Wakati mwingine huwa sio busara kukaa kimya hasa kwa jambo linalokushutumu

BAKIIF Islamic

JF-Expert Member
Jul 11, 2021
594
1,827
Kuna wakati mtu anaweza kukutendea ubaya na ukajikuta umejibu mapigo kwa kugomba na kuropoka maneno mengi makali, kwa wakati huo unaweza usitambue na nafsi yako kuridhika kwa maneno hayo, lakini baadae maneno hayo yakawa mabaya na kukuharibu kiasi cha kujutia.

Ila Kama unadhani ukikaa kimya itakuwa ni njia sahihi, basi ukimya huo huwa una nguvu Sana katika jambo husika au katika shutuma husika.

Chunga kinywa, shusha presha, Kisha kwa umakini Sana, tafuta namna ya kujibu na kutatua jambo lililo mbele yako.

Hakikisha unakuwa na mikakati na njia sahihi za kukabiliana na changamoto yoyote iliyo mbele yako badala ya kutanguliza hisia na jazba.

Kuwa kimya haimaanishi kuwa ni dhaifu.

Mbegu hupandwa na kukua bila kelele, ila pindi mti unapoanguka hutoa kelele na kishindo kikubwa.
Siku zote ujenzi na utengenezaji huwa kimya, ila uharibifu huwa na kelele.

Watu wengi hupenda kujitetea katika kila shutuma inayowakumba, lakini wanasahau kwamba nguvu kubwa ya kuzishinda tuhuma ni kukaa kimya.

Mtu mkimya huonekana mwenye nguvu zaidi. Mtu mwenye nguvu zaidi huogofya na kutisha zaidi kwa kuzungumza maneno machache sana yenye umuhimu kwa jambo husika.

Lolote utakalolisema litakuwa na maana na litabeba uzito zaidi pindi unapolisema ikiwa kwa kawaida wewe ni mtu mkimya na jamii inakufahamu na kukuchukulia kuwa wewe ni mtu mkimya usiye na maneno mengi.

Wakati wote watu watakuona ni mtu usiyetabirika na kuwawia ugumu kukufahamu wewe ni mtu wa namna gani, jambo ambalo litawafanya Mara zote wawe makini na tulivu pindi wanapotaka kuzungumza ama kufanya jambo lolote mbele yako.

Kwa kawaida mtu mkimya huwa na tabia ya kusikiliza na kutazama wengine zaidi, jambo ambalo humsaidia kujifunza Mambo mengi na kuwasoma wengine zaidi, kwa hiyo unaweza kuutambua uongo na taarifa/mambo yasiyokuwa sahihi, unaweza kufahamu ni kwa kiasi gani watu wanaujua ukweli kuhusu jambo fulani.

Uwezo wa kumsoma na kumwelewa mtu ni maarifa yenye nguvu unayoweza kujifunza tuu kwa kujenga tabia ya kuwa mkimya kwa kusikiliza na kutazama zaidi kile kinachosemwa na watu wenye tabia ya kuwa wazungumzaji Sana.

Neno likishatoka kinywani, huwezi kulirudisha. Hupaswi kuzungumza neno/jambo ambalo baadae utalijutia, kuwa kimya (ukimya) ni mbinu na njia kubwa ya kukufanya uwe makini kwa kila unachotaka kukizungumza.

Unapokuwa mtu mtulivu na mkimya ukajenga tabia ya kuwa msikilizaji Sana badala ya kuwa muongeaji Sana, watu watavutiwa na kupenda kuzungumza nawe, kwani unapokuwa unamsikiliza Sana mtu kwa umakini akizungumza unamfanya ajione huru na kumjengea ujasiri wa kuzungumza nawe, kwani watu hupenda kusikilizwa na kueleweka kwa kile wanachokizungumza.

Kama ukiwa kimya na mtulivu kwa kuzungumza kidogo na kusikiliza zaidi, utaonekana kuwa ni mtu mwenye mvuto mbele ya watu wanaokuzunguka katika kila mjadala/mazungumzo.

Katika kutafuta makubaliano/suluhisho kwa jambo lolote, kila upande hutaka kushinda na kupata faida kutoka upande mwingine.

Namna mlolongo unavyozidi, hujenga kiasi cha hofu na aibu kwa pande zote zinazovutana, Kama utakuwa huru na jasiri kwa kujenga ukimya, utakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda na kupata faida zaidi katika hitimisho la suluhisho na makubaliano hayo.

Kama utaishia kuwa muongeaji sana kiholela bila umakini, unaweza kuwaaminisha wengine wakuone kuwa huenda wewe ni mwendawazimu usiekuwa na akili, na hivyo kuwafanya na ama kuwapa nafasi kubwa ya kukushinda na kunufaika zaidi katika hitimisho la makubaliano juu ya mvutano mlionao.

1705086575439.png
 
Back
Top Bottom