SoC01 Upendo, kusudi la maisha

Stories of Change - 2021 Competition

ChrissD

New Member
Sep 22, 2021
2
2
Heko kwa mkandarasi yule tusiewahi kumuona, japo ndie muasisi wa vyote tunavyoviona, kuvisikia na kuvihisi. Ubora na wake ufanisi si vyepesi kuunena, tena abadan si rahisi kuuelezea kwa marefu wala mapana.

Bila malalamiko ya wanyonge na shinikizo la mwenyekiti, wazo lilimjia tangu. Bila shahada na vyeti, akazitafiti mbingu. Bila agizo la mfalme na kamati, akafika mwenyewe saiti asiongozwe na askali mwenye kirungu. Bila fungu na bajeti, akaujenga ulimwengu mzuri wa kupendeza na imara usiochukiza, maji kwa mikusanyiko na nchi kavu kwa mjumuiko, sayari kwa mpishano na mbalamwezi nzuri kwa muonekano, jua letu kwa mtulizano na nyota nyingine nyingi kimrundikano. Katu kwake haikutosha, juu ya ardhi ya kitufe nambari tatu Dunia, chenye anga safi lililotulia na kusheheni hewa murua inayovutia, akatutuliza sisi binadamu na viumbe wengine wengi wenye uhai, wanaotembea na wanaojongea, wanaoogelea na wanaojirukia, lengo lake tutegemeane pasi kusudi lake nyongo kulitia.

Nyuma ya dhamira yake, alitanguliza upendo, ule wa dhati na mzito japo usio na kishindo. Kwa matokeo halisi aliubwaga uhondo huku ubinafsi na tamaa akivisukumia kando. Hatimae, mradi nambari moja wa ulimwengu umesalia juu ya viwango tangu kukamilika na kuzinduliwa kwake. Tangu binadamu wa kwanza mpaka kizazi cha leo cha majungu, kamwe hatujaona wala kushuhudia madhara ya hujuma za mjenzi.

Si dunia kuhama mhimili wake kwa kukosa uimara, si mbalamwezi kutudondokea kisa kani ya mvutano kuongezeka wala sisi kuiacha ardhi na kupotelea angani kisa kupungua kwake, si vimondo kutupiga kwa kukosa uelekeo wala jua kuzimika ghafla na kutuacha gizani kwa kukosa nishati yake ya asili. Ni matokeo ya upendo wa dhati na wa pekee kutoka kwake muasisi, alieyafanya yote kwa utulivu, umahiri na moyo wote asijali jinsi atakavyonufaika na mradi. Furaha yake ni kuona tukidumu upendoni kwenye raha itokanayo na matunda ya upendo wake mkuu huku nasi tukiudumisha na kuurithisha.

Ndugu, kaka, mdogo, mkubwa, rafiki na jamaa yangu, yu nani aliesema wewe si kitu katika kufanikisha jambo muhimu la kimaendeleo katika jamii yako, nchi yako, bara lako na hata dunia yetu ambayo ni yako? Jivue unyonge sasa kwani wewe ni mhimili muhimu ulimwenguni mwenye uwezo mkubwa zaidi ya unavyojifikiria na kujiona.

Kutokuwa na nafasi ama kitengo chenye kubeba mamlaka ya kuamua jambo kupitia wengine walioko chini yako, kutokuwa na kipato kikubwa kuliko wengine ama kukosa nguvu ya ushawishi utokanao na kipaji ama elimu ya kiwango cha juu si sababu za wewe kutobuni, kupanga na kufanya jambo lolote na likawa chachu ya maendeleo, la hasha. Fumba macho yaonayo dosari, ziba masikio yasikioayo propaganda, funika akili ipambanayo na changamoto ikizitafrisi kama matatizo. Mfungulie wewe halisi asieonekana, wewe alie ndani ya kiwiliwili chako kilichokubeba tangu usiku ule ilipotungwa mimba yako. Wewe huyo ni Upendo, upendo alieibeba misingi mikuu chanya ambayo ni Enye nguvu, Enye maarifa na Enye kuweza yote.

Kama mwana halisi na sehemu ya baba yetu muumba(Mkandarasi nambari moja), mwenye kufanana na mwenye sifa kama zake, jione mwenye nguvu katikati ya wajiitao wanyonge, yaruhusu mema mengi zaidi ya mabaya ya wenzio yaziguse mboni za macho na ngoma za masikio yako na kutawala akilini mwako na hatimae kuuzindua mkondo asili wa maarifa na bunifu na kisha zitumie fikra zako kwa hekima ukijenga taswira ya malengo yako chanya kwa wote wakuzungukao na hata viumbe vyote hai na visivyo na uhai ili kuisisimua nguvu halisi iwezayo kila jambo na hatimaye kuzifukuza fikra haribifu za kushindwa. Kwa ari, moyo, msukumo na hamasa ya ndani, fanya jambo lolote liwezalo kuchangia utatuzi wa matatizo ya watu waliokuzunguka bila kujali ukubwa wake huku ukizitanguliza fikra za huduma ziugusao upendo na si zile za faida ziuatamiao ubinafsi.

Chimba mifereji ya kupitisha bomba kwako na kwa majirani kabla ya kudai huduma ya maji, fyatua matofali na kuyachoma kabla ya kudai madarasa kwa wanao, safisha eneo kabla ya kuhitaji kituo cha afya karibu na makazi yako, hamasisha watu kujitokeza kwa wingi kupiga kura zaidi ya kwenda barabarani na mabango kupinga matokeo baada ya kutangazwa. Kwa kufanya hayo na mengine mengi, chemichemi za upendo zivukishazo mvuke wa furaha zitafurika ndani ya moyo wako uliokwishajijengea hali sugu ya kutojidharau na kujishusha na hatimaye kukata tamaa.

Maisha yatakuwa mepesi kuliko kawaida kwani Mkandarasi mkuu kupitia mama yetu Asili atazifanya njia kuwa nyepesi kuelekea mafanikio yako ya viwango vya juu yatakayokujengea furaha halisi isiyokufanya uwe na amani katikati ya wenye huzuni, mwenye chakula tele katikati ya wenye njaa, mwenye kustarehe katikati ya waliao majangani. Wakati wote na mahali popote, utatembea ukijiona suluhisho na mtatuzi wa changamoto za wengine. Hakika, utakuwa na mchango mkubwa katika jamii, nchi, bara na Dunia salama zaidi kuwahi kitokea.

Nanyi vibosile wateule, mashabiki wa suti mliozibeba dhamana nzito na mamlaka ya kuamua na kusimamia hatma ya huduma za kimaendeleo kwenye jamii zetu, zikateni ndimi za uchu na ubaguzi na mzirefushe zile za haki na usawa. Ibunini miradi ya kimaendeleo hata kule pasipo na watoto wa binamu za kaka wa wajomba zenu, fikisheni mafungu yenye uwiano sawa na hesabu za makaratasi yenye sahihi zenu, simamieni utekelezaji kwa utulivu na weredi mkiyazingatia maslahi ya vibarua wanaoishi kwa kula chajio mpaka mwisho wa mradi.

Kuta za madarasa kuwadondokea wanetu kwa upepo wa kisulisuli, madaraja kutitia na gari lililobeba waombolezaji, kituo cha afya kihudumiacho vijiji vitatu kukosa sindano usiku wa manane, mashine ya kuvuta maji kukosa mafuta siku pekee tushindayo nyumbani, hayapaswi kuwa matokeo ya vikao, mipango na michongo yenu muifanyiayo kwenye kumbi za kukodi kwenye hoteli za nyota tano baada ya zile za ofisini kukosa hadhi ya kukutania.

Matokeo bora na imara yatokanayo na nguvu ya upendo kwa watu wote ndio utambulisho mzuri wa ninyi halisi hata baada ya roho kuivua miili yenu nadhifu inayonawili kwa milo mchanganyiko na kupendeza muda wote ikipigwa na kiyoyozi safi ofisini, garini, mgahawani na hata nyumbani, kule kandokando ya fukwe za bahari. Wahudimieni msiowajua, wakarimuni wasiowahi kuwaalika kwenye pikiniki na muwasikilize hata wasiowaomba namba za akaunti zenu masaa machache kabla ya kuihitaji huduma aliyoikosa kabwela juzijuzi.

Kwenye upendo kuna nguvu, kwenye upendo kuna furaha, kwenye upendo kuna amani. Tuudumishe upendo kama nguzo na chachu ya maendeleo ya kweli. Upendo huunganisha, upendo hupatanisha, upendo hufariji. Pasipo kujali asili, kabila, jinsia wala matabaka, tuudumishe upendo, tuyastawishe maisha. UPENDO, KUSUDI LA MAISHA.
 
Back
Top Bottom