Usife kibwege kama Ted Jorgensen

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,446
images (1).jpeg

images.jpeg

AKIWA Kijana, alifanya tukio. Hakujuta. Na akasahau. Akaishi miaka 44 mingine. Ndipo akatokea mtu akamkumbusha kile alichokifanya. Akaumia. Akatamani asahihishe makosa yake. Hakupata fursa hiyo. Miaka mitatu baadaye akafariki dunia akiwa mwenye huzuni kubwa.

Zingatia, ujana ni tapeli mkubwa wa maisha. Ujana utakulaghai na kukufanya uone maisha ni hayohayo uliyonayo katika wakati uliopo. Ujana unaweza kukughilibu na kukusahaulisha ujio wa kesho. Ujana hufumba macho na huziba masikio. Si walisema ujana maji ya moto?

Ted Jorgensen, alipokuwa na umri wa miaka 17, alikutana na binti mrembo, Jacklyn Gise, aliyekuwa na umri wa miaka 16. Wakapendana. Wakaanza safari ya mapenzi.

Jacklyn akanasa ujauzito.
Wakati Jacklyn anashika mimba, alikuwa mwanafunzi wa high school. Ted alikuwa mcheza sarakasi aliyekuwa na ndoto za kufanikiwa kwenye mchezo huo.
Januari 12, 1964, mtoto akazaliwa. Jeffrey ndilo jina walilompa.

Jeffrey alipozaliwa, Ted alikuwa ameshatimiza umri wa miaka 18, Jacklyn miaka 17. Na sababu ya mtoto na malezi, ndoto za masomo zikayeyuka. Ted na Jacklyn wakafunga ndoa.

Maisha ya ndoa yakawa magumu. Ted alikuwa mlevi kupindukia. Mara arudi nyumbani alfajiri au asirudi kabisa. Ted alikuwa na kipato kidogo lakini hakukitumia kulea familia, bali starehe zake binafsi.
Baada ya miezi 17 ya ndoa, Jacklyn akaomba talaka. Ted akakubali. Wakaachana. Jacklyn akarudi kwa wazazi wake. Miaka miwili baadaye, Jacklyn akapata mwanaume mwingine, Miguel Bezos.

Wakafunga ndoa. Bezos akaomba kumuasili Jeffrey awe mwanaye kisheria. Ted akasaini nyaraka zote kuhalalisha mtoto wake atwaliwe na Bezos.

Mwaka 2012, mwandishi Brad Stone alipokuwa anakusanya taarifa ili aandike kitabu “The Everything Store” kilichohusu maisha ya bilionea mmiliki wa kampuni ya Amazon, Jeff Bezos, alimfikia Ted. Akamuuliza kama alikuwa na habari kuhusu mwanaye aliyezaa na Jacklyn mwaka 1964.
Ted akavuta kumbukumbu, kisha akajibu: “Nimekumbuka. Hivi yule mtoto bado yupo hai kweli?” Brad akamjibu: “Yupo hai. Ndio huyu bilionea mmiliki wa Amazon.” Ted akasikitika, lakini akakiri hakuwa baba bora kwa Jeffrey wala mume mzuri kwa Jacklyn.

Kuanzia hapo, Ted alianza kutafuta nafasi ya kuonana na mwanaye Jeffrey, angalau wazungumze, japo amtambue. Nafasi hiyo angeipata wapi?

Mwaka 2014, Ted aliumwa sana. Akaandika barua nyingi kwa Jeffrey, kumjulisha hali yake na kiu yake ya kumuona kabla hajaaga dunia. Hakupata majibu.
Hakuna ajuaye kama Jeffrey aliziona hizo barua na kumkaushia au hakuziona kabisa. Ila ni uhakika kuwa alitambua kuwa baba yake mzazi alikuwepo.

Mwaka 2015, Ted alifariki dunia bila kuonana na mwanaye wa damu, Jeffrey. Aliishia kumsoma na kumuona kwenye vyombo vya habari kama watu wengine.
Kuhusu maisha ya Ted; baada ya kuachana na Jacklyn, aliendelea na mitikasi yake ya kucheza sarakasi na ulevi. Miaka 10 baadaye, akagundua maisha aliyokuwa akiishi hayakuwa na kesho nzuri. Akaacha ulevi. Akafungua duka la kuuza baiskeli. Hiyo ndio ikawa kazi yake mpaka alipofariki dunia.

Ted baada ya kuachana na maisha ya ulevi, alimuoa mwanamke mwingine, jina lake Linda. Hakupata mtoto mwingine. Mkewe, Linda, alikuwa na watoto wanne.

Miaka miwili baada ya kifo cha Ted, taasisi ya utafiti wa mali na utajiri duniani ya Forbes, ilimtangaza Jeffrey kuwa tajiri namba moja duniani. Akimpita tajiri namba moja wa muda mrefu duniani, Bill Gates.
Kwa sasa, Jeffrey ana utajiri wa dola 183.6 billioni, ambazo ni sawa na Sh242.4 trillioni.

Jeffrey anatambua kuwa Ted ni baba yake, kwani cheti chake cha kuzaliwa na kumbukumbu zote za hospitali zinamtaja Ted ndiye baba yake.

Hiyo ni stori kuhusu tajiri namba moja duniani, Jeff Bezos na baba yake mzazi, Ted Jorgensen. Story kuhusu ujana na utapeli wake.

Ted angejua? Maskini hakujua. Alikufa akijuta. Angejua Jeff ndiye mwanaye wa pekee, angekubali kumwacha kwenye mikono ya baba mwingine? Angefunuliwa kuwa Jeff angekuwa tajiri namba moja duniani, unadhani angemtelekeza?
Hata hivyo usimlaumu sana Ted.

Alitapeliwa na ujana. Siku zote elewa hili, ujana ni tapeli mkubwa mno kwenye safari ya maisha.

©Luqman Maloto
 
Mungu anayo nafasi kwa kila mtu mmoja mmoja, hivyo tunapo fanya makosa tunapaswa kutubu na kujutia dhambi zetu na kisha tunarejea katika njia iliyo bora na yenye kumpendeza Mungu.
Binafsi sioni kama Ted alikufa kibwage, bali alikufa kama mtu yeyote anavyo fikia ukomo wa kuishi. Nafikiri Ted alikufa akiwa na sononeko kubwa moyoni.
 
Maisha yamejaa nasibu. Huenda huyo mzee angemlea vizuri jeff, pengine jeff asingekuwa billionaire. Kimsingi hatupaswi kujuta kwa lolote, ila kwa kuwa binadamu huwa na matarajio basi majuto huwepo.
Cause and Effect.

Ni ngumu sana kujua namna gani mtoto angekuwa kama malezi yake yangebadilika
 
Back
Top Bottom