Elections 2010 Ushindi wa Kikwete 2010: Shubiri kwa CCM

Kiungani

JF-Expert Member
Feb 2, 2007
274
71
UCHAGUZI 2010: USHINDI WA JAKAYA KIKWETE, SHUBIRI KWA CCM
Mwaka 2005 wakati Jakaya Mrisho Kikwete akiwania kuwa Rais wa Nne wa Tanzania, aliendesha kampeni za ndani ya CCM kwa hila, mbinu na njia ambazo zilimpa ushindi ndani ya CCM na baadaye kuwa Rais wa awamu ya nne.

Hila, mbinu na njia alizotumia, japo ziliwapa baadhi ya watu na wafuatialiaji wa siasa matumaini makubwa, pia ziliwaumiza na kuwaangamiza wengi ndani na nje ya CCM katika mpito wake kufikia nafasi hiyo. Kuna wachache kama akina S. A. Salim, F.T. Sumaye, J.S. Malecela, P.J. Mangula, na hata B. W. Mkapa ambao bado wanauguza majeraha ya huo msuguano wa kugombea kuteuliwa ndani ya CCM.

Ikumbukwe kuwa B.W. Mkapa hakuwa mgombea mwaka 2005, bali alikuwa ni Mwenyekiti Taifa wa CCM na Rais anayemaliza muda wake, baada ya kupitishwa dhidi ya Kikwete mwaka 1995 kwa nguvu za Mwalimu Nyerere. Hilo halikuwa rahisi kwa Kikwete kulimeza na kamwe hakutaka kumpa Mkapa nafasi nyingine ya kummaliza 2005, hivyo ilikuwa wazi kuwa Kikwete asingependa au kuacha Mkapa awe na the last laugh. Kama wanavyosema waswahili ‘piga, ua’ Kikwete na mtandao wake walidhamiria na kuutaka u-Rais kwa udi na uvumba (literally!!), na hatimaye waliupata.

Kwa mantiki hiyo basi utaona kuwa mvutano na mvurugano uliokuwepo 2005, na kuzidi kupaliliwa na kukuzwa katika kipindi cha miaka 5 kuelekea uchaguzi wa 2010, kunaiweka CCM katika daraja bovu juu ya mto wenye mamba. Wakati wa u-Rais wa Kikwete 2005 – 2010 alitumia na anaendelea kutumia muda mwingi kuhakikisha kuwa maadui wake wa ndani ya CCM wanamalizwa kimya kimya na kufutiliwa mbali kwenye siasa za kitaifa. Viongozi kama Mangula, Salim, Sumaye, Malecela, J.J. Mungai, P. Kimiti, C.M. Mzindakaya, C.D. Msuya, J.S. Warioba, J. Butiku, marehemu Lawrence W. Gama, Mzee P.M. Ndejembi, C.N. Keenja na wengineo waliokuwa na msimamo kama wao walianza kukandamizwa kidogo kidogo na hatimaye kumalizwa kabisa ndani ya CCM ili Kikwete na kundi lake wazidi kujiimarisha.

Kuna wengine kama akina M.J. Mwandosya, S.J. Sitta, A.M. Diallo, W.V. Lukuvi na wengine ambao walipona msukosuko huo na kuzidi kujiimarisha kwa nguvu zao, bali hata hivyo hali zao ni tete na wanategemea kudra za Kikwete na mtandao wake.

Ukisogeza miaka na kuja mbele hadi 2010, utaona kuwa mtandao wa 2005 upo kwa vipande pande na nguvu za Kikwete kama Rais na kama Mwenyekiti Taifa wa CCM, zinasuasua kiasi kwamba sasa yeye Kikwete ndiyo anategemea ukombozi wa maadui zake na kudra za mtandao-mafisadi kama akina R.A. Aziz, A. J. Chenge, A.R. Kinana, N.M. Karamagi, E.N. Lowassa, B.P. Mramba, L.K. Masha, na viongozi wapofu wa maadili kama akina Y.M. Makamba (aka Baba January), K.N. Mwiru, R.M. Chegeni, E.J. Nchimbi, J.A. Msekela, P.J. Serukamba, S.M. Simba, na hasa hasa ‘nguvu’ za mke wake Salma, wanae Ridhiwani na Miraji, na ‘nguvu za ziada’ kutoka kwa wanajimu na wana-sayansi anga.

Vile vile kuna wale wengine ambao hawajui kama walie ama wacheke kama akina C.O. Ole-Sendeka, A.M. Kilango-Malecela, H.G. Mwakyembe, J.D. Lembeli na wengineo ambao aidha kwa nyakati tofauti walijitokeza ‘kumsugua’ vibaya Kikwete na sasa wanahitaji kudra zake ili nao ubwabwa wao usitiwe mchanga.

Kwa maana hiyo basi CCM imekuwa si Kikwete tu, ila vile vile CCM haina njia isipokuwa Kikwete. Hapa kuna maana gani?


Kwa mantiki ya kawaida, CCM kama chama kingembeba mgombea wake kwa hali na mali ili kumuuza kwa wapiga kura, kwa maana kuwa CCM si Kikwete tu bali iwe ye yote yule, CCM ingemnadi kwa nguvu zote.

Hata hivyo, kwa kuwa Kikwete kawamaliza maliza wale wote waliosuguana naye mabega kuanzia 1995 hadi sasa, na wachache waliopo wanaogopwa kumalizwa pia, basi CCM inajikuta haina mtu tena wa kumnadi isipokuwa Kikwete tu. Hata kama CCM watakaa pembeni na kuwaacha Baba, Mama na watoto wakichanja mbuga peke yao, mwisho wa yote CCM itabidi ikubali tu kuwa Kikwete na mizigo yake ndiyo CCM hiyo. Hawawezi kumpinga na hawawezi kumbeba.


Je, ni nini hatima ya haya yote?

Kuna uwezekano mkubwa kuwa uchaguzi wa 2010 Jakaya Mrisho Kikwete atashinda tena na kuwa Rais kwa miaka mingine 5, na muhimu zaidi ni kuwa atakuwa tena Mwenyekiti Taifa CCM kwa miaka mingine 5, kutokana na utaratibu wa CCM wa kuachiana hadi amalize muda wake. Kwa wataotaka kinga zake watasali na kupiga dua kuwa aendelee na katiba ibadilishwe aweze kupata muhula mwingine. Hizo sala na dua hazitafanikiwa. Kwa wale adui zake ndani ya CCM watasali na kupiga dua kuwa asimalize hata hii awamu ya 2010 – 2015, kwani wanajua kuwa watamalizwa ki-kweli kweli ndani ya CCM. Kama ikitokea kuwa hatamaliza 2010 – 2015, hayo yatakuwa mapenzi ya Mungu, na kazi ya Mungu haina makosa.


Ila kilicho wazi ni kuwa Kikwete aliyejeruhiwa 1995 si sawa na Kikwete aliyejeruhiwa 2005. Kikwete wa 1995 hakua anajua utamu wa Ikulu na vipambio viambatanavyo na u-Rais. 1995 aliambiwa wewe bado ‘mtoto’ kaa pembeni wakubwa wafanye kazi. Akakaa pembeni kwa hasira. Kikwete wa 2005 amekwisha onja utamu wa Ikulu kwa miaka 5, na sasa anaona kuna watu wanataka ayakose hayo yote, kuwa wanamwambia hawezi kazi. Hasira za 1995 changanya na 2005.

Ikiwa Kikwete wa 1995 aliweza kuwashughulikia na kuwamaliza hadi kuwa vipande vipande wale wote waliompinga, kumkejeli na kumdharau wakati ‘hajaukwaa’, nachelea kufikiri kile ambacho Kikwete wa 2005 atakachofanya mara tu akichoropoka katika hali hii na kurudi Ikulu na Uenyekiti Taifa CCM. Ya Babu Seya yatakuwa nafuu.

Tukumbuke kuwa kufura kwake wa sasa kunakolezwa pia na Mama na wana haswa Ridhiwani ambaye ni rubani msaidizi, ambao mwanzoni hawakuwa na hili wala lile katika ‘kazi za baba’, ila sasa wanaona kuwa mustakabali wao wa maisha unatishiwa.

Kwa mtazamo huo, ni wazi basi ushindi wa Jakaya Mrisho Kikwete 2010 ni shubiri kwa CCM. 2010 CCM wanacheza lizombe juu ya daraja bovu na chini kuna mto wenye mamba.

Wenye macho na tuangalie.
 
Interesting!!!!

Ikiwa Kikwete wa 1995 aliweza kuwashughulikia na kuwamaliza hadi kuwa vipande vipande wale wote waliompinga, kumkejeli na kumdharau wakati ‘hajaukwaa', nachelea kufikiri kile ambacho Kikwete wa 2005 atakachofanya mara tu akichoropoka katika hali hii na kurudi Ikulu na Uenyekiti Taifa CCM. Ya Babu Seya yatakuwa nafuu.
 
Je, ni nini hatima ya haya yote?

Kuna uwezekano mkubwa kuwa uchaguzi wa 2010 Jakaya Mrisho Kikwete atashinda tena na kuwa Rais kwa miaka mingine 5, na muhimu zaidi ni kuwa atakuwa tena Mwenyekiti Taifa CCM kwa miaka mingine 5, kutokana na utaratibu wa CCM wa kuachiana hadi amalize muda wake. Kwa wataotaka kinga zake watasali na kupiga dua kuwa aendelee na katiba ibadilishwe aweze kupata muhula mwingine. Hizo sala na dua hazitafanikiwa. Kwa wale adui zake ndani ya CCM watasali na kupiga dua kuwa asimalize hata hii awamu ya 2010 – 2015, kwani wanajua kuwa watamalizwa ki-kweli kweli ndani ya CCM. Kama ikitokea kuwa hatamaliza 2010 – 2015, hayo yatakuwa mapenzi ya Mungu, na kazi ya Mungu haina makosa.

I concur with your observations.
 
haya kaka kila mtu aandae sanda yake kusubiri kuzikwa akiwa hai
 
Safi sana kaka. kama ni uchcmbuzi umefanya wa kina. Sasa watakaoendelea kuihsbikia hiyo CCM kwa mapambio na nyimbo za bongo fleva kazi kwao.
 
Hata mimi nilikuwa nawaza kitu kama hicho, JK akifanikiwa kushinda wanaomsusia watakiona, tutajionea mengi ndani ya CCM, dalili zinaonyesha kwa kuzifanya kampeni kuwa za Baba mama na mwana zaidi ya kuwa za chama.
 
Niliposoma post ya Mkuu Kiungani, nilikubaliana naye. Baada ya hapo, nimekuwa nikisubiri wakati kama huu ufike ambapo ccm baada ya kung'amua kuwa magamba waliyojivika yamekuwa kipingamizi. Baad ya utambuzi huo wameamua kujivua magamba, lakini lo, hayavuliki! Mkuu Kiungani aliweza kuona mbali alipotubandikia post hii.
 
Back
Top Bottom