Vigogo wawindana serikalini
Mzozo wa Mengi, Masha
na Charles Mullinda
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
KUVUJA kwa mikakati ya siri serikalini kumetajwa kuwa chanzo kikuu cha mzozo unaoendelea hivi sasa kati ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha na mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi, Tanzania Daima Jumatano imedokezwa.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka vyanzo vya kuaminika zinaeleza kwamba, kauli aliyoitoa Mengi wiki iliyopita imesababisha baadhi ya maofisa wa juu serikalini kuanza kuchukua hatua za kuwasaka viongozi, wakiwamo mawaziri ambao wamekuwa wakivujisha taarifa mbalimbali ya kimaamuzi ndani ya serikali.
Chanzo kimoja cha habari kimeieleza Tanzania Daima Jumatano kwamba, hatua ya Waziri Masha kumpa Mengi siku saba zinazoisha kesho, akimtaka athibitishe madai yake kwamba kuna waziri kijana anayeongoza wizara nyeti, anayeshawishi serikali kumhujumu kibiashara, inalenga kumlazimisha mfanyabiashara huyo amtaje mtu aliyemweleza taarifa hizo ambazo kimsingi zilijadiliwa katika vikao viwili vikubwa vya ngazi ya kitaifa.
Hatua ya Masha kumuandikia Mengi barua ya kumtaka awasilishe ushahidi wa madai yake hayo, inaonekana kuwashtua baadhi ya wanasiasa ambao wameitafsiri hatua hiyo kuwa inayoweza kuwa na madhara makubwa kisiasa katika siku za usoni.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano unaonyesha kwamba, mshtuko huo ndio ambao katika siku za hivi karibuni umesababisha kuibuka kwa wanasiasa kadhaa wazito ambao ama wamejitokeza kumpinga Masha hadharani huku wengine wakitahadharisha na kutaka kusitishwa kwa malumbano haya.
Wanasiasa kadhaa wa CCM na wale wa upinzani waliozungumza na gazeti hili wanasema, lengo moja la mzozo huu wa sasa ni hatua ya baadhi ya viongozi serikalini kujaribu kumdhibiti Mengi ambaye katika miaka ya hivi karibuni vyombo vyake vya habari vimeonekana kuwa mstari wa mbele katika kuhujumu kile wanachokielezea kuwa masilahi yao na ya taifa.
Wakubwa kadhaa serikalini kwa kauli moja wamefikia hatua ya kuanza kumuona Mengi kuwa ni tatizo. Huyu jamaa haeleweki ana malengo gani kisiasa, kwani amekuwa nyuma ya kila jambo kubwa hapa nchini. Ameshiriki kutukifisha mahali pagumu sana, hata kusababisha serikali ishindwe kufanya kazi yake sawasawa, kwa kweli ni lazima ashughulikiwe ipasavyo, alisema mbunge mmoja wa CCM anayeunga mkono hatua ya Masha kumpa Mengi siku saba.
Ofisa mmoja wa juu serikalini aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina gazetini alisema, pendekezo la kutaka serikali ichukue hatua ya kumbana Mengi lilitolewa kwanza katika kikao kimoja cha juu cha kiserikali kinachoshughulikia masuala ya usalama nchini kabla ya jambo hilo hilo kujadiliwa tena katika Baraza la Kazi linalojumuisha mawaziri kadhaa.
Kilichoishtua serikali ni kumsikia Mengi akizungumza kuhusu mambo yaliyojadiliwa katika kikao kimoja nyeti cha kitaifa kinachohusisha watu wazito. Sasa jamaa walichofanya wanataka kumlazimisha Mengi amtaje mtu aliyempa taarifa hizo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake, kilisema chanzo kimoja cha habari.
Chanzo kingine cha habari kilichozungumza na Tanzania Daima Jumatano kinaeleza kwamba, tayari maofisa wa serikali wanaofuatilia nyendo za baadhi ya mawaziri wameshaanza kumtaja waziri mmoja anayeongoza wizara nyeti kuwa mtu ambaye alimpelekea Mengi taarifa za kuwapo kwa mjadala huo, ambao hata hivyo bado haujachukuliwa kuwa msimamo rasmi wa serikali.
Hata hivyo, katika hatua ambayo inaweza kumnusuru waziri huyo, habari hizo zinaeleza kwamba, siku na wakati vikao hivyo vikikaa, waziri huyo anayetafutwa hakuwa miongoni mwa wajumbe waliohudhuria kikao kimojawapo ambacho baadhi ya washiriki wake ni wakuu wa taasisi nyeti za dola.
Hata hivyo katika hatua nyingine, kuibuka kwa mzozo huo kumesababisha kuibuka kwa nadharia mbalimbali kuhusu utendaji na uwajibikaji wa viongozi serikalini.
Kundi moja la wadadisi wa mambo, wanakielezea kitendo cha waziri kupendekeza mfanyabiashara kuhujumiwa kuwa ni hatua ya kihalifu ambayo haipaswi kuungwa mkono kwa namna yoyote na serikali ambayo imeruhusu kisheria ushindani wa kibiashara katika misingi ya haki.
Miongoni mwa watu wenye mtazamo wa namna hii ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ambaye anasema, ni jambo la fedheha kwa kiongozi wa dola kufikia hatua ya kufikiria kumhujumu mfanyabiashara mzalendo kwa kutumia njia za kihalifu.
Hata hivyo kundi jingine la wadadisi wa mambo, pasipo kuangalia uhalali au uharamu wa hatua hii ya kumdhibiti Mengi, wanaeleza kushangazwa na hatua ya maamuzi na mijadala nyeti serikalini kuvuja.
Mmoja wa wahadhiri waandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyezungumza na gazeti hili, alisema kuwa, kufanikiwa kwa Mengi kunasa siri za kikao nyeti serikalini, kunaashiria kuwapo kwa mgawanyiko mkubwa kati ya viongozi waandamizi.
Mengi si mjumbe wa vikao nyeti serikalini, hivyo kuibuka kwake na kueleza kuwa amenasa taarifa kutoka ndani ya vikao vya juu vya viongozi waandamizi, kuna maana kwamba, yupo kiongozi ambaye ni mjumbe wa kikao hicho aliyemfikishia kile kilichojadiliwa ndani ya kikao hicho au mjumbe huyo alikifikisha kwa rafiki wa karibu na Mengi, hivyo kuwa rahisi kumfikia.
Na hii maana yake ni kwamba, serikali haiko salama, maana nyingine ni kumfikishia ujumbe Rais Kikwete kuwa anaoshirikiana nao kuongoza wanamzunguka au wanazungukana. Lakini ujumbe muhimu kwa rais ambao mimi naona Mengi ameamua kumtumia ni kwamba baadhi ya wasaidizi wake hawafai kuwa viongozi, hawajui nini maana ya siri za serikali, alisema msomi huyo.
Mwingine mwenye mtazamo huo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alieleza kuwa Waziri Masha hapaswi kumtisha Mengi kwa kumpa siku saba ili kutoa ushahidi wa madai yake, kwa sababu hata yeye (Zitto) amepata kuzisikia taarifa hizo.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alikaririwa hivi karibuni akieleza kuwa ana taarifa kuwa waziri mmoja ndiye aliyepeleka hoja ya kutaka serikali itumie vyombo vyake kumhujumu Mengi kwa kumbambikia kodi kubwa katika biashara zake.
Habari za hivi karibuni zilizoifikia Tanzania Daima Jumatano na kuthibitishwa na baadhi ya wanasiasa walio karibu na Zitto zinaeleza kuwa, Waziri Masha alishtushwa na kauli hiyo ya Zitto hata akafikia hatua ya kumtumia ujumbe mfupi kupitia simu yake ya kiganjani akimtaka kutojiingiza katika sakata hilo.
Taarifa ambazo zimethibitishwa na Zitto mwenyewe zinaeleza kwamba, Masha alimweleza bayana kwamba, jitihada zake za kujaribu kununua kesi yake na Mengi haziwezi kumfanya amuuzie yeye.
Mengi katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, mbali ya kumzungumzia waziri huyo, alisema kuwa alitumiwa ujumbe wa vitisho vya kuuawa kwa sumu.
Sehemu ya maandishi yaliyo katika ujumbe wa maandishi wa simu uliotumwa kutoka simu namba 0768-373967, ulisomeka hivi: Ni afadhali kunyofoa roho yako upotee kuliko kukuachia uchafue amani na utulivu kwa tamaa zako za kutaka kuwa rais... unachafua sana amani ya nchi kwa uchochezi wako. Tunajua unawahonga wahariri wote na kukusujudia kama Mungu mtu. Unapenyeza sumu kali ya uzandiki watu waichukue serikali. Hivi yakitokea machafuko wewe utasalimika? Wewe ni mnafiki mkubwa, unajifanya upo karibu na Government kumbe ni mnafiki wa kutisha. Jihadhari lazima tukuue!
Siku chache baada ya Mengi kutoa madai hayo, Waziri Masha alitoa kauli ya kumtaka athibitishe madai ya kuwapo kwa waziri kijana anayefanya njama za kutaka kummaliza kibiashara.