#COVID19 UNGA: Afrika yaeleza ukosefu wa usawa chanjo za Corona

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Viongozi wa Afrika wameelezea ukosefu wa usawa katika usambazaji wa chanjo za Covid-19, wakati walipohutubia kikao cha 76 cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York.

Katika hotuba yake ya kwanza kwa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema ukosefu wa usawa duniani katika upatikanaji wa chanjo ya COVID-19 ni wa "kutisha", akiongeza kuwa "inakatisha tamaa" kwamba wakati nchi nyingi barani Afrika zimechanja chini ya asilimia mbili ya raia wake, baadhi ya nchi duniani zinakaribia kutoa chanjo ya nyongeza ili kuimarisha zile ambazo tayari zimetolewa.

"Ni muhimu kwamba nchi zilizo na chanjo za ziada za Covid-19 ziweze kuzigawa kwa nchi nyingine", alisema rais Samia. Aidha kiongozi huyo ameeleza kwamba janga la virusi vya corona "linatishia kurejesha nyuma" mafanikio yaliyopatikana katika masuala ya usawa wa kijinsia kwenye taifa lake. Baadhi ya maeneo ambayo yameathiriwa vibaya na janga la Covid-19 katika nchi zinazoendelea ni pamoja na kipato binafsi, elimu na ukatili wa kijinsia. Nchi baada ya nchi zimekiri kwamba tofauti kubwa ya upatikanaji wa chanjo inatoa taswira ya kwamba suluhisho haliwezi kupatikana.

Naye Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby amesema kuwa "nchi ambazo hazijachanja zitakuwa chanzo cha kuibuka kwa aina mpya ya virusi", huku akikaribisha rai iliyotolewa mara kwa mara na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkurugenzi wa shirika la afya ulimwenguni WHO ya kuwezesha upatikanaji wa chanjo kwa wote. Kwa upande wake Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amegusia chanjo kama ulinzi mkubwa zaidi ambao binadamu anao dhidi ya kukabiliana na janga la corona.

"Kwahiyo ni wasiwasi mkubwa kwamba jamii ya kimataifa haijaweza kufanikisha misingi ya mshikamano na ushirikiano katika upatikanaji sawa wa chanjo ya Covid-19".

Rais wa Namibia Hage Geingob ameiita "chanjo ya ubaguzi wa rangi", ikiwa ni kumbukumbu ya uzoefu wa taifa hilo na ubaguzi wa rangi wakati serikali ya makaburu ya nchi jirani ya Afrika Kusini ilipodhibiti Namibia kabla ya kujipatia uhuru mwaka 1990.

Wakuu hao wa nchi za Afrika wamezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuunga mkono pendekezo la muda la kulegeza baadhi ya vipengele vya hakimiliki vilivyoanzishwa na shirika la biashara duniani kuziruhusu nchi zaidi, hususan zile za kipato cha chini na kati kuzalisha chanjo za Covid-19.

Shirika la afya duniani WHO linasema ni asilimia 15 tu ya michango iliyoahidiwa ya chanjo kutoka mataifa tajiri ambayo imetolewa. WHO inataka nchi kutimiza ahadi zake za kugawana dozi "mara moja" ili ziweze kunufaisha nchi masikini.

Siku ya Jumatano, Rais Joe Biden alitangaza kuwa Marekani itaongeza ugavi wake mara mbili wa chanjo ya Pfizer ili kushirikiana na ulimwengu wa dozi bilioni 1, kwa lengo la kuchanja asilimia 70 ya idadi ya watu ulimwenguni mwaka ujao.

Chanzo: DW Swahili
 
Afrika tunalia-lia toka enzi. Huko UN tunachangia ngapi?. Kwann tusitenge bajeti ya kutengeneza chanjo?
 
Back
Top Bottom