Umenasa kwenye mtego kwa sababu umejichanganya

Apr 19, 2018
83
112
trapped.PNG


Kuna wakati unahisi mambo hayaendi, hasa katika masuala ya fedha na kipato. Unaona unapambana kwa bidii lakini maendeleo ni kama vile hayaonekani.

Unahisi umerogwa siyo?

NATAKA kukwambia UKWELI kwamba ni kweli kuna mtu anakuchezea, lakini mtu huyo si mwingine, bali ni wewe mwenyewe.

Najua unachotaka kusema;

WEWE; “Haiwezekani, mimi ninachapa kazi kweli kweli, kazini sichelewi wala siyo mvivu”.

MIMI; Uko sahihi, na hilo haswaa ndiyo tatizo!
Kuwa na bidii,
Kuchapa kazi!

WEWE; “Unataka kuniambia bidii yangu ndo inasababisha nikwame kimaendeleo na kupitia changamoto za uchumi ninazopitia?”

MIMI; mmmmmh! Kwa namna fulani; ndiyo! lakini hautanielewa kwa mtazamo ulionao sasa. Mtazamo ulionao ni kwamba “kufanya kazi kwa bidii, ndiyo kutapelekea maendeleo kwenye maisha yako”.
Ninaomba usahau hilo kwa muda, Kisha uniazime umakini wako kama vile mtoto mdogo anayetaka kujifunza kitu kwa mara ya kwanza.
Dhana ya 'Fanya kazi kwa bidii' bado haijakamilika, kwa sababu haijibu maswali ya msingi sana ya kifedha na maendeleo. Kama vile, ‘Kwa nini ninafanya kazi?’, au ‘Kuna ulazima wa mimi kufanya kazi ninayoifanya saizi’ au ‘Kwani siwezi kufanya kitu kingine na kulipwa mara mbili au mara tatu ya ninachokipata kwenye kazi hii?’ na maswali mengineyo ya msingi.

Maswali ya msingi ambayo wengi wetu ni vigumu kujiuliza,
Ndiyo maana na wewe umeingia uwanjani kucheza mpira, bila kuzifahamu kanuni zote za mchezo. Umejiamini kwa kuwa unajivunia kanuni moja tu! ‘Bidii’ na yule pacha wake anayeitwa 'Uaminifu'. Ndiyo maana kila ukijaribu kufunga magoli ya ushindi wa kujikwamua kiuchumi, Refa-Umaskini na Uhitaji anapuliza kipyenga na kukupiga faulo.

Kadi za njano ulizopigwa(michongo mingi kufeli) ni nyingi hazihesabiki, Hata ukijaribu kubadilisha uwanja wa mchezo(kubadili kazi au biashara), bado matokeo ni yale yale kwa sababu kilichojaa katikati ya sikio lako la kulia na sikio lako la kushoto ni kile kile na hauna mpango wa kukibadili.

WEWE; “Kama nimeanza kukupata hivi kwa mbali, unadhani ni wapi nitakuwa nimejichanganya?”

MIMI; Anzia hapa katikati ya sikio lako la kulia na la kushoto, pana kitu kinaitwa ubongo. Hivi unajua hicho ndiyo chombo chako cha kusafiria katika ulimwengu wa mafanikio hasa ya kiuchumi?. Nikikuuliza mara ya mwisho kukifanyia service ni lini, unalo jibu?

Tangu umalize shule eti?

Tangu wakupe lile gamba lako lenye mabanda?

Ni nani alikwambia gari unalifanyia service mara moja halafu unakaa tu?

Unategemea mambo mengi ya maisha yataende wakati chombo unachotumia kusafiria ni kibovu kimekaa bila service kwa miaka mingi?

UMEJICHANGANYA; Kama mara ya mwisho kujifunza jambo jipya ni pale ulipotunukiwa kile cheti kilichopo ukutani, basi sasa, spea nyingi sana zilizoko kwenye ubongo wako zilishachakaa. Ndiyo maana zinapiga kelele, kwa maana kwamba; kutatua matatizo mengi unatumia kelele nyingi, na hazikupeleki popote.

SASA; Angalau kila mwezi, Ujifunze jambo jipya linalokusogeza taratibu kwenye ndoto zako na mipango yako, kisha lifanyie kazi.

MIMI; Nisije nikakumezesha chakula kingi kikawa na madhara, kafanyie kazi suala hili moja, halafu nitarudi kukuonesha wapi pengine ulipojichanganya. Ili turekebishane mdogo mdogo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom