Vijana wa Kenya wakumbatia ujuzi wa kidijitali huku kukiwa na ongezeko la ajira za kujitegemea

Vijana wa Kenya wakumbatia ujuzi wa kidijitali huku kukiwa na ongezeko la ajira za kujitegemea

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,242
Reaction score
1,212
VCG211249257044.jpg


Akiwa ameketi kwenye kiti cha plastiki kwenye kituo cha teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika mji wa Ndhiwa, takriban kilomita 366 kutoka Nairobi, mji mkuu wa Kenya, vidole vya Jackline Juma vinacheza kwa kasi wakati anapobonyeza kibodi ya kompyuta.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 ambaye amehitimu shule ya upili mara kwa mara hutazama kwenye skrini ya kompyuta ili kuangalia kama kuna makosa kabla ya kuendelea kuandika. “Nimekuja katika kituo hiki kwa ajili ya mafunzo baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2024 ili nipate ujuzi wa kidijitali wa kuutumia maishani,” alisema Jackline.

Alisema kwamba bila kupata ujuzi huo, angepata tabu kuendelea na elimu yake, kupata kazi, au hata kuwasiliana vizuri.

Jackline ni mmoja wa vijana wengi wa maeneo ya vijijini wanaokwenda kila siku kwenye vituo kama hivyo vilivyopo kote nchini, wakiwa na shauku ya kupata ujuzi mpya ambao utawasaidia kunufaika na fursa zinazoongezeka za ajira za kujitegemea.

Katika vituo hivyo, vijana hujitumbukiza katika programu mbalimbali za kujifunza masuala ya kidijitali, kuanzia ujuzi wa msingi wa kompyuta hadi ujuzi wa juu zaidi kama vile kuweka misimbo, ujasiriamali mtandaoni, kuingiza data, usaidizi wa mtandaoni, ukuzaji wa app na tovuti, na usanifu wa picha.

Ujuzi wanaopata unawasaidia kuwa na mwelekeo mpya wa kazi katika soko la ajira za kujitegemea, ikiwa ni pamoja na kazi za kujitegemea, kuandaa maudhui ya kidijitali, usaidizi wa mtandaoni, uchunguzi wa mtandaoni, kunukuu maandishi ya sauti, na kuingiza data.

Kevin Aroka, meneja wa kituo cha TEHAMA, anasema mafunzo ya bure yanayotolewa chini ya Mpango wa Ajira Digital unaoendeshwa na serikali yanawapa vijana ujuzi muhimu wa kidijitali.

"Vijana wengi sasa wanajua kuwa fursa za ajira za jadi zimepungua kwa hivyo wanatafuta kazi za kidijitali kama vile kuandika, kuandaa maudhui, na kuingiza data," alisema.

Aroka aliongeza kuwa mafunzo hayo, sio tu yanaboresha ujuzi wao wa kidijitali bali pia yanawatayarisha kwa ajili ya soko la ajira za kujitegemea. Mbali na kozi zinazowasaidia vijana kupata pesa mtandaoni, Aroka anasema pia wanafundisha ujuzi wa kifedha na usalama wa kazi mtandaoni.

Alisema kuna vituo vingine vitatu huko Ndhiwa, na kila kituo kinatoa mafunzo kwa wanafunzi wasiopungua 50 kila baada ya miezi mitatu.

"Hapa Kosewe, tumetoa mafunzo kwa vijana wapatao 3,394; Kobodo, 1,930; Ratanga, 2,851; na Pala, 900. Tumefanya hivi kwa takriban miaka miwili sasa, na wengi wao sasa wanapata mapato kutokana na soko la ajira za kujitegemea," alisema na kubainisha kuwa mafunzo hayo yanafadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la eneo hilo.

Kwa mujibu wa Aroka, moja ya kazi mashuhuri iliyokamilishwa na wahitimu wa ustadi wa kidijitali wa kituo hicho ni kunakili hati za Idara ya Mahakama.

"Wanafunzi walikuwa wakipata hadi shilingi 25,000 (kama dola za Marekani 193) kwa mwezi kutokana na kazi hiyo. Jambo hili liliwahimiza wengine wengi kujiandikisha katika programu hiyo, na sasa idadi kubwa ya wanafunzi wanapata kazi za mtandao," alisema.

Kwa mujibu wa John Tanui, katibu mkuu wa Wizara ya Kitaifa ya TEHAMA na Uchumi wa Kidijitali, mpango wa mafunzo ni mojawapo ya mipango ya serikali ya Kenya ya kutoa nafasi za ajira. Hadi kufikia sasa, serikali imeanzisha zaidi ya vituo 400 vya TEHAMA kote nchini, vinavyotoa mafunzo ya fursa za ajira mtandaoni, zikiwemo kazi za kujitegema na soko la kidijitali, kwa zaidi ya watu 500,000.

Rais wa Kenya William Ruto alisema hivi karibuni kuwa serikali yake inatumia teknolojia ya kidijitali na uvumbuzi kutoa nafasi za ajira na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, ambapo asilimia 30 ya vijana hawana ajira. Amesema lengo ni kuunda jumuiya ya wafanyakazi wa kidijitali kote nchini Kenya, na kurahisisha makampuni ya kimataifa kuajiri vijana nchini.

Kulingana na Wakfu wa Mastercard, wafanyakazi wapatao milioni 1.2 wa Kenya, ambao wengi wao wanafanya kazi kwa njia isiyo rasmi, wameajiriwa kufanya kazi za kujitgemea, ambapo inakadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 109 kila mwaka.

Kwa Brighton Odhiambo, mmoja wa wanafunzi, mustakabali wa ajira nchini Kenya, kama katika sehemu nyingi duniani, uko mtandaoni. Amesema anapanga kujifunza ujuzi wa kidijitali kadiri awezavyo ili aje kuwa hodari na kupata mapato mazuri kwenye soko la ajira za kujitegemea.
 
Tukisema kenya wapo mbele mnatunyanyapaa, fikiria program kama hizo zinagharimiwa na mfuko wa jimbo, haya mabunge ya ccm hizo hela za jimbo ndiyo wanaenda kuhongea makahaba
 
Back
Top Bottom