watanzania wenzetu wakiona barabara za milimani wanafikiri tumejengewa na cleopa msuya kwa kuiba tuko hazina ya serikali. kutoka ktk kitabu alichoandika kuhusu narakati zake za kisiasa chedieli mgonja anatoa maelezo haya.
"mbinu zilizotumika kuzichimba barabara zote za milimani zilikuwa ni karibu sawa. kila mahali walitumia mila ile ya kuweka siku maalum kwa wananchi wote kufanya kazi kwa pamoja, kwa manufaa yao wote. kazi za ina hiyo ziliitwa za "MISARAGAMBO." mila hiyo ilikuwa na nguvu sana. karibu wananchi wote walishiriki kwa moyo mkuu na kwa furaha. wachache walioacha kuhudhuria kutokana na utegaji au uzembe, walipigwa faini ambazo zilikuwa zinajulikana sana kama vile kuchukuliwa kwa kuku, mbuzi au hata mali nyingine iuzwe na mapato yatumike kuendeleza "MSARAGAMBO." barabara ya kwenda milimani vudee na ndolwa ilitumia nguvu nyingi za wananchi ambao waliiichimba kuanzia 1961 mpaka gari la kwanza lilipoweza kuingia milimani vudee mnamo mwaka wa 1969. gari hilo lilikuwa la serikali na liliendeshwa na dereva ayubu wa Same Bomani. "
"barabara ilikuwa imefika mahali pagumu kuliko kote, wakati Mwalimu alipafanya ziara yake hiyo ya pili. ilikuwa imefika ktk jabali kubwa liitwalo mhewe. jabali lenyewe lilikuwa limesimama wima sana na lilienea umbali upatao robo kilometa. ilikuwa imeleta picha kuwa bara ulifika hapo, ikaingia kwenye jabali na kukwama kabisa isiweze kuendelea tena. hata mimi mwenyewe, ambaye nilishirikiana na wananchi kuichimba barabara hiyo ktk vipindi mbalimbali kwa miaka mingi, moyoni nilikuwa na mashaka kuwa huenda tusiweze kupita mhewe. lakini sikuthubutu kumweleza mtu yeyote mashaka yangu hayo.
wananchi walikuwa na ari na moyo mkubwa sana ingekuwa ni kuwaumiza sana kujaribu kuleta wazo la kushindwa. risala ya wananchi kwa raisi mwalimu Nyerere ilisomwa kwa moyo mkuu na kwa ukakamavu sana, na mwanamke mwalimu napendaeli mgonja, mwalimu wa shule ya msingi vudee, hembua. akisoma risala alimwonyesha Raisi lile jabali la kutisha na akamweleza kwa imani kuwa juhudi za wananchi zilikuwa zimewafikisha pale, na kutokana na uamuzi wa dhati wa wananchi, jabali lilikuwa na wasiwasi mkubwa, kwa vile hi hakika watalipasua na kupitisha barabara hiyo."
"MWALIMU NYERERE aliagiza serikali itoe msaada ikiwa ni pamoja na baruti za kupasulia mawe ktk kukamilisha barabara ile. alifanya hivyo wakati akijibu risala ya wananchi. ni siku hiyo pia ndipo aliwaita wananchi wa Wilaya ya Pare kuwa ni "Wachina wa Tanzania, " na akaongeza kusema, kama ingeliwezekana, angewaleta Watanzania wengine waione kazi hiyo ya ajabu iliyokuwa inafanywa na wananchi waliojizatiti kujipatia maendeleo"
maelezo haya yanapatikana ktk kitabu "JOHARI YA MAISHA YANGU" C.Y.MGONJA