Huwa nacheka sana ninapoona Chadema wanavyoichezesha na kuichezea serikali ya CCM. Nacheka zaidi ninapoona jinsi serikali hiyo inavyokiogopa na kukichukulia Chadema kwa makini zaidi. Sasa hivi Serikali haithubutu kukipuuza chama hicho cha upinzani. Kwa mfano wakitamka tu kuandamana, Serikali inaacha shughuli zote na kuelekeza nguvu zake kwenye maandamano hayo. Sasa Chadema ikikohoa tu Serikali inasikiliza kwa makini sana. Hii maana yake ni nini? Inamaanisha kuwa Chadema si chama cha kufanyia mzaha. Kikitamka kitatumia Red Brigade kujilinda, Serikali inatumia vyombo vyake vyote kupiga kelele za kulaani. Kama Chadema inatamka tu kelele za Serikali zinakuwa hivyo, basi siku ikiacha kutamka na kuanza kutekeleza maazimio yake kwa vitendo basi Serikali yote itasimama.
Kama kweli Chadema si chochote wala si lolote, basi wapuuzeni. Mbona CCM na Serikali yake wanababaika kiasi hicho kufuatilia nyendo za Chadema. Kama Chadema ni wapuuzi, basi wapuuzeni. Msiseme kwa midomo tu kuwa ni wapuuzi, wapuuzeni kwa vitendo pia. Sasa nimeanza kuona tishio kubwa la Chadema kwa CCMTisho la wazi kabisa. Siipendi Chadema wala siipendi CCM, lakini nafurahia mchezo wa kisiasa ambao serikali ya CCM inachezewa na Chadema. Yaani Chadema wanaandaa mtego wa kisiasa na Serikali inanasa katika mtego huo.