- Source #1
- View Source #1
Ni kwamba watu wa Arusha mmeshindikana au vipi? Hili tukio la huyu jamaa akivuta 'Space Capsule' ni la kweli?
- Tunachokijua
- Wanaanga wa kwanza kusafiri kwenda Mwezini baada ya zaidi ya nusu karne wamerejea salama duniani kufuatia safari ya kihistoria iliyoweka rekodi mpya kupitia safari ya majaribio ya Artemis II ya NASA.
Wanaanga wa NASA Reid Wiseman, Victor Glover, na Christina Koch, pamoja na mwanaanga wa Shirika la Anga la Canada (CSA) Jeremy Hansen, walitua baharini Aprili 10, 2026 pwani ya San Diego, wakikamilisha safari ya takriban siku 10 iliyowafikisha umbali wa maili 252,756 kutoka duniani.
Madai
Kumekuwapo na picha inayosambazwa mtandaoni ikimuonesha mtu mmoja akivuta 'Space Capsule' na kudaiwa kuwa ni kutoka nchini Tanzania.
Je, ni upi uhalisia wa picha hiyo?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia nyenzo za kidigitali umejiridhisha kuwa picha hiyo si halisi bali imetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Unde.
Aidha kupitia Google Reverse Image Search zimebainika picha zinazomuonesha mtu huyo akivuta kifaa hicho na kudaiwa kurekodiwa katika maeneo tofautitofauti. Mfano katika mtandao wa Facebook ukurasa wa The News Vine South Africa na kudai kuwa ni mkusanyaji taka kutoka Afrika Kusini akivuta kapsuli ya Orion dakika chache tu baada ya kudaiwa kurejea kutoka Mwezini.
Lakini picha hiyo inaonekana kuwa na mapungufu kadhaa ambayo huonekana kwenye maudhui yaliyotengenezwa kwa AI, ikiwemo changamoto za vivuli, uelekeo wa kibao cha Arusha huku mikono ya mtu huyo ikiwa haionekani kushika kwa usahihi kinachovutwa.
Pamoja na hayo nyenzo za kidigitali za kutambua maudhui yaliyotengenezwa kwa Akili Unde zinabainisha uwezekano wa zaidi ya asilimia 90 kuwa imetengenezwa kwa teknolojia hiyo