Virusi vya Corona viwe somo kwa aina mpya ya virusi vya homa ya mafua ya nguruwe viliyogunduliwa China

Yoyo Zhou

Member
Jun 16, 2020
72
111
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu watu wengi wamekuwa wakiongelea janga la virusi vya corona ambalo limetikisa dunia nzima. Watu wote wameguswa na ugonjwa huu wa COVID-19 kwa namna moja ama nyingine, mana kama si ndugu yako kuugua ugonjwa huu basi ni rafiki au jirani yako. Lakini nchi na mtu mmoja mmoja wamekabiliana na kuendelea kufanya juhudi ili kuushinda ugonjwa huu, hata kama baadhi ya nchi hali bado ni mbaya, lakini nyingi zimeonesha matumaini.

Tunafahamu kuwa Corona bado haijaisha na kwa mujibu wa wataalamu itaendelea kuwepo kwa muda mrefu, lakini leo sitaki kuongelea sana kuhusu virusi hivi. Ninachotaka kuzungumzia zaidi leo hii ni aina mpya ya virusi vya homa ya mafua ya nguruwe vyenye uwezo wa kuwaambukiza binadamu. Mlipuko huu kwa sasa unaonekana kuwa tishio, kwani kawaida katika miaka ya nyuma ilizoeleka kwamba mafua ya nguruwe yanabaki kwa nguruwe tu. Lakini cha kushangaza na kushtua ni kwamba katika miaka ya hivi karibuni vimefika hadi kwa binadamu na watafiti wa China wamegundua hata virusi hivi vipya pia vina uwezo wa kuleta maambukizi makubwa kwa binadamu.

Tayari watafiti wameshakuwa na wasiwasi kuwa hali hii inaweza kubadilika na kusambaa kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Virusi hivi ambavyo vinaonekana ni tishio kwa watu vinajulikana kwa jina la G4 na vina uwezo mkubwa wa kuambukiza, pia vinaweza kukua na kuongezeka ndani ya seli za binadamu. Katika majaribio yao watafiti hawa wamethibitisha kuwa hivi sasa sisi bindamu bado hatujawa na kingamaradhi dhidi ya virusi hivi.

Ingawa inaonekana kwamba tatizo hili halijatokea kwa kasi kubwa, kama lilivyotokea lile la virusi vya corona, lakini bado tunarudi palepale kwamba virusi hivi ni hatari na pia vinaweza kumwambukiza binadamu. Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kufuatilia kwa karibu sana virusi hivi.

Waathirika wa kwanza inaonekana ni wafugaji, hasa wafugaji wa nguruwe. Kwa mujibu wa watafiti baada ya wafugaji kupimwa kingamaradhi ndani ya damu, ilibainika kuwa asilimia 10.4 ya wafugaji hao wa nguruwe wameambukizwa, huku asilimia 4.4 ya watu wote wakiweza kukabiliana na virusi hivyo. Kwa hiyo hali hii si ya kuifanyia mzaha ni lazima kuwepo na ufuatiliaji wa kina tena si kwa wafugaji wa nguruwe tu, bali hata kwa wafanyakazi wa viwanda vya nguruwe.

Nakumbuka mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka 2009 kule nchini Mexico vililibainika virusi vya mafua ya nguruwe ambavyo viliitwa H1NI, ambavyo vinafanana kiasi na aina hii mpya ya virusi vya homa ya mafua ya nguruwe vilivyobainika hapa China, lakini kwa kiasi fulani vinatofautiana na virusi vipya vya hapa China. Virusi hivyo viliangamiza watu wengi nchini humo na hadi leo kubaki kwenye kumbukumbu za watu. Cha hatari zaidi ni kwamba havikuishia hapo Mexico tu bali vilifika hadi kwenye nchi za bara la Afrika, Afrika Kusini ikiwa mhanga mkubwa. Wahenga wanasema jitihada huzaa matunda, baada ya mahangaiko na juhudi kubwa za wataalamu wa afya, ikapokewa habari ya kutia moyo ya kupatikana kwa chanjo ya virusi hivyo ambayo inawapa watu uhakika wa kuwa na ulinzi kamili.

Tukirudi nyuma katika mwaka 2016 na 2017 India nayo pia ilipata pigo kubwa sana baada ya kuripoti vifo vingi nchini humo kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe. Hivyo virusi hivi ingawa ni vipya lakini sio vigeni.

Kwa upande wa wataalamu wa Afya na mamlaka husika cha kuangalia hivi sasa ni hatua gani zinachukuliwa haraka ili kuhakikisha aina hii mpya ya virusi inadhibitiwa na kuepusha kuwa janga la dunia. Wahenga wanasema “usipoziba ufa utaziba ukuta” hivyo naamini hali hii itadhibitiwa haraka ili kuepusha kuenea zaidi, kwani tayari tumeshapata somo kubwa kutokana na janga la virusi vya Corona.
 
Back
Top Bottom