Watanzania wengi hawazingatii usafi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Watanzania wengi hawazingatii usafi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Oct 21, 2009.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Oct 21, 2009
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  UGONJWA wa kuhara ambao umeripotiwa kuwa wa pili kuwakumba Watanzania wengi baada ya Malaria huenda ukaendelea kuwatesa Watanzania wengi iwapo utaratibu wa kunawa mikono kabla ya kuandaa chakula na baada ya kushika uchafu hautapewa kipaumbele kinachostahili.

  Utafiti uliofanywa umebainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya watu hawanawi mikono baada ya kuwasafisha watoto wao waliojisaidia na hivyo kuchangia kula uchafu wakati asilimia 80 huandaa chakula kabla ya kunawa mikono na kuchagia kuwalisha uchafu wanaowaandalia chakula.

  Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa katika hotuba yake iliyosomwa wiki hii katika maadhimisho ya Siku ya Unawaji Mikono Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Wilaya ya Temeke ambayo HabariLeo Jumapili inayo, pia iliweka bayana kuwa asilimia 60 ya Watanzania hawanawi mikono baada ya kutoka ******.

  “Tunaungana na wananchi na wanaharakati mbalimbali duniani kote kuadhimisha Siku ya Kunawa Mikono Duniani. Lengo la kuanzishwa kwa siku hii ni kuleta msisitizo… katika suala la kunawa mikono … baada ya kutoka ******, kabla ya kuandaa na kupakua chakula, kabla ya kula na kumlisha mtoto na baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia.

  “Nasisitiza ni muhimu kunawa mikono kabla ya kula chakula au matunda. Kila familia ikiweka mkazo katika unawaji mikono, tatizo la maradhi yatokanayo na uchafu litapungua,” alisema Prof. Mwakyusa katika hotuba hiyo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Evansi Balama.

  Prof. Mwakyusa ambaye ni mtaalamu wa tiba ameasa kuwa unawaji mikono kwa sabuni utasaidia kupunguza magonjwa ya kuhara kwa takribani asilimia 40 na kwa kiasi kikubwa magonjwa ya mfumo wa hewa pia yatapungua.

  “Suala la usafi halina mjadala. Suala la unawaji mikono pia halina mjadala kwani utekelezaji wa jambo hili unachangia sana maendeleo ya nchi na kuondoa umasikini.
  “Taifa lenye watu dhaifu wanaosumbuliwa na magonjwa haliwezi kusonga mbele kwani linabeba mzigo mkubwa wa kutibu watu wake na sehemu kubwa ya bajeti yake huenda kwenye tiba,” alisema Prof. Mwakyusa.

  Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2009/2010, sekta ya afya ilikuwa miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele kwa kutengewa fedha nyingi. Sekta nyingine zilizopewa kipaumbele ni miundombinu na elimu.

  Pia Ripoti ya Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Afya (HSPPR) ya mwaka 2008 ambayo HabariLeo Jumapili inayo imebainisha kuwa bajeti ya sekta ya afya imekuwa ikiongezeka na malengo yamewekwa kuwa sehemu kubwa ya bajeti hiyo itumike katika ngazi za wilaya na shughuli za kudhibiti magonjwa kuliko kutibu.

  Aidha ripoti nyingine ya Bajeti ya Kaya (HHBS) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Januari mwaka huu, imebainisha kuwa ugonjwa wa kuhara ndio wa pili kwa kuwashika Watanzania mara nyingi zaidi baada ya ugonjwa wa Malaria.

  Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Watanzania wengi watoto kwa watu wazima walipoulizwa kuhusu ugonjwa walioupata mara kwa mara, zaidi ya asilimia 60 walitaja malaria na kufuatiwa na kuhara.

  Alisema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatambua kuwa matumizi ya elimu na maarifa ya unawaji mikono kwa maji safi na sabuni vitawezesha kufikia lengo la unawaji mikono kwa asilimia 100.

  Alibainisha kuwa Tanzania ikifanikiwa kuelimisha umma kunawa mikono, itafanikiwa kuchangia lengo la saba la milenia la kupeleka huduma za afya na usafi kwa wale wanaokosa huduma hizo kwa kiwango kikubwa.

  Prof. Mwakyusa pia alisema baada ya kuhamasisha kunawa mikono katika siku hiyo. Wataendelea kuhamasisha usafi katika maaadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Duniani itakayofanyika Novemba mwaka huu na pia kutakuwa na uhamasishaji wakati wa Wiki ya Usafi ya Kimataifa.

  Licha ya uhamasishaji huo, pia Prof. Mwakyusa alisema serikali inaandaa Sera ya Afya na Usafi wa Mazingira ambayo inatarajiwa kukamilika mwakani na tayari Bunge limeshatunga Sheria ya Afya na Jamii kwa nia hiyo hiyo ya kukabiliana na changamoto za usafi wa mazingira na tabia ya usafi.
  http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=3910
   
Loading...