Wanawake mashujaa waliosahauliwa tunawakumbuka: makala maalum siku ya wanawake

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,264
AISHA ''DAISY'' SYKES ANAVYOWAKUMBUKA MAMA NA BIBI ZAKE WALIOSAHAULIWA NA HISTORIA

Utangulizi

Kila ninapofikiri kuhusu historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika hasa katika zile siku za mwanzo za TAA kabla ya kuundwa kwa TANU na baada ya TANU kuundwa mwaka wa 1954, nashawishika kufanya rejea katika makala aliyoandika Daisy Sykes katika miaka 50 ya kumbukumbu ya baba yake marehemu Abdul Sykes.

Makala hii ilichapwa katika gazeti la Raia Mwema na ilivutia wasomaji wengi sana kupita kiasi kwa sababu Daisy alifungua mlango wa nyumbani kwao kwa mara ya kwanza na kuonyesha maisha yalikuwaje kwao wakati harakati za TANU zinaanza hadi kufikia Mwalimu Nyerere kuacha kazi ya ualimu baada ya kurudi ktoka UNO na akaenda kuishi nyumbani kwao.

Huenda baadhi ya wasomaji wangu wakachoka kuwa kila mara inapokuja historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika nawarejesha katika rejea ile ile lakini ukweli ni kuwa ikiwa mtu anataka kuijua historia ya kweli hapana budi ila kuwasikiliza wale walioshuhudia historia hii ikifunguka mbele ya macho yao na Daisy ni mmoja wa hawa lau kama alikuwa mtoto mdogo.

Mwaka wa 1952 wakati Julius Nyerere anafika nyumbani kwao Daisy alikuwa binti mdogo mwenye utambuzi wa nini kilikuwa kinatokea.

Nyumba yao iliyokuwa Kariakoo, Mtaa wa Stanley na Sikukuu kwa wakati ule ndiyo ilikuwa moja ya vituo vya mikakati dhidi ya ukoloni wa Waangereza.

Nyumba hii kwa nyakati zile ilikuwa nyumba ya kifahari kwa viwango vyovyote vya nyumba za Waafrika Dar es Salaam.

Nakukaribisha msomaji wangu umsikilize Daisy akihadithia kuhusu wanawake aliowashuhudia katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Wanawake hawa historia imewasahau na hawafahamiki kabisa.

Karibu umsikilize Aisha ''Daisy'' Sykes:

''Mwalimu Nyerere na Hamza Mwapachu ni watu walionivutia sana mimi kwa kiwango cha juu kwa namna walivyokuwa wakilitamka jina langu, ‘’Daisy,’’ kwa lafidhi yenyewe ya Kiingereza kama wanavyozungumza Wazungu na hii ikalifanya jina hili langu la utani linigande na liwe ndilo jina langu halisi.

Nikiwa mtoto nakumbuka sana vipi baba akishughulishwa na kutaka kuona kuwa Mama Maria na watoto wake hawakosi chochote kuyafanya maisha yao kuwa mepesi, ya starehe na furaha akihakikisha chakula kinapelekwa dukani kwa Mama Maria kila siku katika duka lake dogo lilikuwapo Mtaa wa Livingstone kona na Mtaa wa Mchikichi, hiki kikiwa kielelezo chake kikubwa kabisa cha huruma na ukarimu wake.

Ilikuwa katika kipindi hiki cha mimi kuanza kupata akili katika kukua kwangu ndipo nilipokutana na wanawake wazalendo waliokuwa wanaochipukia katika uongozi wa Tanganyika, wanawake kama Bi. Lucy Lameck kutoka Moshi, Mary Ibrahim na akina mama wa Kiislam kama Bi. Titi Mohamed, Bi. Tatu bint Mzee, Bi. Hawa bint Maftah, hawa kutoka Dar es Salaam, wote hawa kwangu mimi walikuwa bibi zangu.

Kitu cha kufurahisha ni kuwa hawa akina mama wa Kiislam wote walivutwa katika siasa na Bibi Chiku bint Kisusa, maarufu akijulikana kama Mama Sakina.

Alikuwa Mama Sakina ndiye aliyewapa hawa wanawake niliowataja hapo juu utambulisho na wakaja kuwa watu maarufu.

Baba yeye ndiye alikuwa kiongozi wa mikakati hii yote kwa sababu bila yeye kuwatia hima kwa kutumia ushawishi wake ingekuwa vigumu kuweza kuwatia hawa wanawake katika kuwahamasisha wanawake wenzao wa na wao watoke majumbani kuja mstari wa mbele katika mikutano wakiimba na kutoa vibwagizo vya kuunga mkono TANU na kudai uhuru.

Hili jambo lilikuwa jipya, jambo ambalo katika utamaduni wetu kwa wakati ule halikutarajiwa na ni kinyume katika utamaduni wetu kwa wanawake wa Kiislam kulifanya katika siku zile.

Nimesikia mazungumzo mengi wakati baba na wenzake walipokuwa wakijadili majina na shughuli ambazo hawa akina mama walikuwa wahusishwe ili kuleta mvuto wa kisiasa katika mikutano yao ya TANU.

Nakumbuka vizuri sana jinsi baba alivyokuwa karibu sana na Mwalimu Sakina na ndugu yake Mwalimu Fatna (wote hawa watoto wa Mama Sakina), na jinsi alivyowaleta ndugu hawa karibu na Mama Maria na hawa wakamjulisha Mama Maria Nyerere kwa mama yao na mashoga zake Bi Hawa Maftaha, Bibi Titi Mohamed na Bi Tatu binti Mzee.

Hawa wanawake ndiyo waliomsaidia Mama Maria kufungua hilo duka lake dogo pale Mtaa wa Livingstone kona na Mchikichi, mahali ambako Mama Maria alishinda kutwa nzima akiuza duka lake.

Nikiwa mtoto nakumbuka kwenda kwenye dula lile kila siku mchana kupeleka chakula kwa Mama Maria, ambako hapakuwa mbali kutoka nyumbani kwetu.

Kwa kuwa baba alikuwa anataka ratiba hii yake ya chakula ifuatwe sawasawa kwa wakati wake, wakati mwingine hii ilikuwa changamoto kubwa sana kwa mama yetu, Bi. Mwamvua bint Mashu.''

Msomaji wangu hiki ni kipande kidogo kutoka kumbukumbu za bint mdogo Aisha Daisy wakati ule akiwa na umri wa miaka mitano au sita hivi.

Lakini wakati haya yakifanyika Dar es Salaam huko katika majimbo TANU ilipoasisiwa walijitokeza akina mama na kuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Hapa Dar es Salaam kulikuwa na tawi lililoasisiwa Magomeni Mapipa, Mtaa wa Jaribu na Ali Msham nyumbani kwake na Mama Maria alihamishia duka lake la mafuta ya taa hapo.

Wanawake wengi wa Magomeni waliliunga mkono tawi hili na ndiyo tawi pekee ambalo historia yake imehifadhiwa katika picha.

Wanawake hawa hakuna anaewafahamu.

Historia imewasahau.
Hebu tuangalie majimboni yaani katika ''provinces.''

Hakuna anejua historia ya Bi. Chande bint Nyange wa Tabora aliyejitolea nyumba yake kuwa ofisi ya TANU.

Historia ya mama huyu nimeiandika miaka mingi ipo ndani ya kitabu cha Abdul Sykes (1998) lakini hakuna aliyejali.

Picha ya Bi. Nyange bint Chande, mwanamke wa Kiganda nimeipata miezi michache iliyopita kutoka kwa mwanae baada ya yeye kuisoma mitandaoni.

Pamoja na Bi. Nyange alikuwapo Bi. Zarula bint Abdulrahman.

Bi. Zarula yeye ndiye alikuwa muuzaji wa kadi za TANU na aliingiza wanachama wengi katika chama.

Hii haikuwa kazi nyepesi kwani watu kama hawa walikuwa wanasakwa mchana na usiku na Special Branch.

Nani aliyepata kumsikia Bi. Shariffa bint Mzee mwanamama shupavu wa TANU Lindi, Southern Province?

Katika matawi yote ya TANU Tanganyika hakuna tawi lililokuwa na nguvu kubwa ya wanawake ukitoa matawi ya Dar es Salaam kama tawi la Moshi Mjini lililoshikwa na akina mama hawa: Mama bint Mwalimu, Halima Selengia na Amina Kinabo.

Picha za kina mama hawa nimezipata siku hizi za karibuni kutoka kwa wajukuu zao baada ya wao kusoma historia zao kisha kuniandikia na mimi nikawaomba picha.

Hakuna aliyekuwa anawajua wanawake hawa mashujaa wa uhuru wa Tanganyika.

Wanawake hawa wamesahauliwa na wanahistoria hata historia zao zilipoandikwa hakuna aliyetaka kuwajua.

Sisi hatuwezi kuwa wezi wa fadhila.

Tunawakumbuka mashujaa wetu hawa katika Siku ya Wanawake Duniani.

PICHA:
1. Bi. Nyange bint Chande
2. Bi. Zarula bint Abdulrahman
3. Bi. Shariffa bint Mzee
4. Bi. Halima Selengia, Bi. Amina Kinabo na Bi. Lucy Lameck
5. Bi. Mwamvua bint Mashu (Mama Daisy), Bi. Titi Mohamed na Bi. Zainab Tewa
6. Aisha ''Daisy'' Sykes

Screenshot_20220307-144752_Facebook.jpg
 
AISHA ''DAISY'' SYKES ANAVYOWAKUMBUKA MAMA NA BIBI ZAKE WALIOSAHAULIWA NA HISTORIA

Utangulizi

Kila ninapofikiri kuhusu historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika hasa katika zile siku za mwanzo za TAA kabla ya kuundwa kwa TANU na baada ya TANU kuundwa mwaka wa 1954...
aisha sykes ndo yupi?
 
aisha sykes ndo yupi?
Mwana...
Mtoto wa kwanza wa Abdul Sykes.
Mwafrika wa kwanza kusoma Aga Khan School na msichana wa pili kusoma University of East Africa, Dar-es-Salaam Campus.

Msichana wa kwanza alikuwa marehemu Tatu Nuru.

Ndiye aliyeandika maisha ya babu yake, "Kleist Sykes The Townsman," (1894 - 1949).

Hii ni sura katika kitabu alichohariri John Iliffe, "Modern Tanzanians," (1973).

Screenshot_20220307-194343_Facebook.jpg
 
Mwana...
Mtoto wa kwanza wa Abdul Sykes.
Mwafrika wa kwanza kusoma Aga Khan School na msichana wa pili kusoma University of East Africa, Dar-es-Salaam Campus...
Asante mzee wangu,

nilikua namuulizia ndo yupi hapo ktk hizo picha ulizotuma?
 
Mwana...
Mtoto wa kwanza wa Abdul Sykes.
Mwafrika wa kwanza kusoma Aga Khan School na msichana wa pili kusoma University of East Africa, Dar-es-Salaam Campus.

Msichana wa kwanza alikuwa marehemu Tatu Nuru.

Ndiye aliyeandika maisha ya babu yake, "Kleist Sykes The Townsman," (1894 - 1949).

Hii ni sura katika kitabu alichohariri John Iliffe, "Modern Tanzanians," (1973).

View attachment 2142394
Sura ya Dully Sykes wa Bongofleva hiyo kabisa!
 
Back
Top Bottom