UVIVU na UZEMBE ni kosa la jinai

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
422
1,049
Je, umewahi kuwaza kuwa UVIVU na UZEMBE ni kosa linaloweza kusababisha mtu akahukumiwa kifungo kwenda jela au kuadhibiwa kulipa faini?

Majibu yapo hapa kwenye makala hii twende pamoja ili kufahamu zaidi.

UVIVU ni hali ya mtu kutotaka kufanya kazi kiakili au kimwili. UZEMBE ni hali ya mtu kukosa uwajibikaji na umakinifu katika kutenda pamoja nakutojali hali ya mazingira.

Mara nyingi watu wanaweza kutenda kosa hili huku wasijue ya kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai linaloweza kusababisha akafungwa jela au kuadhibiwa kulipa faini.

Leo nataka ufahamu mambo yafuatayo ili ujenge umakini katika maisha yako na ufahamu namna ya kujiepusha kutenda kosa hili ambalo watu wengi wanaposhikwa na kutiwa hatiani wanadhani kuwa wanaonewa ili hali ni kweli wametenda kosa la kijinai na wanastahili adhabu kwa mujibu wa sheria.

1. Sheria hairuhusu mtu kufanya Umalaya au kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara au kuzurura na kushawishi mahali popote pa hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya.

2. Sheria hairuhusu mtu kutangatanga au kujiweka mahali popote pa hadhara kwa lengo la kuomba au kukusanya sadaka, kumtuma au kumhimiza mtoto kufanya hivyo.

3. Sheria hairuhusu mtu kucheza kamari kwa fedha au thamani ya fedha katika mahali pa hadhara.

4. Sheria hairuhusu mtu kutangaza nje ya nchi na kujaribu kupata au kukusanya sadaka kwa kuonesha majeraha au kilema.

5. Sheria hairuhusu mtu kujiweka mbele ya hadhara katika hali ambayo inapelekea uvunjifu wa amani. Mfano: kushika bunduki au bomu mbele ya hadhara kunaweza kutishia hali ya amani na usalama na kuwajengea hofu watu waliopo katika eneo husika.

6. Sheria hairuhusu mtu kufanya kitendo cha aibu mbele ya hadhara bila ya udhuru wa halali.

7. Sheria hairuhusu mtu kushawishi kwa mambo yasiyokuwa ya kimaadili mahali pa hadhara.

8. Sheria inakataza mtu mwenye afya kamili kukaa bure bila kujishughurisha na kazi yoyote ya uzalishaji au kukaa bila ya kuwa na namna inayoonekana waziwazi kuwa inamwezesha kujikimu. Hivyo, Kukaa bure bila kazi hali ya kuwa huna tatizo lolote bali una nguvu, akili na uwezo wa kufanya kazi ni kosa kisheria.

9. Sheria inakataza mtu aliyeajiliwa chini ya ajira halali inayotambulika kuchezacheza au kufanya mzaha wakati wa muda wa kazi bila ya kuwa na udhulu halali. Hivyo, inatakiwa katika muda wa kazi uache kufanya masihara au mizaha isiyo na maana na badala yake ufanye kazi kwelikweli ili usije kutiwa hatiani.

Mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kutenda makosa yaliyotajwa hapo juu atahesabiwa kuwa ni mtu MVIVU na MZEMBE na mtu huyo anapaswa kuhukumiwa kifungo cha kwenda jela au kulipa faini au vyote kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 176(a-i) cha Kanuni Ya Adhabu Za Makosa Ya Jinai,Sura ya 16 (Penal Code) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Hadi kufikia hapa nina imani utakuwa umejifunza na kutambua kwa kina zaidi juu ya kosa la UVIVU na UZEMBE.

Elimu bila mipaka na tunaendelea kujifunza na kujikumbusha kila uchwao kuhusiana na mambo mbalimbali ya kijamii.

It's me
A Lawyer and LifeCoach
Mr. George Francis
Contacts: 0713736006
Email: mr.georgefrancis21@gmail.com

Thank you very much.
 
Hizi sheria zingetiliwa mkazo basi tungekuwa na taifa imara sana kwasasa
 
Back
Top Bottom