Kwa hakika ni kwamba serikali inapigana kwa namna yeyote ile kuhakikisha kua huu mswaada wa huduma za vyombo vya habari unaopigiwa kelele kila Kona ya nchi unapitishwa bungeni.
Kuna tetesi kua wabunge wa CCM wameshajipanga kutekeleza hilo kutokana na wingi wao, huu ni mswaada kandamizi ambapo vyombo vingi vya habari hapo baadae vitanyamazishwa kimya.
Sasa kweli wanahabari hiki kitu hatari kwa uhai kwenu kikipita basi mtaonesha udhaifu mkubwa sana, itaonesha kua hamjali maslahi yenu na utakua ni usaliti mkubwa sana kati yenu.
Ninyi ndio sauti ya wananchi, kupitia kalamu zenu mnao uwezo mkubwa wa kukikataa kitu.
Na Mdau Mkereketwa.
Dar es Salaam.
Tangu Serikali iweke hadharani muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 mwezi Septemba mwaka huu, kumezuka mijadala mbalimbali ya baadhi ya wadau huku wengine wakiunga mkono na wengine wakiupinga.
Baadhi ya wadau hao wamekuwa wakitoa hoja mbalimbali za kupinga muswada huo ikiwemo madai ya kukosa muda wa kutosha kwa ajili ya kusoma na kuchambua vipengele vilivyomo kwenye sheria hiyo.
Jambo la kushangaza ni kuwa walikuwa wapi katika kipindi cha zaidi ya siku 30 za kusoma muswada wenye kurasa zisizozidi 29 na kutoa maoni yao.
Jumla ya vyama 16 vya kitaaluma vilihusishwa katika kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu muswada huo lakini vyama hivyo vimekuwa vikidai kukosa muda wa kusoma, kujadili na kuwasilisha maoni na mapendekezo yao.
Miongoni mwa vyama hivyo vilivyoshindwa kutoa maoni ni pamoja na vyama vya wanasheria ambao baadhi yao wamebobea kwenye masuala ya sheria lakini walishindwa kusoma na kutoa maoni.
Vyama hivyo ni pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Taasisi ya twaweza, Taasisi ya Sikika, kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) na wengineo.
Madai mengine ya wadau ni pamoja na mamlaka ya Waziri wa mwenye dhama yalivyoanishwa katika ibara ya 55 ya muswada huo, ambaye kwa mujibu wa maelezo yao amepewa mamlaka makubwa ya kuzuia uchapishaji au utangazaji wa maudhui yanayohatarisha usalama wa Taifa au afya ya jamii.
Swali ni Je, wanaotoa madai hayo wanataka vyombo vya habari vijiendeshe vyenyewe kiholela bila ya kuwa na sheria ya kuvidhibiti na kama ni hivyo wanataka sheria hizo zisimamiwe na nani iwapo Waziri mwenye dhamana ya habari na wajibu wa kulinda maslahi ya umma atakuwa hana mamlaka hayo?.
Hofu yao kubwa ni waziri kuegemea upande wa Serikali lakini wanakwepa kusema ukweli kuwa sheria hiyo pia imeweka vipengele vya kuanzisha Baraza Huru la Habari lenye mamlaka ya kushughulikia malalamiko dhidi ya machapisho.
Aidha kipengele hicho pia kimempa nafasi mtu asiyeridhika na uamuzi wa Baraza kukata rufaa Mahakama Kuu.
Katika Baraza hilo litakalokuwa likiongozwa na wajumbe saba wakiwemo wajumbe wanne ambao watapendekezwa kutoka katika taasisi za tasnia ya habari nchini.
Pia muswada umependekeza kuanzishwa kwa mfuko wa wanahabari utakaotoa fursa ya kujiendeleza kielimu kwa waandishi ili kuwaongezea weledi kuhusu tasnia husika pamoja na kipengele cha utoaji wa bima ya afya na hifadhi ya jamii kwa waandishi wa habari.
Iwapo tuna dhamira ya dhati ya kupandisha hadhi na kuipa heshima tasnia ya habari nchini kama ambavyo wadau wa habari wamekuwa wakiipigania kwa takribani miaka 20 sasa, hatuna budi kuunga mkono muswada wa huduma za habari wa mwaka 2016 ambao tayari umewasilishwa Bungeni kwa ajili ya kusoma, kujadiliwa na kupitishwa.