Vijana waaswa kuondokana na fikra mgando wakihitaji kufanikiwa kimaisha

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
422
1,049
Imeelezwa kuwa tatizo la kubwa la baadhi ya vijana toka familia zenye mazingira magumu kutojikita kuanzisha miradi ya kiuchumi ni kutokana na kujinyanyapaa wenyewe na kuwa na fikra mgando za kukata taamaa kama hawawezi kufanikiwa kiuchumi hata kama wakiwezeshwa .

Akizungumza katika Ukumbi wa Yatima, Kijiji cha Igoda, Kata ya Luhunga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa mara baada ya mafunzo ya mtazamo na miradi ya kilimo na ufugaji yanayotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya R-LABS Tanzania kwa vijana wa mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM) meneja msaidizi wa mradi huo, Danoford Mkumba alisema changamoto ya vijana wengi ni kutawaliwa na fikra mgando katika maisha yao hivyo ni vigumu kufanikiwa katika maisha.

Mkumba alisema vijana wanayo fursa kubwa sana na kufanikiwa katika maisha kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na mradi huo wa YAM pamoja na serikali kupitia Halmashauri zote nchini ambazo zimekuwa zikitenga fedha kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa kundi hilo la vijana ,wanawake na watu wenye ulemavu.

Alisema kuwa katika mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwafundisha fikra inayokuwa na fikra mgando yatasaidia sana vijana hao kujitambua na kuondokana na fikra mgando na kujikita katika fikra inayokuwa ambayo itawawezesha kusonga mbele kimaisha kwa kuja kuwa na miradi ya kiuchumi kupitia raslimali zinazowazunguka.
44c6fc1a-0891-43a9-b558-a2088646ba1e.jpg

Vijana kutoka mazingira magumu kata tatu za Ihanu, Mdabulo na Luhunga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa wakiwa kwenye majadiliano.
Mkumba alisema baadhi ya vijana wanaamini kuwa wakitoka katika familia duni kwao ni vigumu kufanikiwa katika maisha ila kwa mafunzo hayo vijana hao wataweza kujitoa katika fikra mgando na kwenda na fikra inayokuwa.

Washiriki wa mafunzo hayo Diana Yohana, Saraphina Tengelakwi na Andason Mpende wakielezea faida ya mafunzo hayo walisema wanamatumaini makubwa ya kuyatumia kubadili maisha yao kwa kwenda kubunia na kuendesha miradi yao ya kiuchumi .

Diana alisema kwa upande wake kutokana na ulemavu wake wa ngozi jamii inayomzunguka imekuwa ikitoa upendeleo mkubwa kwake na shida ya kutokuwa na mradi wa kufanya ni kutokana na kupata mimba za utotoni hali iliyopelekea kukwamisha ndoto yake ya kusonga mbele kimaisha hasa katika masomo .

Hivyo, alisema kwa mafunzo hayo ya kuondokana na fikra mgando iliyokuwa imemtawala anaamini wazi kuwa atakwenda kuwa mfano mwema kwa kuanzisha mradi wake ama kutimiza ndoto yake ya kurudi shule kwenda kusomea ualimu ili kuja kufundisha wenzake .

Huku Saraphina akidai kuwa sababu kubwa ya vijana kutokuwa na miradi yao ni kutokana na uwezo wao wa kufikiri kimaendeleo na wengi wao kuishia kufikiri kurudi nyuma kwa kujitazama familia wanazotoka zilivyo duni na wao kukatishwa tamaa ya kusimamia kufanya shughuli za kiuchumi na kwa mafunzo hayo wanaweza kusimama kusonga mbele zaidi .

Mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM) umelenga kuwawezesha vijana zaidi ya 770 wakiwemo watoto 150 yatima kutoka kata hizo tatu ambazo zote zitaunganishwa na vijiji 16 za mradi huo.

Mradi huo wa YAM ni wa miaka minne toka mwaka 2021/2024 umefadhiliwa na Serikali ya Finland chini ya Taasisi yake ya Diaconess kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Taasisi ya Foxes Community and Wild Life Conservation.


Chanzo: Matukio Daima
 
Back
Top Bottom