[h=2]Mwanzo 1[/h]
[h=3]Kuumbwa ulimwengu[/h][SUP]1[/SUP]Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia.[SUP]2[/SUP]Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji.
[SUP]3[/SUP]Mungu akasema, Mwanga uwe. Mwanga ukawa. [SUP]4[/SUP]Mungu akauona mwanga kuwa ni mwema. Kisha Mungu akautenganisha mwanga na giza, [SUP]5[/SUP]mwanga akauita Mchana na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya kwanza.
[SUP]6[/SUP]Mungu akasema, Anga liwe katikati ya maji, liyatenge maji sehemu mbili.[SUP]7[/SUP]Mungu akalifanya anga, akayatenga maji yaliyo juu ya anga na yale yaliyo chini ya anga hilo. Ikawa hivyo. [SUP]8[/SUP]Mungu akaliita anga Mbingu. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya pili.
[SUP]9[/SUP]Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, nchi kavu itokee. Ikawa hivyo. [SUP]10[/SUP]Mungu akapaita mahali pakavu Nchi na kusanyiko la maji akaliita Bahari. Mungu akaona kuwa ni vyema.
[SUP]11[/SUP]Kisha Mungu akasema, Nchi na ioteshe mimea. Mimea izaayo mbegu, na miti izaayo matunda yenye mbegu. Ikawa hivyo. [SUP]12[/SUP]Basi, nchi ikaotesha mimea izaayo mbegu kwa jinsi yake, na miti izaayo matunda yenye mbegu kwa jinsi yake. Mungu akaona kuwa ni vyema. [SUP]13[/SUP]Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tatu.
[SUP]14[/SUP]Mungu akasema, Mianga na iweko angani, itenge mchana na usiku, ioneshe nyakati, majira, siku na miaka, [SUP]15[/SUP]na ingae angani na kuiangazia dunia. Ikawa hivyo.[SUP]16[/SUP]Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. [SUP]17[/SUP]Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia, [SUP]18[/SUP]ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema. [SUP]19[/SUP]Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne.
[SUP]20[/SUP]Mungu akasema, Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.[SUP]21[/SUP]Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema. [SUP]22[/SUP]Mungu akavibariki, akasema, Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi. [SUP]23[/SUP]Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano.
[SUP]24[/SUP]Mungu akasema, Nchi na itoe aina zote za viumbe hai, wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini wa kila aina. Ikawa hivyo. [SUP]25[/SUP]Basi, Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa, na viumbe vitambaavyo. Mungu akaona kuwa ni vyema.
[SUP]26[/SUP]Kisha Mungu akasema, Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo. [SUP]27[/SUP] Basi, Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba. Aliwaumba mwanamume na mwanamke. [SUP]28[/SUP]Mungu akawabariki na kuwaambia, Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki; muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho duniani.
[SUP]29[/SUP]Kisha Mungu akasema, Tazama, nawapeni kila mmea duniani uzaao mbegu, na kila mti uzaao matunda yenye mbegu; mbegu zao au matunda yao yatakuwa chakula chenu. [SUP]30[/SUP]Nao wanyama wote duniani, ndege wote wa angani, viumbe vyote vitambaavyo, naam, kila kiumbe chenye uhai, chakula chao kitakuwa majani yote ya mimea. Ikawa hivyo. [SUP]31[/SUP]Mungu akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema kabisa. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya sita.