SoC02 Umuhimu wa kuripoti madhara yanayohusishwa kusababishwa na matumizi ya dawa

Stories of Change - 2022 Competition

rizwan gamal

New Member
Jul 9, 2015
1
2
Umuhimu wa kuripoti madhara yanayohusishwa kusababishwa na matumizi ya dawa

Binadamu ni kiumbe anayehitaji afya njema ambayo inajumuisha utimamu wa mwili na akili ili aweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa bila vikwazo. Hivyo basi ikitokea akapata maradhi kwake huwa ni kikwazo na hutafuta tiba iliyosahihi ili aweze kupona. Dawa mbalimbali zimekuwa zikitumika kama tiba kwa maradhi ya binadamu kwa miaka mingi sana na kutokana na utashi ambao binadamu amejaaliwa kiasili ameweza kugundua dawa za maradhi mbalimbali yanayomsumbua hata kabla ya ujio na ukuaji wa tekinolojia.

Dawa nyingi ambazo binadamu amekuwa akizingundua zimetokana na mimea inaweza kuwa mizizi, majani, magome au mbegu za mmea husika au pengine ni mchanganyiko. Kwa miaka mingi tokea uwepo wa binadamu duniani huo ndio umekuwa utaratibu wake wakujitibia mpaka pale teknolojia ilipokua nakuongezeka kwa utaalam wa kisasa wa utengenezaji wa dawa, tafiti mbalimbali za kimaabara kufanyika Pamoja na uzalishaji wa dawa viwandani kuanza kwa mapana yake.

Yote hiyo imeleta ahuweni sana kwa binadamu kwakuwa magonjwa mengi yameweza kupata tiba na kupona kabisa, hata yale yasiyo na dawa ya kuponyesha basi yana dawa ya kuongeza ahuweni kwa mgonjwa mfano dawa za kansa au yana chanjo mfano COVID 19.

Kwa namna ya kisasa ya kutengeneza dawa kuna mchakato mrefu wenye umakini mkubwa na uliyodhibitiwa kikamilifu kuanzia utafiti wa kimaabara, ugunduzi, uzalishaji, usafirishaji na uhifadhi wa dawa kabla na baada ya kumfikia mtumiaji wa mwisho.

Nchini Tanzania mamlaka inayodhibiti dawa ni Mamlaka ya dawa na vifaa tiba Tanzania (TMDA) ili kuhakikisha dawa zinazotumiwa na watanzania zimefikia ubora unaotakiwa. Mamlaka hii imekuwa ikijitahidi kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinazvyotumika nchini viko katika viwango vinavyotakiwa ili kuhakikisha malengo ya watu kupata tiba kwa usahihi yanaweza kufikiwa.

Mtu yeyote atakayetumia dawa ambayo imetolewa kwenye dozi iliyosahihi, kwa mgonjwa sahihi, kwaajili ya ugonjwa sahihi na kwa njia iliyosahihi tunategemea apate nafuu na endapo akipata maudhi yatokanayo na dawa basi apate yale maudhi ambayo yanafahamika kutokana na utafiti wa dawa husika.

Wakati mwingine hali huwa tofauti kwa baadhi ya wagonjwa na mambo huenda tofauti hata baada ya dawa kutolewa kwa usahihi wake wote. Wengine hupata madhara yanayonapelekea kuharibika kwa ogani zao za mwili, mzio usiotarajiwa, mabadiliko ya mifumo ya mwili, ukosefu wa usingizi, kusababisha maradhi mengine na mambo mengine yasiyotarajiwa.

Katika mifumo ya udhibiti wa dawa duniani na Tanzania mambo haya yamewekewa utaratibu utakaosaidia kuyadhibiti na kukusanya taarifa vizuri zaidi kwa utafiti yakinifu wa kisayansi ikiwemo kuondolewa sokoni kwa dawa ambayo itakuwa na madhara makubwa kwa jamii kuliko manufaa yake katika matibabu.

Mfumo huu ulianza kufanya kazi baada ya miaka ya 1960 pale ambapo Dr Widukind Lenze na Dr. William McBride kugundua kuwa mama wajawazito waliyokuwa wakitumia dawa aina ya thalidomide kwa ajili ya kudhibiti maudhi yatokanayo na ujauzito walijifungua Watoto wenye ulemavu wa viungo.

Baada ya utafiti Zaidi kufanyika dawa ile iliwekewa katazo la kutumika kwa wajawazito. Na dawa hiyo imekuwa na historia maarufu kwaathari iliyosababisha kwa watu wengi barani ulaya kwa miaka hiyo. Tokea hapo ikaonekana kuna umuhimu mkubwa wa kufuatilia madhara yanayoweza kuwa yamesababishwa na dawa hata baada ya dawa kukidhi vigezo na kupata usajili wa kuingia sokoni.

Inawezekana dawa ikawa inatumika na kusababisha athari zisizohitajika na zisizokuwepo katika kumbukumbu za utafiti husika hivyo kuripoti athari hizo kama madhara mara tuu zitakazogundulika ni muhimu sana ili ziweze kutambulika na kupimwa madhara yake ukifananisha na umuhimu wa matibabu ya dawa hiyo. Jamii yote kwa ujumla wetu tunayo dhima ya kuhakikisha tunaripoti madhara yanayoonekana kutokea baada ya matumizi ya dawa iwe ni yale yanayooneka kuwa madogo au makubwa.

Mamlaka inayohusika na kukusanya taarifa hizi za madhara baada ya matumizi ya dawa ni Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA). TMDA imeweka utaratibu mzuri wakuhakikisha taarifa zinazoripotiwa na kuzikusanya kupitia idara yao ya kukusanya taarifa za madhara yasiyotarajiwa yanayohusishwa na utumiaji wa dawa. Kumekuwa na changamoto ya TMDA kupokea ripoti chache hiyo ni kwasababu wengi wetu huwa haturipoti madhara haya iwe kwa kujua au kwakutokujua.

Moja ya jambo muhimu la kuzingatia wakati wa kuripoti ni kuripoti madhara yaliyotokea baada ya dawa kutumika. Vilevile kuripoti jina la dawa husika inayohisiwa kusababisha madhara hayo, bila kusahau umri wa mgonjwa na aina ya madhara aliyopata, tarehe dawa lipoanza kutumika na tarehe ya madhara yalipoanza. Itapendeza Zaidi ukiweka na mawasiliano ili mamlaka iweze kuwasiliana nawe kama itahitaji taarifa Zaidi kuhusu madhara yaliyotokea.

Ni wakati sasa, sisi kama jamii kushiriki kikamilifu kutoa ripoti hizi kwa mifumo iliyopo ili kuisaidia mamlaka iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi na sisi tuweze kupata tiba bora Zaidi. Tunaweza kuripoti kwa kutumia fomu za njano zitolewazo na TMDA katika vituo vya afya nchini ili kuripoti madhara yatokanayo na dawa.

Vilevile tunaweza kuripoti popote tulipo kwakutumia simu janja za Aneroid kupitia aplikesheni yao inayojulikana kama (TMDA reporting tool) au kwa kutumia simu zisizo janja kwa kupiga *152*00 na kisha kufuata maelekezo. Kupitia kuripoti haya madhara tutakuwa tumeshiriki vyema kudhibiti ubora wa dawa tuzitumiazo nchini kwetu.
 
Back
Top Bottom