Uwekezaji Mahiri Katika Maeneo ya Kimkakati ya TAWA Kuiingizia Serikali Zaidi ya Dola za Marekani Milioni 314

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,898
943

UWEKEZAJI MAHIRI KATIKA MAENEO YA KIMKAKATI YA TAWA KUIINGIZIA SERIKALI ZAIDI YA DOLA ZA KIMAREKANI MILIONI 314

Na Beatus Maganja, Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema Serikali inatarajia kupata mapato yanayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 314 katika kipindi cha miaka 20 kutokana na uwekezaji mahiri katika maeneo saba (7) yaliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA

Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo Januari 03, 2024 katika hafla ya utiaji saini mikataba ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas - SWICA) kati ya TAWA na Makampuni manne ya uwekezaji yanayofanya shughuli za utalii ndani na nje ya nchi iliyofanyika chuo cha utalii cha Taifa (NCT) Jijini Dar es Salaam.

Waziri Kairuki amesema kupitia uwekezaji huo unaokadiriwa kuwa na thamani ya TZS bilioni 696 wawekezaji watawajibika kuwekeza kwenye miundombinu katika maeneo yao ya uwekezaji na kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo hayo wananufaika na kuona umuhimu wa aina hiyo ya uwekezaji.

Aidha amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania kwa kufanya filamu maarufu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeleta matokeo makubwa kwa kuleta ongezeko kubwa la watalii nchini

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema baada ya upembuzi yakinifu uliofanywa katika nchi za SADC kuhusu uwezekano wa modeli hii ya biashara (SWICA), uzoefu ulionesha kuwa modeli hii inajulikana kwa uwezo wake wa kuwezesha Mamlaka za eneo lililohifadhiwa kuzalisha mapato endelevu kwa ajili ya uhifadhi na maendeleo.

Aidha amesema mapato yanayotarajiwa kuzalishwa kwa mwaka ni mara tisa (9) ya mapato yaliyokuwa yakipatikana awali kwa shughuli za utalii zilizokuwa zikifanyika maeneo hayo, hivyo ongezeko hili la mapato linaashiria kwamba mpango wa biashara wa SWICA ni chaguo zuri la kufikia matumizi bora na endelevu ya rasilimali ya wanyamapori kwa manufaa ya kiuchumi

Aidha amesisitiza kuwa TAWA imejipanga vyema kuhakikisha inatekeleza vyema miradi yote ya SWICA katika maeneo husika kwa kushirikiana na wawekezaji

Maeneo ya kimkakati ya uwekezaji mahiri yanayotajwa kuwekezwa ni Pori la Akiba Mkungunero (Dodoma), mapori ya akiba Ikorongo na Grumeti (Mara) pamoja na Pori la Akiba Maswa (Kimali, Mbono na Kaskazini) Mkoani Simiyu.

Aidha, Makampuni yaliyowekeza katika maeneo hayo ni Bushman Safari Trackers Ltd (Maswa GR North), Grumeti Reserves Ltd (Grumeti na Ikorongo GR), Mwiba Holdings Ltd (Maswa GR Mbona na Maswa GR Kimali) pamoja na Kampuni ya Magellan General Trading LLC (Mkungunero GR).

Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb), Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko

Wengine ni Makamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Uhifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), baadhi ya watendaji na maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA pamoja na wadau mbalimbali wa uhifadhi.
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.28(1).jpeg
GC693DXXEAAY7xN.jpg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.29(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.29(2).jpeg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.32.jpeg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.41.jpeg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.40(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.40.jpeg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.37(2).jpeg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.35(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-01-03 at 18.14.39(1).jpeg
 
Back
Top Bottom