UTEUZI: Rais Magufuli amteua Profesa Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali

chakii

JF-Expert Member
Sep 15, 2013
19,696
22,727
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk. John Magufuli amemteua Prof. Adelardius Lubango Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali.

Rais Magufuli amefanya uteuzi wa kwanza tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania kwa kumteua Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Kilangi ameteuliwa baada ya uteuzi wa awali kumalizika leo.

1604598550993.png


=====


RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameanza kuunda Serikali atakayoiongoza kwa miaka mitano ijayo 2020-2025 kwa kumteua Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Uteuzi huo umefanyika leo Alhamisi tarehe 5 Novemba 2020 saa chache kupita tangu Dk. Magufuli alipoapishwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuwa Rais wa Tanzania

Dk. Magufuli na makamu wake, wameapishwa kwa pamoja Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

“Profesa Kilangi ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili baada ya uteuzi wa kipindi cha kwanza kumalizika leo tarehe 05 Novemba, 2020,” imeeleza taarifa ya Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Kilangi alikuwa AG, wadhifa alioteuliwa tarehe 1 Februari 2018 na Rais Magufuli ili kuchukua nafasi ya George Masaju ambaye alimteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Itakumbukwa, mara baada ya Rais Magufuli kuingia Ikulu kwa mara ya kwanza tarehe 5 Novemba 2015, alimteua Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Masaju alishika wadhifa huo wa AG kuanzia tarehe 3 Januari 2015 alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete ili kuchukua nafasi ya Fredrick Werema.

Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani, aliendelea na Masaju kwa kumteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) nafasi aliyohudumu hadi tarehe 1 Februari 2018 alipomteua Profesa Kilangi.

Kabla ya uteuzi huo wa Profesa Kilangi kuwa AG, alikuwa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (St. Augustine University) kituo cha Arusha na pia Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (Tanzania Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA).
 
Back
Top Bottom