Wahadhiri wamtilia ngumu Warioba, wasisitiza kugomaTuesday, 27 April 2010 21:14
WAHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana walimshambulia mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Jaji Joseph Warioba alipotaka kuwatuliza ili wasisitishe mgomo walioupanga.
Wahadhiri hao, wakionekana kuwa na jazba, walikataa ushauri wa Jaji Warioba na kusema kuwa maneno yake ni mepesi na hayana uzito wowote.
Wahadhiri hao wameamua kugoma baada ya kuona serikali imeshindwa kushughulikia madai yao ya kutaka kuboreshwa kwa mafao ya wastaafu ambayo yanatolewa na Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF) na ule wa wafanyakazi waandamizi (Senior Staff Superannuation Scheme, SSS).
Pia wanataka menejimenti za vyuo vikuu ziwaruhusu waajiriwa wapya kujiunga na mifuko mingine ya pensheni wanayoitaka kama LAPF.
Jana Jaji Warioba alikwenda kwenye mkutano wa wahadhiri hao wa vyuo vikuu ulioitishwa kwenye ukumbi wa Cafeteria 1 ulio UDSM ili kutoa taarifa ya kura za maoni kuhusu mpango wa mgomo huo na akatumia fursa aliyepewa kuwashauri wasomi hao wasitishe kutekeleza azma yao ya kugoma na kuwaelezea athari zake.
Tunakubali kuwa suala hili limechukua muda mrefu kushughulikiwa, lakini kwa jinsi katibu mkuu kiongozi alivyolishughulikia katika miezi minne na nusu tu hadi kufikia kupeleka waraka kwa Baraza la Mawaziri, tunaamini halitachukua muda mrefu tena kuamuliwa, alisema Warioba.
Wanataaluma wanatakiwa kuwa na subira; kama mmeweza kusubiri kwa miaka takribani kumi, msikate tamaa bali mvute subira kwa miezi miwili, mitatu ijayo ili serikali ikamilishe azma yake.
Baada ya Jaji Warioba kutoa maoni yake kuhusu mgomo huo aliomba kuondoka bila kusikiliza maoni ya wahadhiri hao huku mwenyekiti wa Chama cha Wahadhiri wa UDSM (Udasa) akimuomba asikilize maoni ya wajumbe.
Lakini Warioba hakutaka kuendelea na kikao hicho na badala yake akaomba ashirikishwe kwa kupewa taarifa za kikao iwapo watapanga kukutana.
Baada ya Jaji Warioba kuondoka kwenye ukumbi huo, wahadhiri hao waliendelea na kikao ndipo mwenyekiti wa Udasa, Dk Damas Nyaoro alipotoa fursa kwa wajumbe kuchangia ushauri wa waziri mkuu huyo wa zamani.
Maneno ya Warioba yote ni mepesi, hayana uzito wowote. Kama wameshindwa kutoa suluhisho la tatizo ndani ya miaka kumi itakuwaje katika miezi miwili? Sisi si watoto wadogo, alisema mmoja wa wahadhiri.
Alisema wamesikitishwa na kitendo cha Warioba kuondoka kabla ya kusikiliza maoni yao kwa sababu walihitaji awepo apo ili wampe maneno yao.
Ningefurahi sana kama Jaji Warioba angekuwepo hapa ili asikilize maoni, ila naomba mfikishie sisi tutagoma kama tulivyopanga hii ni kutokana na makubaliano ya vyuo vyote, alisisitiza mmoja wa wahadhiri hao.
Wahadhiri hao walisema suala lao lisiwekwe kisiasa bali wanachohitaji ni utekelezaji na siyo ahadi hewa.
Serikali imechelewa sana, pia haina nia njema na wanataaluma na anayetaka kuahirisha mgomo, aahirishe kichwani mwake na si kuwashauri wajumbe, alisema mhadhiri mwingine.
Akitoa taarifa za mpango wa mgomo huo, Dk Nyaoro alisema wahadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce) wameazimia kugoma kwa asilimia 100, Chuo Kikuu Cha Dodoma (Udomasa, 98%) na Udasa asilimia 95.
Alitaja vyuo vingine kuwa ni Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) 95%, Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa (Mkwawa) 92%, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (Mucobs) 89%, Chuo Kikuu cha Ardhi (Arisa) 85% na Chuo Kikuu cha Mzumbe 75%.
Alisema kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Out) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) havikuweza kuwasilisha mapendekezo kuhusu mgomo huo.
Dk Nyaoro alisema mgomo huo, ambao ulianza rasmi jana, unashinikiza madai mbalimbali ya wahadhiri baada ya kuchoshwa na ahadi hewa zinazotolewa na serikali kuhusu malipo hayo.
Aprili 9 mwaka huu tulikutana baadhi ya wanataaluma wa vyuo mbalimbali vya umma na katika mkutano huo tulifikia uamuzi wa kufanya mgomo, lakini kwa kuzingatia kutokuwepo kwa baadhi ya wahadhiri tuliamua viongozi wao wapeleke uamuzi huo ili waweze kushirikishwa, alisema Dk.Nyaoro.
Alifafanua kuwa mgomo huo utakuwa wa kusitisha kufundisha pekee lakini kazi nyingine za kiofisi zitaendelea kama kawaida.