SoC01 Waraka wa Wanyama kwa Binadamu

Stories of Change - 2021 Competition

Dizasta Vina

Member
Jul 15, 2021
15
37
Salamu waja.
Waraka huu utumike kama mashitaka kwa binadamu kwa kushindwa kuishi kwenye daraja la ustaarabu wake, kushindwa kuwajibika na kutumia vyema vipawa alivyozawadiwa na asili. Namtuhumu binadamu kwa kuwa kiumbe mbaya sio tu kwa wanyama wengine na mazingira, bali hata kwa binadamu wenzake. Namtuhumu kwa kuwa MJIVUNI, MNAFIKI, MCHOYO, MWONEVU, MUUAJI, MWONGO, MKATILI, MJINGA, MSHENZI na MBINAFSI na nipo tayari kusimamia tuhuma hizi kwa niaba ya wanyama wengine wafugwao na wasiofugwa. Kwa kuanza, nina maswali makuu kwake.

Amestaarabika?

Nina shaka na maana na kipimo cha ustaarabu kwa sababu kuu mbili.
- Moja, uhalisia hauonyeshi hivyo, ni ngumu kujadili ustaarabu na kiumbe ambaye amemiliki na kuuza binadamu mwenzake kama bidhaa kitumwa, ametoa sadaka ya damu, amepigana vita kadhaa akigombea miliki ya ardhi, mipaka na rasilimali ambazo akifa anaziacha, anabagua haki ya umiliki wa rasilimali kwa kigezo cha jinsia na rangi, ukabila au utaifa na pia ngumu kujadili ustaarabu na kiumbe anayefuga majeshi kujilinda na binadamu wenzake. Hizi na nyingine nyingi si dalili za kustaarabika.

- Pili, vyote (maana na kipimo cha ustaarabu) vimewekwa na yeye binadamu, kumjadili binadamu bila muktadha linganishi nje ya jamii yake. Labda ndiyo maana ustaarabu unapimwa kwenye kutendea usawa kwa binadamu tu na si viumbe wengine na mazingira (UBINAFSI). Kifupi kwenye mtihani, mtunzi ni binadamu, mfanyaji ni binadamu na msahihishaji ni yeye mwenyewe.

Tukikubali binadamu kastaarabika, viumbe wengine wanafaidikaje na kustaarabika kwake?

Asili imemjaalia binadamu nguvu kuu tano,
  • Ufahamu, Uwezo wa kupokea na kutafsiri taarifa kwa muktadha na maana sahihi kiasi kuweza kufanya mrejesho stahiki.
  • Mantiki, Uwezo wa kupangilia mawazo kwa uyakinifu wa kimaana na kimuktadha.
  • Kutambua kuwa anaishi na kurindima na maisha, na kuhisi thamani ya uhai (being sentient)
  • Kidole gumba kinachozunguka (Opposable thumb) kinachomuwezesha awe msanii, kiasi ameunda, umeumba, amechora, amejenga n.k.
  • Lugha.
Hivi vipawa ni muhimu. Kwanini ni muhimu pia kwa viumbe wengine? Binadamu ni Kiumbe wa kijamii (a social being), ana majukumu ya kijamii (kwa viumbe na mazingira). Kuyafunga majukumu hayo kwa binadamu pekee ni UCHOYO. Wanazuoni walisema, palipo na nguvu kubwa, pana jukumu kubwa, (where there is a great power, comes great responsibility). Ni muhimu kuhakikisha anashirikisha viumbe wengine mafanikio ya karama hizi na si kuwasababishia changamto tu.

Kumiliki mnyama kunakinzana na dhana ya kustaarabika?

Miaka na miaka binadamu amemiliki mnyama kwa chakula, ulinzi, urembo, mavazi n.k, kama kumiliki mnyama kwa ajili ya mavazi na urembo si haja kuu ya asili ya maisha kwa binadamu, vipi kuhusu mnyama kama chakula? Je, binadamu aliumbwa kula nyama kiasili ? na tunamtambuaje mnyama mla nyama kiasili?

Tuchunguze jedwali
SIMBABINADAMU
Ana kasi ya kukimbiza windoHana kasi ya kukimbiza windo anatumia mitego, silaha na kulaghai (kufuga)
Ana kucha za kuraruaHana kucha za kurarua, anatumia nyenzo mfano kisu
Ana machonge ya kuchanaHana machonge ya kuchana, anatumia nyenzo
Ana mataya yenye nguvu ya kutafuna nyamaHana mataya yenye nguvu ya kutafuna, anaunguza na moto na mafuta/maji kwanza
Mfumo wake wa kumeng'enya unaweza kumeng'enya nyamaMfumo wake wa umeng'enyaji hauwezi kumeng'enya nyama mpaka iunguzwe
Nyama ni chakula kikuu, hana mbadala wa chakula zaidi ya nyamaNyama si chakula kikuu ni ziada
Anawinda kwa ajili ya haja ya asili ambayo chakula tuAnafuga kwa ajili ya haja za ziada kama ladha ya muda mfupi, na kuzalishia bidhaa kama mavazi na mikoba

Utagundua kuwa binadamu aliundwa na asili kuwa mwokota matunda, mchimba mizizi, mbegu na mboga mboga. Mikono yake, kucha zake, meno na mfumo wake wa uvunjaji chakula vyote vinaonyesha binadamu ni Herbivore.

UTUMWA NA UFUGAJI
Utumwa ni pale ambapo binadamu mmoja anammliki binadamu mwingine kama bidhaa au mali kwa ajili ya matakwa binafsi kama uzalishaji na usaidizi BILA RIDHAA YA ANAYEMILIKIWA na pia bila malipo au marejesho (consideration/remuneration).
Ufugaji ni pale ambapo binadamu anammiliki mnyama kwa ajili ya chakula, usaidizi na sababu nyingine binafsi.
Kuna mstari mwembamba sana kati ya maana ya utumwa na ufugaji.

Umiliki wa kiumbe mwenye nafsi, damu, nyama na mifupa na ufahamu bila idhini yake wala makubaliano kwa sababu binafsi haitofautiani sana kimaana na utumwa kama ambavyo kuchinja kwa ajili ya chakula hakutofautiani na UUAJI

tuchunguza jedwali la 2
UTUMWAUFUGAJI
Binadamu ni bidhaa/mali/kizalisha maliMnyama ni bidhaa/mali/kizalisha mali
Binadamu ananunulika/kuuzika kubadili umiliki (transfer of ownership)Mnyama ananulika/kuuzika kubadili umiliki
Hakuna thamani ya ndani ya mtumwa bali ile inayopimwa na nguvu yake ya uzalishaji/utimizaji wa haja ya mmiliki (no intrinsic value).MFANO Binadamu ni bora akiwa anazalisha bidhaa, mrembo kumvutia mmiliki n.kHakuna thamani ya ndani bali ile inayopimwa na nguvu ya uzalishaji/utumizaji wa haja ya mmiliki (no intrinsic value). MFANO Ngómbe ni mzuri akiwa anazaa au kuzalisha, anatoa maziwa kwa ajili ya mfugaji n.k
Hakuna marejesho/malipo kwa anayemilikiwaHakuna marejesho/malipo kwa anayemilikiwa
Miaka bora ya anayemilikiwa (akiwa na nguvu na afya) ni miaka ya kumtumikia mmiliki
Mf. binadamu mwenye nguvu, kijana, mrembo , mwenye kasi anamtolea hizi zawadi zote mmiliki na si kwa ajili yake
Miaka bora ya mnyama (akiwa na nguvu na afya) ni miaka ya kumtumikia mmiliki. mf. Ng'ombe akiwa na maziwa mengi si kwa ajili ya ndama wake bali ni kwa ajili ya mfugaji, akiwa na afya ni kwa ajili ya chakula cha mmiliki na si kwa ajili ya maisha yake
Halali kidini na kijadiHalali kidini na kijadi
Haramu kisheriaHalali kisheria

Licha ya mfanano huo, kimoja ni halali na kingine ni haramu kisheria. Hapo unagundua legality is not about morality. Kwanini hizi tuhuma ni valid kumwelekea binadamu, hasa ikiwa wapo viumbe wengine wanakula wanyama wenzao? Kwa kiumbe anayenadi ufahamu, mantiki na kustaarabika ni mashitaka stahiki kabisa.

Mimea nayo ni viumbe?

Mimea ni viumbe lakini wamekosa kitu kimoja muhimu, Sentience, uwezo wa kujua iko hai na kuwa na vitambuzi vya hali tofauti uhai (furaha na huzuni, hasira, wivu, kero baada ya bugdha, upendo, huruma, tamaa au hamu ya ngono) (si maelezo rasmi ila maana sahihi). At least haijathibitika kuwa mmea una huu utambuzi hasa kwakuwa unahitaji ubongo au mfananao wa ubongo kiufanyaji kazi kutafsiri hisia hizi. Labda ndio maana ni bora kuanza kula mimea kabla ya wanyama wenzio. Kama ambavyo hawezi kumla binadamu mwenzake palipo na ngombe, ndivyo ambavyo hawezi kumla ngombe palipo na matunda. Inaitwa kupima degree of necessity. Asili haijaonyesha binadamu hatakiwi kula viumbe, La hasha imeonyesha hatakiwi kula wanyama.
WAZO 2 ukiwa kwenye mtumbwi uliopotea baharini, yapo matunda, nyani mmoja, mbuzi mmoja na mtoto mdogo. Ukiwa kwenye hali ya kawaida kiakili utaanza kula matunda kisha mbuzi, kisha nyani alafu inapobidi kutimiza golden rule kuwa hakuna bora zaidi ya uhai wako utamla binadamu kwa mapambano. Nje ya hii order ni shaka la ufahamu.

Ipo nafasi sawa ya kupigania uhai kwa viumbe walao nyama?

Kiasili, kila kiumbe mla nyama ameundwa na nafasi sawa ya kupigania maisha. Ndio maana simba anaingia mawindoni kupambana na swala ambaye naye asili ilimuunda kujua na kukimbia hatari. Simba atapambana na atapata chakula kimoja kwa wakati mmoja, inaitwa fair chance to fight for survival na ipo kwa ALL SENTIENT BEINGS. hii ni sawa kwa chui, duma, mamba n.k isipokuwa binadamu. Binadamu ana njia zisizo za asili kupata chakula kwa sababu sio chakula chake cha asili. moja ya sadaka anazotoa ni kutotoa nafasi sawa kwa viumbe wahanga kupigania maisha yao akiamua kuwafuga, kuwategea mitego au gesi za sumu si nafasi sawa ya kupigania uhai. Kama binadamu ana akili ya kuunda vifaa haimaanishi ana uhuru wa kutumia vifaa hivyo kuumiza. MWONEVU.
WAZO 3 Maluweluwe ni kusema virutubisho muhimu vinapatikana kwenye wanyama tu. Ni binadamu tu anashinda kwenye viwanja vya mazoezi kupunguza mwili, ni binadamu tu anasumbuka na Obesity (unene kupita kawaida) na ni binadamu tu anayeumwa magonjwa ya moyo. Kiasilia kundi la primates wote ni wala mimea, kama Orangutani, Bonobo, chimpanzii n.k ni wanyama wa karibu na binadamu kibaiolojia, kifiziolojia na kianatomia, binadamu hawezi kusimama nao hata kidogo kwa nguvu, kasi au ustahimilivu dhidi ya kiu, njaa na maradhi na ni wala mimea. Labda tuwaulize mamalia wakubwa zaidi mwituni Tembo na Kifaru wanapata wapi virutubisho ikiwa wao pia ni wala mimea? Virutubisho ni sababu ya UONGO

Mungu kaumba wanyama kuliwa na binadamu?

Mungu anayeshuhudiwa na binadamu aliumba wanyama waliwao kama chakula akawapa milango ya fahamu. neva za maumivu, hofu na haja kuu ya kuishi. Rudia hiyo sentensi iliyopita tena. Mnyama anapochinjwa anasikia maumivu kwakuwa ameumbiwa vihisi maumivu, anasikia dhuruma kwakuwa ameumbiwa haja ya kuishi na anasikia hofu kwakuwa pia ameumbiwa wasiwasi. Mungu wa huruma na upendo kwa binadamu tu, alishusha kitabu cha uongozi kwa binadamu tu kuruhusu matumizi ya wanyama kama chakula. Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, hizi ni busara za vitabu vinavyosemwa ni vitakatifu na vina elimu na busara zisizo na kipimo.
WAZO 4. Basi nami nakuja na Kitabu cha Mungu wangu, Mungu wa wanyama, Mungu anaitwa ASILI, dini inaitwa MANTIKI na dhambi pekee ni kuwa MJINGA.

Ni Mungu yupi ambaye hajajua daraja la juu zaidi la ustaarabu,upendo na huruma?
Kupenda, kuheshimu na kulinda binadamu ni daraja la ustaarabu, Kupenda, kuheshimu na kulinda wanyama ni daraja la juu zaidi la kustaarabika. Binadamu wastaarabu hawajajua daraja hili, Lakini cha ajabu ni kwamba hata nguvu kuu ya imani zao (MUNGU) naye hajajua daraja hili la juu la kustaarabika. Kama ambavyo tumesubiri miaka na miaka Utumwa na biashara yake kutangazwa ni haramu, basi tusubiri miaka mingine mingi biashara ya kitumwa ya wanyama iwe haramu. AU TUSUBIRI MPAKA SIKU WANYAMA WAONGEE KUWA WANAONEWA NDIO TUAMINI?
WAZO 5. Unahitaii Mungu kusema jambo ni baya ili liwe baya? Na je, jambo ni baya kwa sababu mungu kasema au ni baya ndiyo maana mungu kasema?

Binadamu ni wa maalumu kuliko viumbe wengine?

Kujua umuhimu na umaalumu wa kitu ni kupima changamoto kipindi hakipo. Hii ni mifano ya kimantiki ya yatayotokea ikiwa binadamu atatoweka. Joto litapungua kwa sababu hewa ya kabonidioksaidi itapungua. Hewa hii inazuia joto kuondoka duniani. Binadamu anazalisha zaidi hewa hii kwa kuunguza ghafi za kaboni na visukuku(fossils) kwa shughuli mbalimbali binafsi, Ozoni itafunga kabisa kwa sababu inapata mushkeli kwa uzalishaji wa hewa chafu unaotokana na shughuli za kibinadamu, Uzalishaji wa chupa za plastiki utaisha, kelele za viwanda na vyombo moto zitaisha, Uharibifu wa mazingira kwa sababu ya vita na shughuli nyingine kama uchimbaji madini, kilimo na ujenzi utaisha. Udongo utasheheni rutuba, kifupi dunia itapona vidonda.
Umuhimu wa binadamu upo wapi? Ikiwa Phytoplanktoni inazalisha karibia asilimia 70 ya oksijeni duniani, Nyuki ambao ni wachavushaji wa karibia theluthi moja ya mimea inayomea ardhini kwa njia hiyo kuzuia dunia nzima kuwa jangwa? Minyoo midogo ya udongoni wanaendesha mzunguko wa rutuba udongoni? viumbe ambao wakiondoka sio tu binadamu atakufa bali hata dunia itatikisika.
Umaalumu wa binadamu upo wapi? ikiwa ameundwa na vijenzi vile vile vilivyounda sehemu kubwa kama si yote ya ulimwengu, Hidrojeni, Oksijeni, kaboni na Nitrojeni. Namtuhumu binadamu UJIVUNI wakati vipo asivyoviweza, asivyovijua na vipo muhimu na maalumu zaidi yake.
Kama ni maalumu kwa sababu ya uwezo wa kuongea, kuwasiliana, kujenga n.k basi tai ni maalumu kwa sababu anaona mbali, kinyonga ni maalumu kwa sababu anaweza kunakiri rangi za mazingira akinuia kujificha, popo ni muhimu analala akining'inia kichwa chini miguu juu, ndege anapaa, samaki wanapumua kwenye maji. Umaalumu unapotea ikiwa kila mtu ana kipawa chake.

Je kufuga na kula ni vyema kwa sababu imehalalishwa kisheria?

being legal, does not mean moral. Kitu kuwa halali haimaanishi ni adilifu. Miaka kadhaa nyuma utumwa ulikuwa ni halali, ukeketaji wa mabinti ulikuwa ni halali na mpaka sasa binti analipiwa mahari akibadilishiwa mji wa mwanaume kutoka kwa baba kwenda kwa mume, haina maana ni adilifu. Kuweka sheria zinazohalalisha ubazazi ni sababu tu ya UBINAFSI.

JE,BADO BINADAMU NI MSTAARABU?

Kuwa mstaarabu ndio uongee ustaarabu, acha kuuza binadamu wenzio, ndio uongee ustaarabu, acha kukandamiza wanawake, watoto, maalbino na walemavu wengine ndio uongee kuhusu ustaarabu. Acha kubagua umiliki wa rasilimali kwa kigezo cha rangi na jinsia ndio uongee kuhusu ustaarabu, acha kulipia au kukubali malipo ya mahari na kukeketa wanawake ndio uongee ustaarabu. Linda mazingira , acha kupigania mipaka ya kuchorwa kwenye karatasi ndio uongee kuhusu ustaarabu. Acha kuwagawia watoto makabila na dini, concepts zinazoishi vichwani zikiwagawa kiasi kuchukiana na mwisho, acha kuonea wanyama ndio tuongee kuhusu ustaarabu. Kwa yeyote ambaye ataona picha hizi mbili chini ni tofauti basi hayuko tayari kuanza safari ya kustaarabika. Kwa niaba ya wanyama wote, Nawasilisha!
imgonline-com-ua-twotoone-SmGWR7asKoXoYy.jpg
imgonline-com-ua-twotoone-hVIUvGIFyWBrGyV.jpg
 
Dizasta vina ndio future yako, ni kama kijogoo uliyemkwepa mtaani afu ukamkuta kwako.../

Umetishaa mwamba
 
Salamu! pongezi sana kwako Dizasta kwa uandishi huu makini uliojitofautisha! uandishi wako umewasilisha mawazo muhimu sana kwa ustadi wa hali ya juu, pia andiko limepambwa na lugha tamu sana, maana nimejifunza misamiati mipya ya kiswahili hapa.

Hili andiko lisipochukua nafasi ya kwanza ya ushindi basi wanaohusika kwenye mchakato wa kuchagua washindi watakuwa hawajasoma andiko hili.

Nina mambo machache ya kujadili hapa kwenye andiko hili makini.

Kwanza ni kuhusu wazo la mwandishi kuwa asili haikumuunda binadamu ale nyama kwa kuangalia uwezo na maumbile ya mwili wa binadamu mfano kukosa uwezo wa kumeng'enya nyama mbichi au kukosa makucha au meno makali ya kuwakabili wanyama. Sidhani kama ni sahihi kwa sababu vipo vitu hai vingine kama mizizi ya mimea, mayai ya ndege na vingine tunahitaji kuviunguza kwanza ili kuvila, swali ni je? binadamu hatukuundwa kula mayai au majani? Utagundua kwamba tunaunguza au kuchemsha nyama, mayai, mizizi, au matunda kwa sababu kama afya(kuhakikisha tunapunguza au kuondoa uwezekano wa kuambukizwa na bacteria au minyoo inaoweza kuwa kwenye nyama mbichi), kupata ladha tofauti ya chakula, kulainisha chakula kuusaidia mfumo wa mmeng'enyo wa chakula kufanya kazi yake kwa ufanisi wa hali ya juu.

Pili, wazo la mwandishi kwamba Primates ni herbivores, Sidhani pia kama hii ni sahihi sababu wanyama waliopo Order ya PRIMATES tukiondoa binadamu(Homo sapiens) wanakula wanyama wengine pia kama ndege na mayai yao, wadudu, na vingine. Binafsi nimewahi shuhudia tumbili akila kifaranga cha kuku.

Ukijifunza vizuri utagundua tabia ya vitu hai zinabadilika kulingana na mazingira kubadilika kila siku, vitu ambavyo vitashindwa kubadilika kuendana na mazingira husika mara nyingi hushindwa kuishi(The survival of the fittest theory by Darwin). Binadamu ni moja ya vitu hai vyenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na mabadiliko ya mazingira yake kuhakikisha anaishi, matumizi ya moto, matumizi ya silaha kuwinda wanyama na mabadiliko mengine nayaona kama adaptations za binadamu kwenye mazingira yake ambayo ni mafanikio yake! Sikatai kuhusu athari za hayo mafanikio yake kwa mazingira(wanyama wakiwemo).

Tatu ni kuhusu umuhimu wa binadamu kwenye hii sayari na ulimwengu pia. namnukuu mwandishi "kujua umuhimu na umaalumu wa kitu ni kupima changamoto wakati hakipo" nafikiri tunaweza kujifunza umuhimu wa binadamu vizuri kama watatoweka hapa duniani. Kila kitu hai na vingi visivyo hai vina nafasi yake kwenye ikolojia ya sayari hii, ukikiondoa kimoja lazima kutakua na imbalance of nature hata kama wakati athari yake si kubwa kuweza kuonekana wazi.

Ni muhimu tujifunze kuheshimu maisha, iwe ni kwa binadamu, mnyama, mdudu, mmea n.k ilimradi ni maisha. Mwandishi ameeleza kuwa hatujui kama mimea ina hisia kama kuumia au kuhisi kuwa inaishi, hii sio sababu ya kutufanya tusiheshimu uhai wa mimea pia. Najutia kuwahi kukata mti au sehemu ya mti(hata jani moja) bila kuwa na sababu ya muhimu ya kufanya hivo, kwa sababu mmea husika unakuwa umetumia muda mrefu na nishati nyingi kuteneneza jani lake moja, kulikata bila sababu ni ukorofi, kutojali na kutoheshimu maisha.

Binadamu si vitu hai pekee wenye tabia ya kugombea rasilimali zinazowazunguka licha ya ukweli kwamba wakifa wataviacha. wanyama, ndege, hata bacteria pia hupigana sababu ya nafasi kwa kwa lugha ya kiikolojia inaitwa Territorial behaviour. vitu vingi vilivyo hai vina kawaida hiyo.

Binadamu tumekuwa chanzo cha kuhatarisha maisha ya vitu vingine hai, na kusababisha kupotea(extinction) kwake pia, lazima tutafakari upya namna tunavyoishi.
 
Asante kwa kusoma, kupongeza na kukosoa
 
Back
Top Bottom