Wabunge CHADEMA wamshtaki Zitto
*Waitaka Kamati Kuu imuhoji kwa kukiuka maamuzi
*Wamo pia wengine 9 waliokacha ufunguzi bunge
Na Edmund Mihale
WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameiandikia barua Kamati Kuu ya chama hicho kuiomba imuite Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe na wabunge wengine tisa ili wajieleze kwa nini walikiuka maamuzi halali ya
vikao.
Hatua hiyo imetokana na kitendo cha Bw. Kabwe na wenzake kutoingia bungeni Novemba 18, mwaka huu ambapo wabunge hao walikuwa wameafikiana kwa kura, kuwa watoke nje ya ukumbi wa bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akizindua bunge.Pamoja na makubaliano hayo, Bw. Zitto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni na wabunge hao hawakuingia bungeni.
Wengine ambao hawakuonekana siku hiyo ni Bw. Said Arfi (Mpanda Mjini) ambaye ni Makamu Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Mhonga Luhwanya (Viti Maalum), Bw. John Shibuda (Maswa Magharibi), Bi. Maulida Komu (Viti Maalum), Profesa Kulikoyele Kahingi,(Bukombe), Bi. Rachel Mashishanga (Viti Maalum), Bi. Raya Ibrahimu (Viti Maalum), Bi. Lucy Owenya (Viti Maalum) na Bi. Suzan Lyimo(Viti Maalum).
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, Mnadhimu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani bungeni, Bw Tundu Lisu alisema kuwa Bw. Zitto amendikiwa barua mbili tofauti na wabunge wengine kutokana na kitendo hicho.
"Zitto kama Zitto ameandikiwa barua mbili, moja ikiwa ya kitendo cha kushindwa kuingia bungeni jambo ambalo tuliamua katika kikao ambacho hata yeye alikuwepo."Barua hiyo iko tayari lakini ninachojua kuwa yuko Ughaibuni na sijui kama amerudi kwa kuwa alinitumia ujumbe mfupi wa simu kuwa anakwenda Malaysia lakini hajaniambia kuwa amerudi. Kusema kuwa yuko hapa nchini ndiyo sasa unaniambia," alisema Bw. Lissu.
Alisema kuwa barua ya pili imeandikwa kwenda Kamati Kuu na wataitwa na kutoa maelezo mbele ya kamati hiyo. "Kwa kanuni za Katiba ya CHADEMA, Kamati Kuu ndiyo yenye uamuzi wa mwisho ama kumpuuza kama itaona jambo hilo halina uzito, au kama lina uzito itaunda tume kuchunguza tuhuma hizo na iwapo itabainika itachukua hatua," alisema Bw. Lissu.
Alisema kosa lingine la Bw. Zitto ni kitendo cha kuwapigia simu baadhi ya wabunge kuwataka kutoka nje ya kikao kilichoitishwa na chama hicho baada ya kutoka bungeni, akiwataka kutoka katika kikao hicho na kumfuata aliko, jambo lililokera wabunge hao, hivyo kutoa taarifa katika kikao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw Zitto alisema hadi sasa hajapata barua yoyote, na kuwa hizo ni habari za mitaani kwa kuwa hakukuwa na kikao chochote klichoketi ili kujadili suala hilo.
Alisema yeye ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Naibu Katibu Mkuu na pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, hivyo alipaswa kujua hayo yote."Hizi ni habari za mitaani, mimi sijapata barua yoyotem niliyoandikiwa na CHADEMA," alisema Bw. Zitto.