Utamu wa PM: (JF series)

Utamu wa PM: (JF series)

Ryan The King

JF-Expert Member
Joined
Oct 6, 2016
Posts
2,789
Reaction score
2,706
UTAMU WA PM.

MTUNZI:
MICHAELRAY.

Itarushwa Kila jumamosi saa 20:30 Usiku.

Eneo lote lilifunikwa na giza huku ukungu na mawingu mazito angani yakifanya msitu ule kutisha. Msitu ulikuwa kimya kiasi kwamba hata panya angekuwa akitembea basi nyayo zake zikitoa sauti.

Micky alipata fahamu. Hakujua yupo wapi na kwa Nini yupo pale. Hakujua ni vipi alifika kwenye eneo hilo hatari.

Micky alivuta kumbukumbu Lakini hakuweza kukumbuka chochote. Alivuta pumzi nzito na kuiachia taratibu. Kiasi alijisikia afya baada ya zoezi hilo.

Alitaka kunyanyuka lakini hakuweza. Alihisi maumivu kutoka mgongoni. Taratibu alipeleka mkono wake kuelekea mgongoni akakuta jeraha kubwa linalovuja damu. Micky alilia sana. Hakujua ni jinamizi gani lililomkuta.

Michirizi ya machozi ilipita katika mashavu yake huku kwikwi ikimkaba na kusababisha atoe sauti iliyovuruga utulivu wa msitu.

Alijiburuza Kama chatu aliyemeza kuelekea asipopajua. Bado msitu ulikuwa kimya Sana. Upepo wenye kaubaridi ndivyo vilikuwa vikiranda randa.

"Lazima nijikaze Kama mwanaume"
Micky aliongea akijaribu kusimama. Wakati huu alifanikiwa japo alitembea kwa kuchechemea.

Alitembea Kama mita Mia moja akiwa na lengo la kutafuta barabara lakini alichoambulia ni Vichaka vyenye miba.

Kilichomsaidia kwa muda ule ni kuwa mwili wake ulikuwa umekufa ganzi. Hivyo hakuweza kuhisi maumivu yoyote.

Ghafla Mick alisimama na kutega sikio Kama mtu aliyesikia kitu. Alisikia sauti ya mvumo wa maji mengi Kama maporomoko ya maji. Alitembea Kama mtu aliyepata tumaini jipya.

Haikumchukua dakika kumi tayari mbele yake aliona mto mkubwa ambao katikati kulikuwa na majabali makubwa.

Micky aliinama akanywa maji ya mto ule na kuosha uso wake uliokuwa umejaa nyasi. Muda huu alionekana kuchangamka zaidi. Alivua nguo zake na kujimwagia mwili wake uliokuwa umekufa ganzi kwa majeraha.

Sasa aliamsha hasira ya majeraha yaliyokuwa yamesinzia katika ngozi yake. Maumivu aliyoyapata hakuwa kuyapata tokea kuzaliwa kwakwe. Yalikuwa maumivu yasiyo na mfano.

Micky alijilaza ukingoni mwa mto. Aligugumia Kama beberu lenye nyege.
Alishtuka kusikia kishindo ndani ya maji. Aliangalia kule kishindo kilipotokea. Mapigo ya moyo yalimuenda mbio. Vinyweleo vilimsisimka. Hakuamini alichokiona. Alijihisi Kama yupo kwenye filamu za Hollywood. Sasa akili yake iliweza kuvuta baadhi ya kumbukumbu. kumbukumbu iliyomjia haraka ilikuwa kumbukumbu ya filamu ya KingKong.
Hii ni baada ya kuona kiumbe Cha kutisha kifananacho na Sokwe Mtu.

Micky alisahau habari za majeraha yake. Alikimbia Kama mwanariadha mashuhuri anayewania Nobeli ya dunia. Lile jitu mfano wa Sokwe nalo lilimfuata kwa mwendo wa ado ado. Na kila lilipoweka nyayo basi liliacha na kishindo. Kishindo kilichoupasua moyo wa Michy.

Micky aliona kifo kikimpungie mkono wa ukaribu huku uhai ukimpa ishara ya huzuni ya kwaheri. Lazima ajitahidi. Hilo ndilo lilikuwa moyoni mwake.

Kila Mara alitazama nyuma kumuangalia zimwi linalomuandama. Kila alipokatisha Jitu lipo nyuma yake mithili ya kivuli chake.

Mbele yake pango kubwa, nyuma yake Jitu kubwa. Micky alizama kwenye pango ambalo lilikuwa na pazia la utando wa buibui. Tandabui zile zilimsonga usoni akasimama na kugeuka nyuma. Lile jitu lilishindwa kupenyeza kwenye mlango wa Pango.

Lilinguruma kwa sauti yenye kutisha na kufanya msitu wote mzizime. Na popo waliomo pangoni walitoka wakimpiga vikumbo Micky aliyekuwa akitweta Kama panya aliyekoswa koswa na mtego.

Lile Jitu liliondoka likiwa limekosa kitoweo. Popo waliendelea kutangatanga pangoni pale wakimzonga Micky kana kwamba wanamkaribisha.

Micky alitafuta sehemu tulivu mule pangoni akajipumzisha. Mawazo yalibisha hodi katika kichwa chake. Aliwaza hatima ya maisha yake pale msituni. Alifikiri ni kwa namna ipi ataweza kutoka pale msituni ikiwa hajui alifika vipi.

Usingizi ulimnyemelea Micky akajikuta akikoroma kwenye Msitu wa kuzimu. Akiwa usingizini Micky alianza kuota;

"Isabela alifungua geti na kuingia ndani. Mwendo wake wa haraka ulionyesha Shari aliyokuja nayo. Alifungua mlango wa sebuleni kwa nguvu Hali iliyomshtua Mama Kelvin aliyekuwa amejilaza Sofani Akitizama Luninga.

Mama Kelvin akiwa na hofu alimtazama Msichana aliyembele yake ambaye ni hakika alikuwa hamjui. Isabela alimuangalia kwa hasira Mama Kelvin.

"We Malaya, ujana wako uliulia wapi mpaka ulie uzee wako kwa Micky wangu?"
Isabela aliongea kifua kikipanda na kushuka.

"Weeee! Wee! Koma! Malaya Mama yako"
Mama Kelvin alibwatuka tayari akiwa amesimama kwa Shari.

Micky aliingia getini, akiwa karibu na Mlango alisikia kelele za Mama Kelvin na Isabela wakigombana.

Hakutaka kufungua Mlango. Alibaki nje akisikiliza Ugomvi wa wapenzi wake.

Ndani Ugomvi ulizidi kupamba Moto. Isabela alimvamia Mama Kelvin na kumbwaga chini Kama gunia. Isabela alitumia ujana wake vizuri hivyo alimshinda Mama Kelvin wepesi na nguvu.

Mama Kelvin akijitahidi akaponyoka pale chini na kukimbilia kwenye Kochi. Alipofika kwenye Kochi alinyanyua mto na kutoa Bastola iliyomfanya Isabela amtazame Mama Kelvin kwa Wasi wasi mwingi.

"Nakuua we mwanaizaya"
Mama Kelvin aliongea akiwa amemnyooshea Isabela Bastola.
Isabela alibaki kumtazama akishusha pumzi Kama Bata dume.

Mara sauti ya risasi ilisikika na Isabela akadondoka chini. Micky kusikia Mlio wa Bastola alifungua Mlango na kuingia ndani kwa Kasi.

Macho yake yalikutana na mwili wa Mpenzi wake ukiwa umedondoka sakafuni huku damu nyingi zikitoka.

"Hapana! Noo! Isabela"
Alipiga makelele akiwa tayari ameufikia mwili wa Isabela. Alimtikisa akimuamsha bila mafanikio. Isabela Bado alikuwa kalala.
Mama Kelvin Bado alikuwa ameshika Bastola yake akiingalie sinema aliyoibuni yeye.

"Umemfanya Nini Mchumba wangu wewe Paka shume"
Micky alisimama na kumuuliza Mama Kelvin.
Hata hivyo Mama Kelvin alibaki kumtazama bila kumjibu.

"Si naongea na wewe"
"Mbwa kafia kwa muuza supu, wewe ndiye mnywaji chukua Mbwa wako"
Mama Kelvin alijibu.

"Kwa hiyo wewe mjanja si ndio"
Micky aliongea huku alicheka machozi yakidondoka moja moja Kama mvua ya msimu wa kiangazi.

"Na wewe unataka ufe"
MaMa Kelvin aliuliza na hapo hapo akaachia Risasi.

Micky alishtuka mno. Kumbe ilikuwa ni ndoto alikuwa anaota akiwa pangoni.

Sasa alikumbuka kila kitu.

Itaendela...
 
Back
Top Bottom