Kwa miaka mitatu na nusu, Amina Ally Sauko amesaidia kuratibu operesheni za treni za Shirika la Reli la Tanzania (TRC) kutoka kwenye Kituo chake cha Usimamizi wa Operesheni kilichoko jijini Dar es Salaam, ambako uhakika na kufanya kazi pamoja kama timu ni muhimu. Amina, ofisa usafiri wa TRC mwenye umri wa miaka 35, anasema kituo hicho, ambacho ni kiini, ni zaidi ya sehemu ya kazi; ni sehemu ambapo matakwa ya Tanzania ya maingiliano, ufanisi, na ukuaji yanakutana.
Mwaka 2025, kazi yake hiyo ilimpeleka mbali zaidi ya mipaka ya Tanzania. Baada ya kuchaguliwa kujiunga na mradi maalum wa ujenzaji wa uwezo, alitumia miezi mitatu nchini China akipata mafunzo ya kina kuhusu njia za reli, uzoefu anaouelezea kama “fursa ya dhahabu.”
Amina alikuwa miongoni mwa wataalamu 67 wa reli wa Tanzania, wakiwemo wanawake 11, ambao walimaliza mradi ulioandaliwa na Shirika la Kiraia la Uhandisi na Ujenzi la China (CCECC) na kufanyika katika Chuo Kikuu cha Jiaotong mjini Beijing na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi wa Reli na Ufundi Stadi cha Zhengzhou. Mradi huo uliandaliwa kukabiliana na mahitaji ya dharura ya wafanyakazi wenye uzoefu kuongoza mtandao unaopanuka wa reli ya SGR nchini Tanzania. Washiriki walitoka katika nafasi mbalimbali, kutoka madereva, wakaguzi wa mabehewa, mafundi, wafanyakazi wa mizigo, mpaka maofisa wa usalama.
Katika Chuo Kikuu cha Jiaotong mjini Beijing, wataalamu wanatambulishwa kwenye mifumo ya msingi ya reli za kisasa, na Amina anasema mafunzo hayo yalikuwa ya kina na yamewapa msingi imara wa kazi yao. Baada ya wiki moja mjini Beijing, wataalamu hao walielekea Zhengzhou, kituo kinachoshamiri cha reli kilichoko katikati ya China, ambapo walitumia karibu miezi mitatu wakijikita katika mafunzo ya kivitendo.
Katika Chuo cha Ufundi wa Reli na Ufundi Stadi cha Zhengzhou, mtaala ulijikita katika maeneo manne muhimu: ufundi na ukaguzi wa magari, ili kuhakikisha vichwa vya treni na mabehewa yanakidhi vigezo vya kimataifa vya usalama; usimamizi wa usalama wa abiria na mizigo, ambako walijifunza itifaki za kulinda abiria na mizigo; ufanisi wa usafirishaji, ambapo walifundishwa sanaa ya kuratibu treni kwenye mitandao yenye shughuli nyingi; na usimamizi wa mifumo ya uendeshaji, inayohusisha kuingiza usimamizi wa teknolojia na binadamu kwa udhibiti mzuri.
Mafunzo hayo yalihusisha maelekezo darasani na mafunzo kwa vitendo, na wataalamu walifuatilia operesheni za moja kwa moja za uendeshaji, kusomea mifumo ya kisasa ya ishara, na kujifunza kwa vitendo changamoto za kuigiza zinazoendana na za hali halisi. Amina anasema, waliunganisha kile wanachokifahamu kutoka Tanzania na kile walichojifunza nchini China, na hivyo kuimarisha zaidi ujuzi wao.
Kujionea mifumo ya kisasa ya reli nchini China kumewasaidia wataalamu hao kutoka Tanzania kufikiria hatma ya baadaye ya reli nchini humo, sio kama ndoto iliyo mbali, bali kama jambo linalowezekana. Kwa kuona jinsi mambo yanavyotendeka nchini China, wataalamu hao wanasema wameweza kuelewa jinsi ya kuboresha usalama, kuwa makini na muda, na uratibu nchini Tanzania.
Akiwa jijini Dar es Salaam kwa sasa, Amina anatumia kile alichojifunza nchini China katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Anasema kwa sasa anatazama operesheni za reli hiyo kwa njia tofauti, kwani anafikiria zaidi kuhusu ufanisi, uratibu, na usalama, na pia ana hisia kali ya kufanya kazi kwa pamoja kama timu.
Kwa upande wake, anaona kuwa safari kutoka Dar es Salaam hadi Beijing na Zhengzhou na kurudi tena Dar es Salaam ni ukumbusho kuwa nyuma ya kila ratiba ya treni na mifumo ya uendeshaji, kuna watu ambao wanajifunza, wanabadilika, na wanafanya kazi kuvuka mpaka ili kuziwezesha treni kusonga mbele.