Wanne wahukumiwa kunyongwa kwa kuua albino Tanzania

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,331
33,147
mahakama_geita.jpg

Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mlemavu wa ngozi, Zawadi Magimbu (32) wakiwa ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita baada ya kuhukumiwa kunyongwa. Kutoka kushoto ni Nasoro Charles, Singu Siantemi, Masaru Kahindi na Ndahanya Lumola. Picha na Jackline Masinde.

KWA UFUPI

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Joacquine De-Mello wa Mahakama Kuu, ambaye alisema alisema Mahakama imeridhika pasi na shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kwamba walihusika moja kwa moja na kifo hicho.



Geita/Dar. Watu wanne wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na kosa la kumuua Zawadi Magindu (32) mwenye ulemavu wa ngozi, mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Wilaya ya Geita mkoani hapa.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Joacquine De-Mello wa Mahakama Kuu, ambaye alisema alisema Mahakama imeridhika pasi na shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kwamba walihusika moja kwa moja na kifo hicho.

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Nassoro Charles mkazi wa Kijiji cha Beda mkoani Kagera, Masaru Kahindi mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Ndahanya Lumola na Singu Nsiantemi wakazi wa Kijiji cha Kakoyoyo, Wilaya ya Bukombe.

Jaji De-Mello alisema washtakiwa walifanya kosa hilo Machi 11, 2008 saa 1:00 usiku nyumbani kwa akina Zawadi wakati wakipata chakula cha usiku, walimkata kwa shoka na panga miguu yote na mkono wa kulia.

Alisema Masaru Kahindi aliyekuwa jirani na Zawadi, Nassoro Charles aliyekuwa mume wa marehemu walivamia nyumbani kwao wakati wanapata chakula cha usiku, huku wakiwa na panga na shoka kisha kumkata miguu na mkono wa kulia .

“Watu hao walikwenda na shoka na panga, walitumia shoka kumkata Zawadi huku mama yake Magdalena Mashimba na mjukuu wake, Semen Hamisi wakipigwa na kutupwa nje na wauaji hao,” alisema Jaji De-Mello.

Aliendelea kusema kuwa, wakati wanamkata Zawadi, mtoto wake Semeni alijibanza mlangoni na kuwatambua wauaji hao kuwa mmojawapo alikuwa mume wa mama yake na mwingine jirani yao.

“Walionwa na shahidi Magdalena na Semeni waliwatambua kwa sauti na mwonekano, kwani wakati wanafanya hivyo kulikuwa na mwanga wa mbalamwezi,” alisema.

Pia, Jaji De-Mello alisema washtakiwa Ndahanya na Nsiantemi walikuwa wafanyabiashara wa viungo vya albino, walikamatwa na polisi baada ya kutegewa mtego.

“Polisi walikuwa kwenye operesheni ya kuwatafuta watu wanaojihusisha na vitendo vya kuua albino, walipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna watu wanataka viungo vya albino ndipo walipotafuta albino wawili, mmoja akiwa mtoto na mwingine mtu mzima,” alisema.

Alisema baada ya kutegwa mtego huo walikamatwa washtakiwa wawili; Ndahanya na Nsiantemi ambao walikiri kuhusika na mauaji ya Zawadi na kuchukua viungo hivyo, kisha kuvipeleka kwa mganga wa jadi, Mussa Ally mkazi wa Katoro ambaye alihusika kuvipima ili kujua iwapo vina ubora.

“Wakati watu hawa wanahojiwa na polisi waliwataja wenzao wengi ambao hapa mahakamani hawapo sijui ni kwa nini… wakiongozwa na Robert Kagoma ambaye ndiye alikuwa wakala wa kulangua viungo hivyo na kuvipeleka kwa mganga wa jadi aliyetajwa kwa jina la Gerald Mazuri ambaye pia huviuza kwa ‘wazungu’ Geita,” alisema Jaji De-Mello.Jaji De-Mello alisema Ndahanya alipohojiwa alikiri kuhusika na rafiki yake Robert kutafuta walipo albino, waligundua kuwa kuna albino Kijiji cha Nyamaruru na walipopanga mbinu na kutafuta watu wa kukata mapanga ambao walifanikiwa kumkata Zawadi.
“Baada ya kukata walichukua viungo hivyo na kuvipeleka kwa mganga Ally kwa ajili ya vipimo, ili kujua kama vina kidhi mahitaji kusudiwa, walipima viungo hivyo kwa kutumia redio, shilingi moja ya zamani na wembe lakini vipimo hivyo vilionyesha viungo hivyo havikuwa na ubora,”alisema.

Alisema kutokana na ushahidi wa mama yake Zawadi na mtoto wa miaka 11, unaonyesha Kahindi na Nassoro walionwa wakiua, mwonekano wa wao ulionyeshwa mahakamni na mashahidi hao.

“Sina budi kusema watu hawa wanahusika,” alisema Jaji De-Mello.

Kuhusu Ndahanya na Nsiantemi, alisema ushahidi unaonyesha walikiri kufanya biashara hiyo baada ya kunaswa kwenye mtego wa polisi kwa maandishi.

“Nitamke kuwa kutokana na matatizo ya mauaji ya walemavu wa ngozi kuongezeka kila kukicha, mauaji haya ni ukatili, hivyo nimewatia hatiani kwa kuhusika na kifo hiki kwa mujibu wa sheria kifungu cha 199 na 197 cha kanuni ya adhabu, kifungu namba 16 mnahukumiwa kunyongwa hadi kufa,” alisema Jaji De-Mello.

Tangu mwaka 2007 hadi 2015, Wilaya ya Geita zaidi ya albino sita wameuawa huku wengine wanne wakijeruhiwa kwa kukatwa viungo vyao.

Hukumu hiyo ni ya 16 kitaifa kutolewa kuhusiana na mauaji ya albino na kwa Mkoa wa Geita ni ya kwanza.

Wadau wapongeza

Mbunge wa Lindi Mjini Salum Barwany ambaye ni mlemavu wa ngozi, amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha anatia saini hukumu hiyo ili utekelezaji ufanyike haraka iwezekavyo.

Alisema imekuwa ni jambo la kawaida kwa adhabu hizo kutolewa lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu hali inayosababisha wahusika kuendelea kuwepo.

“Ningemuomba Rais kabla hajamaliza muda wake achukue hatua hiyo ninayoweza kusema muhimu kwetu na itamfanya akumbukwe siku zote, hususani katika suala kubwa kama hili,” alisema Barwany Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu anayewawakilisha watu wenye ulemavu wa ngozi bungeni Al-Shaymaa Kwegyir alisema adhabu hiyo ni sahihi kwa kuwa wahusika walionyesha kukusudia kuua.
“Nimefarijika kuona hatimaye Serikali imesikia kilio chao na kuanza kutoa adhabu ambayo itakuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo.”

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHR,C Dk Helen-Kijo Bisimba alisema licha ya kuwa adhabu hiyo inalenga kukomesha vitendo hivyo vya kinyama, lakini inakiuka haki za binadamu.

Alifafanua kuwa kuna haja ya kuangaliwa upya kifungu cha adhabu ya kifo na kuondolewa kwenye sheria, huku wanaofanya makosa ya mauaji wakihukumiwa kifungo cha maisha.

“Kwa kosa walilofanya wanastahili adhabu kubwa ambayo binafsi naona kifungo cha maisha kingewafaa zaidi, ili wakiwa huko waweze kujifunza na kujutia makosa yao lakini siyo kuwaua,”alisema. chanzo.Wanne wahukumiwa kunyongwa kwa kuua albino Tanzania - Kitaifa - mwananchi.co.tz

HATA MIMI NINAMUUNGA MKONO JAJI ALIYE WAHUKUMU KIFO HAWA WAUWAJI WA WALEMAVU WA

NGOZI (ALBINO) NA WANYONGWE ILI IWE FUNDISHO KWA WATU WENGINE.




 
17 kunyongwa mauaji albino.


JK-06March2015(1).jpg

Rais Jakaya Kikwete, akisalimiana na Mariam Stanford, aliyekatwa mikono yote miwili, baada ya kukutana na viongozi wa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Halima Kambi


Watu wanne waliohukumiwa jana na Mahakama Kuu kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuua albino, wameongeza idadi ya waliokwisha kutiwa hatiani ili wanyongwe kwa kosa hilo kufikia 17 nchini.

Idadi hiyo imeongezeka baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kuwatia hatiani watu wanne jana kwa mauaji ya mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi yaliyofanyika mwaka 2008.

Kabla ya jana, watu 13 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa kutokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo kadhaa ya Tanzania hususan mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na imani za kishirikina.

HUKUMU YA JANA
Watu wanne akiwamo mume wa marehemu, walihukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mlemavu wa ngozi, Zawadi Mangidu (22), mkazi wa Nyamalulu, Kata ya Kaseme, wilayani Geita.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, huku ndugu wa waliohukumiwa adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa ambao walikuwa miongoni mwa wakazi wengi wa mji huo waliofurika mahakamani hapo kushuhudia hukumu hiyo, wakiangua vilio.

Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Masalu Kahindi (54), Ndahanya Lumola (42), Singu Nsiyantemi (49) na Nassor Said (47), mume wa marehemu Zawadi Mangindu.

Mahakama hiyo iliwahukumu watu hao ambao ni wakazi wa wilaya hiyo, baada ya kupatikana na hatia ya
kula njama na kushiriki kumuua kwa kukusudia mlemavu huyo wa ngozi.

UAMUZI WA JAJI
Akitoa hukumu hiyo, Jaji De-Mello, alisema amezingatia kwa makini na tahadhari kubwa katika kufikia uamzi huo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi 12 wa upande wa mashtaka na utetezi, kwamba washtakiwa walitenda kosa hilo bila kuwa na shaka yoyote.

Jaji De-Mello alisema katika hukumu zilizotangulia, pia zilibainisha kuwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamekuwa yakitekelezwa na mtandao mkubwa na siyo rahisi kuubaini kirahisi.

Jaji De-Mello alielekeza kufikishwa mahakamani wanunuzi wa viungo vya watu wakiwamo wenye ulemavu wa ngozi na waganga wanaopiga ramli.

Jaji alisema kwamba wauaji pekee ndiyo wamekuwa wakifikishwa mahakamani dhidi ya vitendo hivyo vya kinyama.

Alisema alijaribu kufanya utafiti mdogo kwa kutoka nje saa moja usiku akiwa nyumbani kwake na kubaini kuwa kwa mazingira ya Geita ni rahisi kumbaini mtu anayefanya tukio kama hilo.

Alisema wakati tukio hilo linatokea ilikuwa rahisi kwa wenyeji (watuhumiwa) kubainika.

Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Hezron Mwasimba, akisaidiana na wakili Janeth Kisibo, ulidai kuwa washtakiwa kwa pamoja kwa makusudi walishirikiana kula njama na kutenda kosa la kumuua mlemavu huyo wa ngozi, saa moja usiku, Machi 11, mwaka 2008 katika kijiji cha Nyamalulu kata ya Kaseme wilayani Geita.

Uliongeza kuwa mbali na kumuua mlemavu huyo wa ngozi, wahukumiwa hao pia walimjeruhi kwa panga mtoto wa marehemu, Chausiku mwenye umri wa miezi tisa, katika mkono wake.

Upande wa mashitaka uliendelea kudai kuwa washtakiwa walikamatwa kwa nyakati tofauti na taratibu za kisheria zilizingatiwa ikiwa ni pamoja na kupewa nafasi ya kutoa maelezo ya onyo na kutoa ungamo, kisha kufikishwa mahakamani na upande wa Jamhuri ukiita mashaihdi wake 12 ambao walitoa ushahidi.

Uliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washtakiwa ili kuwa fundisho kwa watu wengine wanaohusika katika vitendo hivyo vya mauaji ya watu wakiwamo wenye ulemavu wa ngozi.

Wakati wa kesi hiyo, upande wa mashitaka ulidai kuwa washtakiwa walipokea Sh. 250,000 kati ya Sh. 1,250,000 kutoka kwa wakala wa kununua viungo vya marehemu na baada ya kuvifikisha mahali husika, ilibainika kuwa havikuwa na kiwango cha ubora unaotakiwa.

Kutokana na hilo, wakala wao ambaye alitajwa mahakamani hapo kuwa ni Hamis Hamad, alikataa kumalizia kiasi cha Sh. milioni moja kilichokuwa kimesalia.

Ilidaiwa kuwa baada ya mlemavu wa ngozi kuuawa, viungo vyake hufanyiwa utambuzi wa ubora wa viungo vyake kwa kutumia wembe, redio na sarafu ya Shilingi kumi kwa kugusishwa kwenye redio ambayo hukwaruza na kupiga kelele.

Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo kutolewa, Jaji De-Mello alitangaza iwapo kuna yeyote anaweza kukata rufaa.

Hukumu hiyo imetolewa huku kukiwa na mfululizo wa matukio ya kinyama kwa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini akiwamo mtoto Yohana Bahati, ambaye aliuawa mkoani humo na mama yake kujeruhiwa vibaya huku mtoto mwingine akiibwa katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa hakuna taarifa yoyote kuhusu mtoto huyo mahali alipo.


KIKWETE AKUTANA NA VIONGOZI WA ALBINO
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa serikali inasikitishwa na kufedheheshwa sana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na itafanya kila linalowezekana kukomesha mauaji haya.

Alisema hayo jana Ikulu Dar es Salaam alipokutana na viongozi wa Chama Cha Watu Wenye Albino Tanzania, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Ernest Kimaya.

“Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana, msidhani hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali, lakini imefikia wakati tuongeze juhudi hizo,” alisema Kikwete.

Katika kikao hicho viongozi wa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini walisoma risala ambayo imetoa kilio chao na mapendekezo yao kwa serikali na hatimaye ikaafikiwa kuwa na haja ya kuunda kamati ya pamoja.

Kamati hiyo itajumuisha Serikali, viongozi wa watu wenye ulemavu wa ngozi, viongozi wa waganga wa jadi na wadau wote wakuu katika suala hilo, ili kupata mapendekezo na mkakati wa pamoja ambao hatimaye mauaji haya kukomeshwa kabisa nchini Tanzania.

Rais Kikwete alisema mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi hayafanywi na Serikali bali watu ambao wako katika jamii kwa kushirikiana na waganga wa jadi na watu wengine wenye tamaa mbalimbali katika jamii, hivyo ni lazima yakomeshwe.

“Kwenye familia, jamii na hatimaye vyombo vya ulinzi na usalama na hilo ndiyo jukumu kubwa ambalo Serikali inapaswa kulisimamia na tutalisimamia kwa ushirikiano wa pamoja,” alisema na kuongeza kuwa kamati hiyo ya pamoja itaweka mikakati ya kuwabaini wote wanaohusika kuanzia wakala, waganga na hatimaye wanaonufaika na viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Rais Kikwete pia alisema Serikali itasaidia familia na waathirika wa vitendo vya mauaji kwa hali na mali ili waweze kujimudu na pia kuwapa ushauri nasaha ili kuondokana na majonzi yanayosababishwa na vitendo hivyo.

Alisema vitendo hivyo vinawaletea waathirika na watu wanaoishi na albino mfadhaiko na msongo wa mawazo katika jamii na hivyo kushindwa kuendelea na maisha yao ama kufanya shughuli zao za kila siku.

Katika kikao cha jana, viongozi wametoa kilio chao kwa serikali kuziangalia na kuzimulika taasisi zisizo za kiserikali ambazo pamoja na kujipambanua kuwa zinatetea haki za watu wenye albino nchini bado hazina mkakati wa pamoja na hazipo wazi kwa walengwa hapa nchini.

Mara baada ya kufika Ikulu, kulitokea sintofahamu baina ya viongozi wa Chama cha Watu Wenye Albino na watu wasio wanachama kwa kile kilichoelezwa kuwa uongozi huo siyo halali kwa vile muda wake wa kukaa madarakani umeshakwisha.

Hata hivyo, Kimaya alielezea masikitiko kwake kwa Rais na kuelezea kuwa uchaguzi haukuweza kufanyika kutokana na ukosefu wa fedha na wamemuomba Rais awasaidie kutimiza azma yao ya kuitisha mkutano na kuchagua viongozi wa Chama chao.

Kulingana na Kimaya wamepanga kufanya mkutano huo wa kuchagua viongozi katikati ya mwaka huu wakati pia dunia itakua inaazimisha siku ya watu wenye albino duniani.

Rais alikubali ombi hilo na hiyo itazungumzwa kwa urefu katika kamati ya pamoja ambayo inatarajiwa kuwa imekamilika wiki ijayo.


CHANZO: NIPASHE

 
sheria ifuate mkondo wake anaye uwaa basi na yeye auwawe........hvy co km wanaonew
serikali ya tanzania ioneshe mfano kwa watuhumiwa haoo
...kam ilvy china ukikamatwa unanyongwa hilo ndi shuruhsho
....naninadhan ikiwepo sherua ya kunyongwa weng wataogopa na kuacha
kabisa kufanya ukatili huoooo
 
Back
Top Bottom