SoC03 Watoto wafundishwe haya mashuleni kwa suluhisho la ajira

Stories of Change - 2023 Competition

R0301

New Member
Jun 22, 2023
3
2
Tatizo la ajira kwa vijana limekuwa moja kati ya matatizo makubwa sana yanayosumbua jamii zetu. Tatizo hili limekuwa chanzo cha matatizo mengine mengi kama vile uporaji (panya road), ulevi uliopindukia, umalaya, migogoro mbalimbali kwenye familia inayopelekea familia kuvunjika. Vijana wanaambiwa wajiajiri lakini inakuwa ngumu sana kwasababu hawana misingi mizuri na maarifa sahihi juu ya kujiajiri. Kuna umuhimu mkubwa wa kubadilisha mitazamo ya watoto na vijana wetu wawapo mashuleni kuhusu dhana ya ajira. Mambo yafuatayo yanapaswa kuwa sehemu ya mada katika mitahala yetu mashuleni ili waweze kujiajiri na kupata mafanikio.

1. WANAFUNZI WAFUNDISHWE UJASIRIAMALI; Tunajua dhahiri kwamba kwa dunia ya sasa, watu wengi ni wafanyabiashara wadogo kwa wakubwa. Tatizo linalowakumba wengi ni kutokuwa na maarifa sahihi kuhusu biashara, laiti kama wangefundishwa namna sahihi na kuchagua na kuendesha biashara ndogondogo na hata zile kubwa, basi wengi wangefanikiwa kujikwamua kimaisha na kuajiri wengine. Hivyo basi, elimu ya ujasiriamali ni muhimu Sana kuingizwa kwenye mitahala yetu ili hata vijana wasipoajiriwa waweze kujiajiri.

2. WANAFUNZI WAFUNDISHWE KAZI ZA MIKONO; Zamani shule zetu zilikuwa na miradi mbalimbali kama vile mashamba, ng'ombe, kuku na bustani ambazo wanafunzi ndio waliokuwa wakiihudumia, lakini leo hii miradi hiyo imekuwa ikihudumiwa na wafanyakazi maalum walioajiriwa na mingine haipo tena. Ni shule chache sana ambazo wanawafundisha wanafunzi kazi za mikono, kuna watoto hawajui hata jinsi ya kutunza bustani ya maua. Ni vizuri tukarudisha utamaduni wa kuwafundisha wanafunzi kazi za mikono ili wasipate shida ya kujiajiri kwenye kilimo na ufugaji kwasababu watakuwa na maarifa sahihi.

3. WANAFUNZI WAFUNDISHWE NIDHAMU YA PESA; vijana wengi wanaojaribu kujiajiri kwenye secta mbalimbali wanajikuta wakishindwa kuendelea na hatimaye kukata tamaa kabisa kutokana na kushindwa kuendesha secta hizo kwasababu ya matumizi mabaya ya fedha. Vijana wengi hawajui ni jinsi gani wanaweza kutumia fedha zao katika mpangilio mzuri ambao utawasaidia kufanikiwa, kinyume chake wanakuwa na matumizi makubwa kuliko vipato vyao. Kwahiyo tunapaswa kuliweka jambo hili kwenye mitahala yetu ili wanafunzi wafundishwe matumizi sahihi, uzungushaji na hata kujiwekea akiba ili kusudi watakapojiajiri waweze kufanikiwa.

4. WANAFUNZI WAFUNDISHWE MATUMIZI SAHIHI YA TEKINOLOJIA; sayansi na tekinolojia kwenye ulimwengu wa Leo ni jambo ambalo linakua kwa kasi sana, tekinolojia hizi zinakuwa na faida nyingi sana lakini pia zina hasara zake pale tunapokuwa hatujui namna sahihi ya kuzitumia. Leo hii watoto wengi wanajifunza tabia zisizofaa kuigwa kutoka magharibi ambazo hazifai kwenye jamii zetu za kiafrika, kuna vitu vingi watoto wanajifunza kutoka mitandaoni (televisheni, Facebook, Instagram, Twitter, nk). Hatuwezi kuzuia tekinolojia ikikua na tunapenda ikue kwasababu ina faida nyingi, tunachoweza kufanya ni kuweka mada katika mitahala yetu ambazo zitakuwa zinafundishwa mashuleni kuhusu matumizi sahihi ya tekinolojia hizi. Wanafunzi wafundishwe vitu ambavyo wanaweza kujifunza kutoka mitandaoni ambavyo vinaweza hata kuwaunganisha na watu wa thamani wa ndani na nje ya nchi ambao watawasaidia kujua thamani zao, watoto wanaweza kujijenga kiakili, kiuchumi, kisiasa, kimaadili na hata kijamii kwa kutembelea kurasa na akaunti zenye mambo chanya.

5. WANAFUNZI WAJENGWE VIZURI KWENYE SAIKOLOJIA YA MAHUSIANO; tatizo linalosumbua sana kwenye ulimwengu wa leo ni suala la mahusiano, hapa namaanisha mahusiano ya aina zote (kibiashara, kijamii, kirafiki, kikazi, kimapenzi, nk) watoto wetu wanapaswa kufundishwa namna sahihi ya kuhusiana na watu kulingana na dhumuni la mahusiano. Tatizo la afya ya akili linaongezeka kila siku na linasababisha matatizo makubwa mno kwenye jamii zetu kama kuwapoteza ndugu zetu tuwapendao, lakini ukitazama kwa jicho pevu utagundua kwamba matatizo mengi yanatokana na tatizo la kutojua namna sahihi ya kuhusiana. Watu wanashindwa kuendelea baada ya kujiajiri kwasababu hawajui namna sahihi ya kuhusiana na watu, hivyo wanafunzi wanapaswa wafundishwe namna sahihi ya kuhusiana.

6. WANAFUNZI WAFUNDISHWE NIDHAMU YA MUDA; hii inapaswa kufundishwa kwa vitendo. Zamani tulipokuwa tunasona tulikuwa tunawahi sana shuleni na hii ni kwasababu walimu walikuwa wanatoa adhabu kwa wachelewaji, hii ilikuwa ni moja ya njia bora kabisa ya kuwafundisha wanafunzi kutunza muda. Leo hii ukipita barabarani utakutana na watoto wanaenda shuleni saa mbili tena kwa mwendo wa pole! yaani hajali kabisa kwamba anakwenda wapi! Hii ni kwasababu hawajafundishwa faida za kutunza muda, tatizo hili linakuja kuwa kubwa zaidi pale kijana anapojiajiri. Ajira binafsi bila nidhamu ya muda huwezi kufanikiwa, ni lazima uwe na uwezo wa kujisimamia mwenyewe kwa kutunza muda wako. Hivyo walimu wanapaswa kuwafundisha wanafunzi kutunza muda ili watakapojiajiri wafanikiwe.

HITIMISHO; Nimeandika mengi Sana kuhusu mambo ambayo hayafundishwi shuleni ilihali yakifundishwa yanaweza kupunguza au kumaliza kabisa lawama za ukosefu wa ajira kwa vijana. Ushauri wangu kwa serikali yetu ni kubadilisha mfumo wa elimu yetu kwa kuanzisha mada ambazo zinaendana na maisha ya sasa, hakuna maana yeyote ya wanafunzi kujifunza mambo ambayo yamekwisha pitwa na wakati na ambayo hayawezi kuwasaidia kwenye ulimwengu wa sasa. Ujumbe huu pia uwafikie wazazi wote, kila mzazi anapaswa kujua kwamba yeye ndio mwalimu wa kwanza kwa mwanae, mzazi usitegemee mwalimu akufundishie mwanao kila kitu.

Mfunze mwanao kupika, kufua, kuosha vyombo, kutengeneza bustani, kwenda sokoni(kupanga bajeti), kumiliki vitu vidogovidogo kama kuku, sungura,nk. Usimnyime mwanao hela ukidhani kwamba ni tabia mbaya mtoto kumiliki hela, zoea kumpa mwanao hela halafu umfundishe matumizi sahihi na jinsi ya kutunza akiba, mfundishe kutumia simu kwa manufaa mazuri, simu Ina mambo mengi Sana chanya ambayo mwanao anaweza kujifunza na kufanikiwa kumuunganisha na dunia ya maendeleo.

KILA LA KHERI KWA WALIMU NA WAZAZI KATIKA MALEZI YA WATOTO WETU.
 
Back
Top Bottom