwezekano wa usafiri wa ndege pamoja na usafiri wa gari wa kutoka uwanja wa ndege kwenda alikozikwa.
-Nilitoa baiskeli kwa mlemavu wa .... yenye thamani ya Tsh 60,000 na 100,000/- kumnunulia mlemavu mwingine baiskeli ya gurudumu tatu.
-Nilimsaidia mama mtu mzima kupata haki zake Dodoma zilizokuwa hatarini kupotea bure.
-Nilimsaidia Salehe na rafiki yake (shs 40,000) nauli ya kutoka Dar es Salaam, waliokuwa wamekwama.
-Niliwasafirisha vijana wawili kutoka jimboni mwangu waliokwenda Dar es Salaam baada ya kudanganywa waende huko ambako wangepatiwa ajira.
-Nilitoa ada ya mtoto wa mzee wa Mahakama ya Mwanzo binti yake aliyekuwa akisoma sekondari ya kata.
- Tarehe 24/6/09: Nilihudhuria mazishi ya mzee Maddu aliyezikwa huko Mtakuja na kuchangia sh 100,000 kama rambirambi.
Ningepata nafasi ya kumkumbusha ndugu yetu huyu ni kwamba kati ya yote aliyoyataja hakuna hata moja linalohusiana na kazi yake ya ubunge. Labda alitaka kujitangaza kwamba yeye ni raia mwema. Hivyo anafaa kuchaguliwa kuwa mbunge. Hata hivyo bado ana kazi ya kujifunza na kuzifahamu kazi za mbunge!
Sasa hivi tunaingia kwenye kipindi cha uchaguzi. Waheshimiwa wabunge wameanza kupita kwenye majimbo yao. Wengine wanayachukulia majimbo haya kama mali yao kama ilivyo nyumba, ardhi, gari au familia. Jinsi mtu asivyotaka nyumba yake au ardhi yake isiguswe ndivyo waheshimiwa wabunge wasivyotaka majimbo yao yaguswe. Sasa ndipo wanaanza kuwakumbuka wapiga kura. Wale waliokuwa wakiishi Dar es Salaam na Dodoma, wanaanza kuyakumbuka majimbo yao.
Mbunge anaweza kuishauri serikali kujenga shule, lakini si kazi ya mbunge kujenga shule kwa pesa zake binafsi, akifanya hivyo, itakuwa si kwa vile ni mbunge, bali ni kwa vile atakuwa raia mwema mwenye uwezo na roho ya kuwasaidia wananchi wenzake.
Mbunge anaweza kutoa sukari kama vile wananchi wenye nia njema na uwezo wanavyofanya, lakini si kwamba ni kazi ya mbunge, kugawa sukari, kana kwamba asipotoa sukari au vitenge atakuwa hakufanya kazi yake ya ubunge. Hata hivyo si lazima kila raia mwema kuingia bungeni. Raia wema, ambao tunao wengi, wanaweza kuendelea na kazi yao ya kuihudumia jamii kwa matendo yao mema, na wanasiasa wenye uwezo wa kujieleza na kueleza kile walichotumwa na wananchi.
Wenye uwezo wa kuchambua na kuiweka sawa miswada mbali mbali inayowasilishwa bungeni, wasomi, wazalendo na wenye moyo wa kukubali kutumwa, wapewe nafasi ya kuwatumikia wananchi Bungeni.
Tunaweza kuzifahamu kazi za mbunge, kwa kuangalia kazi za Bunge, maana mbunge, ni mwakilishi wa jimbo (wananchi) katika Bunge: " Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi. Kuisimamia na kuishauri serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba hii," Ibara ya 63(2), pia na Ibara ya 64(1) inaelezea kazi za Bunge, juu ya kutunga sheria.
Hivyo basi, Mbunge ni mwakilishi wa jimbo lake katika chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kina madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake. Hivyo kutoa misaada, kusalimia misiba na kuwatembelea wagonjwa si kazi za mbunge. Huu ni wajibu wake yeye kama mwananchi katika jamii anamoishi. Hata asingekuwa mbunge, angetakiwa kufanya hivyo maana wananchi wote wanafanya hivyo, wawe madaktari, walimu, viongozi wa dini au viongozi wengine wa vyama na serikali. Inawezekana pia kwamba hata wananchi wanafikiri kwamba kazi za mbunge ni kujenga madaraja, ni kuleta maji, ni kuleta umeme, ni kusalimia misiba na kujenga shule.
Ndiyo maana wale wanaohimiza elimu ya uraia si wa kupuuzwa, ni lazima serikali isikie kiliko hiki na kuweka nguvu zote katika kufundisha elimu ya uraia. Ni jambo muhimu kabla ya uchaguzi wa mwaka huu wananchi wote pamoja na wale wanaotangaza nia ya kugombea wakatambua wajibu na kazi za mbunge. Hayo matendo ya ndugu yetu niliyoyataja hapo juu si ya kubuni au kutunga, hili ni bango liliotundikwa na kusambazwa kwa wananchi wa jimbo lake.
Bila shaka mbunge huyo, anaomba kurudi tena bungeni. Yote aliyoyataja hakuna linalohitaji mtu kuwa mbunge, ndipo alitende. Haya ni matendo ya kujituma katika jamii. Kusalimia misiba na kutoa rambirambi ni jukumu la kila mwananchi.
Kusafirisha watu, kulipa karo, kununua jeneza ni matendo ya kawaida katika jamii. Mtu kutaka kuyatumia katika kampeni ya kuingia bungeni, ni kielelezo kwamba mtu huyu anakuwa si makini vya kutosha.
Kama ni mtu anayetetea kiti chake, kama inavyoelekea kwa mbunge huyu, tungependa kusikia jinsi alivyoishauri serikali kujenga hospitali, kuwapatia watu maji, kujenga shule, kujenga barabara nk. Na si kwa jimbo lake peke yake, lakini kwa majimbo jirani na majimbo yaliyo na shida zaidi. Mtu anapojinadi, ni bora kutaja kazi za Bunge, Ni bora kutaja alivyowawakilisha wananchi katika chombo kikuu cha nchi, chombo chenye mamlaka ya kutunga na kuzifuta sheria.
Bango hili nililolitaja katika makala hili ni ushahidi wa kutosha kwamba watu wanaendelea kupumbazwa na wagombea ubunge. Wanapumbazwa kwa ahadi za kitoto.
Kuna haja ya kuwafundisha watu wakazijua kazi za Bunge. Wajue kwamba hawamchagui mbunge wa kutembelea misiba, kulipa karo na kusafirisha maiti. Wajue kwamba mbunge ni sauti yao ya kuwatetea na kufikisha malalamiko yao bungeni. Malalamiko ya maendeleo na ustawi wa jamii.
Wajue kwamba Mbunge, anaendelea kuwa mmoja wao katika jamii, hivyo anapofika kwenye msiba si tendo la huruma au msaada, na wala si tendo la kibunge! Bali anakuwa anatimiza wajibu wake kama mwanajamii. Mbunge anayeshindwa kuelezea mafanikio yake katika kuchangia maendeleo ya jimbo lake, si kwa misaada yake binafsi, maana si kazi yake kulisaidia jimbo lake binafsi, hafai kuchaguliwa kuingia bungeni.