UCHUNGUZI uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhusu ajira za upendeleo kwa watoto, ndugu na jamaa za wakubwa ndani ya Benki Kuu (BoT), umekamilika.
Kukamilika kwa uchunguzi huo kulitangazwa mbele ya waandishi wa habari jana na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu.
Ingawa hakuwa tayari kusema kile kilichomo ndani ya taarifa hiyo kwa maelezo kuwa TAKUKURU ni taasisi inayojitegemea, Gavana Ndulu alisema, tayari BoT imeshaanzisha uchunguzi wake mwingine kufuatilia suala hilo hilo la ajira.
Gavana Ndulu alisema kuwa katika uchunguzi wake, TAKUKURU ilikuwa ikichunguza ajira za watu 14 wanaohusishwa na viongozi waandamizi kulingana na maelezo waliyopewa na ngazi husika.
Alisema baada ya kupata taarifa hiyo ya TAKUKURU, BoT nayo ikaamua kuanzisha uchunguzi wa ajira za wafanyakazi wake wote, ili kuepusha malalamiko kutoka upande fulani pamoja na kuepuka kupelekwa mahakamani.
"Wale TAKUKURU walifanya uchunguzi wa ajira za watoto wa vigogo kulingana na maelezo waliyopewa, lakini sisi tunataka kufanya uchunguzi wa ajira za wafanyakzi wote," alisema Ndulu.
Alisema kuwa ndani ya BoT kila mfanyakazi ni sawa, awe mtoto wa kigogo au wa mkulima, ndiyo maana wameamua kuwashirikisha wafanyakazi wote kwenye uchunguzi huo.
"Unajua leo hii ukifanya uchunguzi wa ajira za watoto wa vigogo pekee, kesho unaweza kujikuta hata hao watoto wa wakulima nao walipata ajira kwa njia zisizokubalika," alisema Ndulu.
Aidha, alisema uchunguzi wao utakuwa tofauti zaidi, kwani wao watafuata sheria ya mwaka 2004 (iliyobadilika), wakati TAKUKURU walitumia sheria ya mwaka 2000.
Ndulu hakuwa tayari kufafanua utofauti wa sheria hizo, lakini alidai kuwa katika uchunguzi huo, TAKUKURU haikutumia sheria iliyotumika kuwaajiri watoto hao.
"Hapa kunaweza kutokea tofauti ya kutokuelewana na jamii ikachukulia vibaya mambo haya, kwani sheria zilizotumika kufanya uchunguzi zilishabadilishwa, sasa sijui itakuwaje," alisema Ndullu.
Aidha, alisema ni vizuri jamii ikavuta subira ya kupata matokeo ya uchunguzi wa BoT kuhusiana na ajira za wafanyakzi wake na asingependa kutoa matarajio ya kazi hiyo mapema.
"Jamani nisingependa kuwaahidi nyinyi au wananchi wengine hivi sasa matarajio ya uchunguzi wetu, bali ninawaomba tungoje hayo matokeo," alisema.
Hivi karibuni, vyombo mbalimbali vya habari vilitoa taarifa na kutaja majina ya watoto wa vigogo ambao wanafanya kazi BoT, wakisadikiwa kuwa walipata kazi hizo kutokana na ushawishi au nafasi za ndugu zao.
Taarifa hizo pia zilinukuu viongozi wa TAKUKURU wakidai wanachunguza ajira za watoto hao wa vigogo kuona kama walipata ajira BoT bila kufuata taratibu zilizotakiwa.
Juhudi za Tanzania Daima kumtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hosea, kuthibitisha kukamilika kwa uchunguzi wa ajira za watoto wa vigogo hao ziligonga mwamba baada ya simu yake kutokuwa na majibu.
Taarifa kwamba kulikuwa na ajira za upendeleo ndani ya BoT kwa mara ya kwanza zilisambazwa katika mtandao wa intaneti kabla vyombo kadhaa vya hapa nchini kuripoti taarifa hizo.
CHANZO: Tanzania Daima