Mkurugenzi wa Tanesco abanwa ajiuzulu kwa kashfa ya Dowans
Na Geofrey Nyang'oro
SIKU moja baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kutangaza kususa ununuzi wa mitambo ya Dowans, wasomi, wanasiasa na wananchi nchini wamezidi kumkaba koo Mkurugenzi wa shirika hilo, Dk Idrisa Rashid ajiuzulu.
Watu hao wanataka, Dk Raishid ajiuzulu kutokana na kauli yake ya kueleza kuwa kwa vile watu wengi hawataki mshirika lake linunue mitambo ya Dowans basi asilaumiwe kama nchi itakuwa giza.
Sambamba na hali, Rais Jakaya Kikwete ametakiwa kumwonfdoa katika wadhifa wake Waziri wa Nishati na Madini, Wiliiam Ngeleja na kuvunja menejimenti nzima ya Tanesco.
Maneno yaliyomweka pabaya Dk Rashid aliyasema juzi katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa Shirika lake, likisema lisibebeshwe lawama kwa yatakayotokea.
Alisema wananchi wa Tanzania watafanya maamuzi yao hapo ambapo nchi itakapokuwa imegubikwa na kiza, mahospitali hayatoi huduma; viwanda havizalishi, wanafunzi vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu ya kushindwa kufanya maamuzi.
Uamuzi wake huo umekuja siku mbili baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta kueleza kuwa msimamo wa kamati ya Nishati na Madini iliyoshauri mitambo hiyo isinunuliwe ndio msimamo wa chombo hicho cha kutunga sheria na hivyo kumaliza mvutano uliokuwepo kati ya kamati hiyo na ile ya hesabu za mashirika ya umma, inayoongozwa na Zitto Kabwe iliyounga mkono kununuliwa kwa mitambo.
Mtaalamu wa Ugonjwa ya Ukimwi, Dk Fedelis Owenya aliliambia Mwananchi Jumapili jana kwa njia ya simu kuwa kauli ya Dk Rashid inaonyesha jinsi gani kiongozi huyo aliyeteuliwa kumsaidia rais ameshindwa kufanya kazi yake.
Alisema Dk Rashid amekiuka misingi ya kazi yake ambayo ilikuwa ni kuandaa mipango ya muda mufupi na muda mrefu ya upatikanaji wa umeme na kuishauri serikali, badala yake sasa ameamua kushinikiza kununuliwa kwa mitambo hiyo na kutoa vitisho kwa wanachi na rais wake.
Kauli kwamba anawaachia wananchi kuamua wenyewe pindi nchi itakapokuwa kuwa giza ni vitisho vinavyoitaka serikali kuvunja hata sheria ya manunuzi, kitu ambacho kinaonyesha kuwa kuna nguvu nyuma yake.
Alisema hatua aliyoichukua Mkurugenzi huyo inaonyesha kuwa hujuma nzinaweza kufanywa ili kukomoa wananchi, hivyo, hatua zaidi zinafaa kuchukuliwa dhidi yake.
"Hii ni nchi ya kidemokrasia,sisi tumemchagua rais na tumempa dhana ya kutuongoza,yeye kwa nafasi yake amewachagua watu watakaomsaidia katika suala zima la utendaji ili nchi iweze kuendelea,Dk Rahidi aliyeteuliwa na rais kushika nafasi hiyo, anawatishia wanchi au anamtishia rais aliyempa nafasi hiyo?alihoji Dk Owenye na kutongeza kuwa watu wa aina hii wanapaswa kushitakiwa.
Owenya aliiasa Serikali kufanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na sheria ya ununuzi wa umma ili kutunza na kuendeleza heshima na usitawi wa nchi na jamii yake.
Kwa upenda wake, Tundu Lisu ambaye ni mwanasheria licha ya kumtaka Dk Rashid awajibishwe pi alipendekeza uwepo uwajibikaji kisiasa na kuwataka waliomteua wawajibishwe pia.
Hayo aliyezesema juzi alipokuwa akichangia kwenye kipindi cha Kipamajoto kinachorushwa hewani na Kituo cha Television cha ITV.
Alisema kitendo cha kulazimisha ununuzi wa mitambo hiyo wakati akijua kuwa ni mitumba ni kuwatukana watanzania.
Lisu alipinga kuwepo kwa dhararu ndani ya shirika hilo na kueleza kuwa ni uharamia ulipangwa kufanyika ndani ya shirika hilo kwa kuwa wao walijua tangu siku nyingi.
Alisema kimsingi kampuni hiyo inapaswa kufikishwa mahakamani kutokana na mkataba wake kuwa tata anashangaa kuona mpaka sasa suala hilo halijafanyika.
Katika hatua nyingine mwanaharakati, Renatus Mpinga alimtaka rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Mkurugenzi huyo haraka kwa kuwa ameonyesha utovu wa nidhamu mbele ya watanzania.
Alisema kitendo chake cha kulazimisha ununuzi wa mitambo hiyo kinataka kutonyesha kuwa mitambo hiyo ndiyo bora kuliko mengine.
Naye Mtaalamu wa sheria ya Manunuzi ya Umma, Wasonga Benjemani alisema sheria ya manunuzi inaeleza wazi kuwa mzabuni akionyesha dalala za kutumia rushwa katika kupata tenda yake anatakiwa kusimamishwa kushiriki katika kufanya biashara ya serikali kwa muda wa miaka kumi au kufikishwa mahakamani.
Alisema kitendo cha Taneseco kunuia kununua mitambo hiyo iliyozua mashaka hapa nchini ulikuwa ni ukiukwaji wa wazi wa sheria zilizopo.
Naye Joyce Mmasi anaripoti Mbunge wa Vunjo Aloyce Kimaro amesema watu watakao liingiza taifa katika ununuzi wa mitambo ya Dowans washitakiwe na kufungwa jela.
Ule wakati wa kukosea na kujiuzulu umepitwa na wakati, sasa hivi ni mahakamani kwa wote waovu, wazembe na wanaotumia madaraka yao vibaya, sasa ni kufungwa sio kujiuzulu, alisema.
Alisema serikali iache kutumia baadhi ya wabunge kuhalalisha uzembe. Tujiulize hivi huku Tanesco kuna nini hadi kutaka kuvunja sheria? Haiwezekani kampuni ambazo zilizoifanya serikali nzima kujiuzulu leo tunaendelea kuzifuata, alisema Kimaro.
Kimaro alisema anashangazwa na kitendo cha mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya kusimamia hesabu za mashirika ya umma alivyolikomalia suala hilo.
Naye Burhani Yakub,Tanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Dk Idriss Rashid,amelalamikiwa kwa kauli aliyotoa wakati akijiondoa katika ununuzi wa mitambo ya Dowans Tanzania Limited ya kuwa ikiwa nchi itakuwa giza asilaumiwe.
Wananci waliohojiwa nya kati tofauti jijini hapa jana , wamesema kauli hiyo haikupaswa kutolewa na kiongozi kama yeye kwa kuwa inatoa mwanya kwa watumishi wasiokuwa na uaminifu wa Tanesco kufanya hujuma.
Malalamiko hayo waliyatoa jana kwa nyakati tofauti wakati wakielezea maoni yao juu ya kauli ya Dk Rashidi aliyotoa kwa waandishi wa habari kuelezea kujito kwa Tanesco katika ununuzi wa mitambo ya Dowans.
"Asitufanye wananchi ni wajinga,inakuwaje wang'ang'anie kununua mitambo ya Dowans ilhali wanafahamu kuwa ni mikongwe?halafu anaamua kususa baada ya Kamti ya Bunge ya Nishati na madini kuweka msimamo wake"alisema Khamisi Ali mkazi wa Makorora Jijini Tanga.
Mustafa Shembeyu wa Barabara ya 15 Jijini Tanga,alisema kauli iliyotolewa na Dk Idriss inaonyesha kuwa ameshindwa kuliendesha shirika la Tanesco hivyo anastahili kujuzulu ili kuepusha madhara kama ataendelea kuwepo.
"Ili kuinusuru Tanesco inabidi Dk Idriss ajiuzulu,kwani kwa kauli yake inaonyesha kuwa mwisho wake wa kushauri umefikia kwa Kampuni ya Dowans na kwamba hana njia nyingine ya kuweza kutafuta ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini"alisema Sembeyu.
Kiongozi wa umoja wa vyama vya upinzani Wilaya ya Korogwe,Calistus Shekibaha,alisema baada ya kusikia kuwa Rais Jakaya Kikwete amemteua Dk Idriss kushika wadhifa huo alipata wasiwasi kwa kuwa ndiye anayeshutumiwa kuivuruga hata benki ya NBC.
"Kwa wale wenye mazoea ya kusoma magazeti watakumbuka mara baada ya uteuzi wa Idriss nilitoa maoni yangu katika gazeti la Mwananchi na kumwambia Rais atavuna machungu kwa kitendo chake cha kumteua Dk Idriss kuongoza Shirika nyeti kama Tanesco.
Alisema wakati Dk Idriss akiwa NBC watumishi walimlalamikia kuwa alikuwa akiendesha benki hiyo kimabavu na kusababisha mabo mengi kuharibika jambo lililosababisha wamkumbe Mkurugenzi wao wa zamani Amon Nsekela.
Shekibaha aliipongeza Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli,William Shelukindo kwa msimamo walioonyesha katika kutetea mitambo ya Dowans isinunuliwe.
Aliitaka Serikali kutafuta mbinu za ununuzi wa mitambo mipya ili kumaliza kabisa tatizo lililopo kwani ni jambo la iabu kwa nchi ya Tanzania kuhangaikia umeme wakati ina vyanzo vingi.