Ushirikiano kati ya China na Tanzania waendelea kuimarika

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
1.jpg



Caroline Nassoro

Mwaka 2013, ndani ya mwezi mmoja tangu aingie madarakani, rais Xi Jinping wa China alifanya ziara nchini Tanzania, ambako alitumia ziara hiyo kutambulisha sera ya nchi yake kuelekea bara la Afrika, akisisitiza kuwa pande hizo mbili zitaendelea kutegemeana katika nyanja zote.

Katika ziara hiyo, pande hizo mbili zilisaini saini mikataba kumi na saba ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili itakayoshuhudia kuimarika kwa uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Kwa takriban miaka hiyo 10, tumeshuhudia miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu iliyotekelezwa na kampuni za China nchini Tanzania, ikiwemo barabara ya Shinyanga – Bariadi – Lamadi ambayo imejengwa na kampuni ya CHICO ya China.

Nikiwa mwenyeji wa mkoa wa Mara, kujengwa kwa barabara hiyo kumeweza kupunguza muda wa safari kwa saa kadhaa, kwani sasa hakuna haja ya kupitia Mwanza ili kwenda Musoma, bali ni rahisi zaidi kupitia barabara hiyo ya Shinyanga – Bariadi – Lamadi, na hivyo kupunguza kidhahiri muda wa safari.

Kutokana na ujenzi wa barabara hiyo, nimeshuhudia maeneo yaliyo kando na barabara hiyo yakipata maendeleo, kwa kuwa sasa yanafikika kirahisi na barabara imejengwa kwa ubora wa juu. Wakazi wengi wa maeneo hayo wamefungua maduka ya bidhaa ndogondogo wanazowauzia wasafiri, na pia wengine wamefungua migahawa na kuwauzia wasafiri chakula.

Mwezi Juni, mwaka 2018, shehena ya kwanza ya Muhogo mkavu kutoka Tanzania iliwasili katika bandari Qingdao nchini China, na hii ni kutokana na makubaliano kati ya nchi hizo mbili yaliyofungua mlango wa bidhaa hiyo kuingia katika soko la China. Lakini si zao la muhogo tu kutoka Tanzania ambalo limepata soko nchini China. Mwezi Oktoba, 2020, China na Tanzania zilisaini makubaliano ya kuruhusu maharage ya Soya kutoka nchini Tanzania kuingia kwenye soko la China. Kusainiwa kwa makubaliano hayo kati ya Ubalozi wa Tanzania hapa China na Mamlaka ya Forodha ya China kulifuatia majadiliano ya muda mrefu kati ya pande hizo mbili, na utafiti kuhusu uwezo wa Tanzania kuzalisha maharage hayo na kukidhi vigezo vinavyotakiwa ili kuingia kwenye soko la China. Mwezi Juni mwaka jana, shehena ya kwanza ya Soya yenye uzito wa tani 120.2 kutoka Tanzania iliwasili katika bandari ya Qingdao nchini China.

Si hayo tu, China pia imekuwa ikipeleka madaktari wake nchini Tanzania kusaidia kutoa matibabu kwa wananchi wa huko. Mwaka 2017, meli kubwa ya matibabu kutoka China ilitia nanga katika bandari ya Dar es Salaam, na madaktari wa Kichina waliweza kutoa tiba kwa wakazi wa jiji hilo na wale wa pembezoni bila ya malipo. Hii ni mara ya kwanza kwa China kupeleka timu ya madaktari wake nchini Tanzania, kwani ilianza kufanya hivyo kwa zaidi ya miongo mitatu sasa.

China pia imeshiriki katika ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu nchini Tanzania, ikiwemo barabara ya Shinyanga – Bariadi – Lamadi kama nilivyoeleza mwanzo. Lakini pia Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere kilichopo jijini Dar es Salaam, daraja la Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ambalo mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu, makusanyo yanayotokana na tozo yalifikia Tsh bilioni 66.

Katika sekta ya kilimo, uwekezaji wa China umeendelea kuonekana nchini Tanzania. Tukitolea mfano zao la mkonge, ambapo shamba kubwa la mkonge lililowekezwa na Kampuni ya Uwekezaji wa Kilimo ya China-Africa Tawi la Tanzania limeanzishwa kilomita 300 Magharibi mwa jiji Dar es Salaam. Katika shamba hilo, teknolojia za kilimo kutoka China zimegeuza eneo lililokuwa la nyika kuwa shamba lenye rutuba, na kutoa ajira kwa wakazi wengi wa eneo hilo.

Hapa nchini China nimepata fursa ya kukutana na wanafunzi wengi kutoka Tanzania ambao wamepata ufadhili wa masomo hapa China, na hivyo kuweza kujiendeleza zaidi kielimu, na kutumia ujuzi walioupata hapa China kujijngea uwezo zaidi wa kutimiza majukumu yao baada ya kurejea nchini Tanzania.

Si rahisi kukamilisha makala hii bila kuongelea msaada wa China kwa Tanzania mara baada ya janga la COVID-19 kutokea nchini humo. Wakati huo, pamoja na kuwa China ilikuwa inajitahidi kudhibiti maambukizi ya ndani, lakini ilikuwa mstari wa mbele kubadilishana uzoefu wake katika kukabiliana na virusi hivyo kwa nchi nyingine ikiwemo Tanzania. China ilipeleka shehena za vifaa tiba na vya kujikinga na maambukizi nchini Tanzania, na pia imepeleka dozi za chanjo ya virusi hivyo ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na maambukizi ya COVID-19.

Kwa mifano hiyo michache, ninaweza kusema kuwa, China imekuwa mwenzi mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania, na kutokana na ziara iliyofanywa na rais Xi Jinping nchini Tanzania mwaka 2013, na ziara iliyofanywa na rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan nchini China mwezi huu, ni wazi kuwa uhusiano wa kirafiki na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili utaendelea kudumishwa na kuendelezwa zaidi kwa ajili ya manufaa ya nchi hizo mbili pamoja na watu wao.
 
Back
Top Bottom