Mimi napenda kwanza kukushukuru kwa uchunguzi wako, hali kadhalika kwa kutuletea changamoto hii, ukumbini humu.
Kiswahili kama lugha nyingine yoyote kinakua sambamba na utamaduni wetu unavyokua na kupanuka.
Neno "ahsante" linaashiria kushukuru kwa kuridhika mtu na kile alichofanyiwa. Ni wajibu kwa yule anayeshukuriwa kuitambua shukurani anayopewa kwa kumjibu anayeitoa shukurani hiyo.
Hili la majibu yayotolewa kutokana na jinsia ya mtu, kwangu mimi, halina mtazamo tofauti. Nafikiri tofauti inaletwa na fikra pia mtazamo wa mtu anayeiona hiyo tofauti.
Majibu yote ya "ahsante" uliyoyatoa kama mifano, naona ki-maana, hayana kasoro. Ahsante (kwa) kushukuru, ni kwamba nawe kwa upande wako unampa shukurani kwa kukushukuru.
"Unakaribishwa" au "karibu," unamrahihishia, akiwa na tatizo jingine asisite kukujia kwa msaada.
Uko tayari kumsaidia kwa mara nyingine tena.
"Hakuna/Hamna neno/taabu, Poa(Cool), ni kwamba haikuwa tatizo kwako kumsaidia au kumfanyia ulichomfanyia huyo anayekushukuru.
Yote hayo, kwangu mimi, ni sahihi na sioni sababu ya kimsingi ya kuufanya mwitikio wa "ahsante" uwe wa namna moja tu maalumu au utofautishe jinsia ya anayeshukuru au anayeshukuriwa.