Waheshimiwa,
Mimi naamini hatuwezi kuondoa wizi wa kura, lakini jitihada zinaweza kufanyika, angalau kuupunguza wizi huo.
Kilio changu cha kwanza kabisa ni KATIBA. Inanisikitisha kusema kuwa mimi nilikuwa mwanachama wa TANU, sijakuwa na wala sitakuwa mwanachama wa CCM. Nilipokuwa mwanachama wa TANU, niliamini kuwa chama cha TANU kilikuwa chama cha Wakulima na Wafanyakazi na sasa naamini kuwa CCM ni chama cha Matajiri na Wajanja.
TANU, ilifanya kazi nzuri sana ya kuweka na kuitekeleza mikakati ya kumuondoa Mkoloni, kwa madhumuni ya kumpatia mkulima na mfanyakazi (wananchi) uhuru wa kujitawala wenyewe.
Lakini, baada ya kushika madaraka TANU badala ya kuwapa wananchi HATAMU za nchi, zikachukuliwa na TANU yenyewe. Tanu si wananchi, TANU ni kikundi cha wananchi kilichoshirikiana na wananchi wengine katika harakati za kupata uhuru. Sasa badala ya wananchi kujitawala, TANU ikaziba nafasi iliyoachwa wazi na Wakoloni. TANU ikaanza kutawala.
Kwa kuwa KATIBA ya kwanza iliyotengenezwa Lancaster House, London, haikuwapa TANU nafasi ya kutawala, kitu cha kwanza TANU ilichofanya ni kuibadili kuwa KATIBA ya Jamhuri ya TANGANYIKA. Hapo ndipo TANU ilipopata nafasi ya kuweka vyama vyote vya wafanyakazi chini ya mwavuli wa TANU, Kisha ikavipiga marufuku vyama vyote vingine vya kisiasa. Ikaunda tena KATIBA na kuchukua HATAMU. Hapo sasa hata migomo ikawa haramu. Hapo ndipo ukawa UTAMU wote TANU.
Kwa bahati mbaya au nzuri ukapatikana huu muungano, ikabidi sasa iingie AFRO-SHIRAZ. Hii AFRO-SHIRAZ na Mzee Karume Snr.,
kidogo walikuwa wanaleta leta kinaa.Ikabidi itafutiwe mbinu ya kudhibitiwa. Hapo ndipo ikazinduliwa hii CCM. Nafikiri ingekuwa bora kama ile nyundo na lile jembe katika nembo ya bebendera ya CCM ingeondolewa ikawekwa nembo ya TWIN TOWERS.
Kisa hiki nilichokihadithia kwa muhtasari tu ndicho kinachonifanya niweke kilio changu katika KATIBA hii tuliyonayo hivi leo. KATIBA hii ndiyo inayotoa mianya ya wizi wa kura.
KATIBA haina "checks and balances" baina ya Executive Branch, Judiciary na Legislature.
Kila kitu kiko chini ya CCM na Viongozi wake and especially Rais. Na Rais ni Mwenyekiti wa CCM. Hupati nafasi ya kumkamata mwizi wa kura wala kuthibitisha wizi wenyewe.
Tangu mawakala vituoni, wahesabu kura, watunza daftari za wapiga kura, sijui mashekha, returning officers, polisi, na wengine wote mpaka National Electral Commission. Wote wako pale kwa ajili ya CCM na serikali yake. Iwe kwa ridhaa yao au kwa kuogopa kumwaga unga au kwaa kujikomba komba. Wizi wa kura utaondokaje?
KATIBA, KATIBA, KATIBA hapo ndio penye KICHAKA. Si unaona? Ukiitaja tu wenye nchi yao wanakwambia, KATU, hilo halitafanyika. Kwa nini? UTAJAZA MWENYEWE.