Uliniua Gloria

*Sehemu ya 04*


Peter hakuonekana kufahamu kitu chochote kile ambacho kilikuwa kikiendelea nyuma ya pazia, hakujua kwamba rafiki yake, Kaposhoo alikuwa akitembea na mpenzi wake, Gloria, msichana ambaye alikuwa akitarajia kumuoa katika kipindi kichache kijasho. Kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea kwake alikichukulia kawaida sana.

Maisha yaliendelea kusonga mbele kama, Peter aliendelea kupigwa upofu katika kila kilichokuwa kikiendelea katika maisha ya Gloria. Hata Kaposhoo aliposema kwamba alikuwa akibaki nyumbani kwa kuwa hakuwa akijisikia vizuri, Peter hakuonekana kuwa na wasiwasi hata kidogo.

Uaminifu wake alikuwa ameuweka kwa Gloria kupita kawaida, ilikuwa radhi aambiwe kitu chochote kile lakini si kuambiwa kwamba Gloria alikuwa akimsaliti. Uaminifu wake kwa Gloria ulikuwa mkubwa kupita kawaida, alimuamini zaidi ya mtu yeyote yule katika maisha yake..

Gloria hakuonekana kujihukumu moyoni mwake, alikuwa akiendelea zaidi kutembea na Kaposhoo ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi hata mara moja.

Katika kipindi ambacho Gloria aliendelea kubaki nyumbani hapo ndicho kilikuwa kipindi ambacho Kaposhoo akatoa wazo moja ambalo lilionekana kuwa zuri sana, wazo ambalo lingeendelea kumuwekea upofu Peter kwa kutokujua kile kilichokuwa kikiendelea.

“Ndiyo hivyo. Msichana kukaa nyumbani tu si kitu kizuri, mtu kama huyu inabidi atafutiwe kazi na kuanza kuelekea kazini kwa ajili ya kujiingizia kipato” Kaposhoo alimwambia Peter ambaye alikuwa makini kumsikiliza.

“Hilo ni wazo zuri sana lakini tatizo sijui nitaanzia wapi kumtafutia kazi hiyo, sijawa mwenyeji sana hapa Zambia” Peter alimwambia kaposhoo.
“Hilo si tatizo, suala hapa ni kumuuliza yeye alikuwa akihitaji kazi gani” Kaposhoo alimwambia peter.

Gloria akaitwa mahali hapo na kuulizwa kazi ambayo alikuwa akiihitaji. Kaposhoo hakuonekana kuwa na wasiwasi hata mara moja, kitu ambacho alikuwa akikiamini ni kwamba kazi yoyote ile ambayo Gloria angeichagua kwake lisingekuwa tatizo kuipata.

Fedha za baba yake zilimfanya kujiamini kupita kawaida, umaarufu wa baba yake nchini Zambia ukaonekana kuwa mkubwa kiasi ambacho kusingekuwa na mtu yeyote yule ambaye angeweza kusema kitu chochote kile kwake.

Ukiachana na hilo, heshima kubwa ambayo alikuwa ameitengeneza baba yake nchini Zambia ilikuwa ikimpa kiburi sana jambo ambalo aliamini kwa asilimia mia moja angefanikisha suala zima la Gloria kufanya kazi katika kampuni yoyote ile.

“Kazi yoyote tu ambayo itanifanya kuondoka mahali hapa kila nyakati za asubuhi” Gloria alimwambia Kaposhoo.
“Unaweza kuwa mhudumu wa hoteli, wa kukaa pale mapokezini?” Kaposhoo alimuuliza Gloria.

“Ila sijasomea”
“Hilo si tatizo. Bila kusomea, unaingia popote unapopataka, kila kitu kipo chini yangu. Utaweza?” Kaposhoo alimwambia Gloria na kumuuliza.

“Hakuna tatizo” Gloria alimjibu.
Kwa Kaposhoo, jambo lile likaonekana kuwa dogo sana ambalo wala halikuweza kumsumbua kichwani mwake Alichokifanya ni kuanza kujifikiria ni hoteli gani ambayo ilikuwa nzuri zaidi nchini Zambia kwa ajili ya kumpeleka Gloria kuanza kazi, kwake akaiona hoteli ya Paradise 5 ambayo ilikuwa pembezoni mwa jiji la Lusaka.

Kitu alichokifanya Kaposhoo ni kuwasiliana na baba yake, Bwana Charles Mbwana ambaye akalichukulia uzito suala hilo na kisha kuanza kuwasiliana na meneja wa hoteli hiyo kubwa na ya kitalii, Bwana Stewart Paul.

Kutokana na heshima walizokuwa wakiwekeana wawili hao, Bwana Stewart hakuonekana kupinga, alichokitaka yeye ni kuonana na Gloria tu kwa ajili ya mahojiano kadhaa kabla ya kuanza kufanya kazi.

“Niliwaambia, hili si tatizo hasa kwangu mimi” Kaposhoo aliwaambia huku akionekana kuwa na furaha.

“Mbona mambo yamekwenda kirahisi namna hii?” Peter aliuliza huku akionekana kushangaa.

“Mjini hapa, wenye fedha ndio wanaopata vile wanavyovitaka” Kaposhoo alimwambia Peter huku akionekana kuwa na furaha.

“Nashukuru sana Kaposhoo...nashukuru sana rafiki yangu” Gloria alimwambia Kaposhoo.
“Usijali Gloria” Kaposhoo alimwambia Gloria.

Kila kitu kilichokuwa kikiendelea machoni mwa Peter kilionekana kuwa msaada mkubwa kwa mpenzi wake kumbe ukweli ni kwamba ule ulikuwa mchezo mkali ambao ulitakiwa kumpoteza kabisa na hatimae aweze kuachana na Gloria na Kaposhoo amchukue jumla jumla.

Siku iliyofuata ilikuwa siku ambayo Kaposhoo na Peter walikuwa na jukumu la kumpeleka hotelini.

Ndani ya gari, Kaposhoo na Gloria walikuwa wakiangaliana kwa macho ya wizi huku wakionekana kuwa na kitu ambacho kilikuwa kinaendelea kati yao.

Uwepo wa Peter ndani ya gari lile ukaonekana kuwanyima kufanya mambo fulani ambayo walitakiwa kufanya kama wapenzi.

Peter alikuwa amekwishaondoka ndani ya moyo wa Gloria na nafasi yake kuchukuliwa na kijana mwenye pesa, Kaposhoo.

Safari ile iliendelea zaidi mpaka walipofika katika eneo la hoteli ya Paradise 5 ambapo wakateremka na moja kwa moja kuelekea katika jengo la hoteli hiyo na kutaka kuonana na meneja ambapo wakaelekezwa katika ofisi aliyokuwepo.

Bwana Stewart ambaye ndiye alikuwa meneja wa hoteli ile akawakaribisha na kisha kuanza kuongea nao.

Wala hakukuonekana kuwa na tatizo lolote lile kwani Bwana Mbwana alikuwa amekwishaongea ne kila kitu.
“Karibu sana” Bwana Stewart alimkaribisha Gloria huku akimshka mkono.

“Asante sana”
Hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza kwa Gloria kuingia ndani ya hoteli ile kubwa ya kitalii, hakuamini kama kweli alikuwa akienda kuanza kazi ndani ya hoteli ile ambayo ilikuwa na jina kubwa nchini Zambia.

Peter akashindwa kuvumilia, kila siku akawa mtu wa kumshukuru Kaposhoo kwa kile alichokuwa amekifanya bila kugundua mchezo mchafu ambao ulikuwa ukichezwa nyuma ya pazia.

Mahusiano hayakukatika, japokuwa kila siku Gloria alikuwa akishinda hotelini lakini Kaposhoo alikuwa akiendelea kujiachia nae kama kawaida kiasi ambacho wafanyakazi wote wa hotelini wakajua kwamba Gloria alikuwa msichana wa Kaposhoo na si Peter kama ilivyokuwa.
****
Jina la Stewart Paul lilikuwa ni miongoni mwa majina ya watu waliokuwa wakijulikana kuwa na fedha sana katika nchi ya Zambia.

Mzee huyo aliyekuwa na miaka hamsini na mbili alikuwa akijulikana zaidi kutokana na kumiliki hoteli kadhaa zilizokuwa zikiitwa Paradise 5 ambazo zilikuwa zikipatikana nchini Zambia, Zimbabwe na mbili ambazo zilikuwa zikijengwa nchini Tanzania katika mkoa wa Arusha na Dar es Salaam.

Katika kipindi chote alichokuwa akikaa Zambia, Bwana Stewart hakutaka kumpa mtu nafasi ya umeneja, alijua fika kwamba alikuwa mkurugenzi lakini kutokana na kutokuamini mtu yeyote hasa katika mali zake, akajipa vyeo hivyo viwili, vyeo ambavyo vilimfanya muda mwingi sana kuwa bize.

Bwana Stewart alikuwa mtu wa watu, alikuwa akipenda kumsikiliza kila mtu ambaye alikuwa na shida iliyokuwa ikihitaji fedha, hakuzichungulia fedha zake, kila mtu ambaye alikuwa akihitaji msaada, alikuwa akimpatia bila maswali yoyote yale.

Jambo hilo likawafanya watu wengi kumpenda na kumthamini kutokana na mchango ambao alikuwa akiutoa kwa wananchi ambao walionekana kuwa na njaa kali nchini Zambia.

Serikali ilimuona Bwana Stewart kuwa mtu wa maana sana, mtu ambaye alikuwa akihitajika katika kila jamii ya watu katika Bara la Afrika, mali zake pamoja na fedha zake hakula peke yake, alikuwa akipenda kutumia na watu ambao walikuwa katika umasikini mkubwa.

Hoteli za Paradise 5 ndizo zilikuwa hoteli pekee zilizokuwa zikitoa vyakula kwa watu wasiokuwa na vyakula katika siku ya Ijumaa na Jumapili jambo ambalo liliwafanya watu wengi masikini kuendelea kumshukuru kila sku.

Katika maisha yake yote, alikuwa akiwathamini sana masikini, aliyajua vilivyo maisha ambayo walikuwa wakipitia watu masikini, alikuwa akiyafahamu vilivyo maumivu waliyokuwa nao masikini kutokana na yeye kupitia maisha hayo.

Aliuchukia umasikini, hakupenda kuwaona watu wakiwa masikini, wakilala bila chakula au wakiwa na uhitaji wa fedha. Katika kila pumzi ambayo alikuwa akivuta, alikuwa akiwafikiria masikini ambao bado walikuwa wakiendelea kuhitaji msaada kutoka kwake.

Bwana Stewart hakuwaacha, aliendelea kuwajali na kuwasaidia kama kawaida yake.
Kupitia misaada mbalimbali ambayo alikuwa akiitoa bila majivuno yoyote yale, Bwana Stewart akajikuta akipata fedha zaidi, baraka za Mungu zikaonekana kumjalia katika maisha yake.

Mipango yake mingi ambayo ilikuwa haikamiliki ikakamilika kama alivyokuwa akitaka.
“Wenye matatizo wanahitaji kusaidiwa, haitakiwi chakula kimwagwe hata mara moja. Hata hayo unayoyaona kwamba ni makombo, wape wasiokuwa na vyakula nao watayaona kuwa chakula bora kwao” Bwana Stewart aliwaambia wafanyakazi wake na kuendelea:

“Unapomwaga chakula, unapata laana. Wewe unakimwaga na wengine wanakitafuta. Mteja akibakisha chakula, kiwekeni, kipasheni moto, mkiona mtu mwenye shida na chakula anapita, muiteni aje ale kuliko kwenda kukimwaga” Bwana Stewart aliendelea kuwaambia wafanyakazi wake.

Katika mambo yote, hakupenda kuona chakula kikimwagwa jalalani na wakati kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa wakihitaji chakula, kila siku akawa mtu wa kuwasisitizia wafanyakazi wake kwamba ilikuwa ni lazima kuwagawia vyakula watu ambao walikuwa na shida mbalimbali na si kuvimwaga kama walivyokuwa wakifanya wafanyakazi wa hoteli nyingine.

Japokuwa alikuwa akisaidia watu wengi, japokuwa alionekana kuwa mtu muhimu katika jamii ya watu wa zambia lakini Bwana Stewart alikuwa na ulevi mmoja maishani mwake, wanawake.

Bwana Stewart alikuwa mtu wa wanawake sana, katika maisha yake hakuwa mtu wa kunywa pombe wala kuvuta sigara, vitu hivyo viwili alikuwa amepigana navyo sana na kuvishinda lakini katika suala la wanawake, alikuwa ameshindwa kabisa kupigana nalo.

Kila siku alikuwa mtu wa kutembea na wanawake mbalimbali, kila siku akawa mtu wa kuwahonga wanawake mbalimbali na kulala nao kama kawaida. Nyumbani alikuwa na mke pamoja na watoto watatu lakini suala la wanawake kwake wala halikuisha.

Kila mwanamke mzuri ambaye alikuwa akipita mbele yake alikuwa anahakikisha analala nae kama kawaida.
Kutokana na fedha ambazo alikuwa nazo, wanawake walikuwa wakimpapatikia sana, kila siku walikuwa wakimfuata hotelini, aliwapa fedha na kuendelea na mchezo wake kama kawaida.

Mke wake, Bi Hilda alikuwa ameongea sana lakini Bwana Stewart hakuonekana kubadilika hata mara moja.

“Wanawake...aisee siwezi kuwaacha. Ni bora uninyime chochote kile maishani mwangu lakini si kuacha kutembea na wanawake wazuri” Bwana Stewart alimwambia tajiri mwenzake, baba yake na Kaposhoo, Bwana Mbwana.

“Hilo ndio la muhimu, unapokuwa na fedha lazima uwe na wanawake wengi hasa sisi kwa wazee ambao ujanani mwetu wazee wetu walikuwa wakituchunga sana” Bwana Mbwana alimwambia Bwana Stewart.

Hiyo ilionekana kuwa kama kazi yao, wawili hao walikuwa wakipenda wanawake kupita kawaida. Hawakujali wanawake wa aina gani, wale wembamba, wanene, warefu kwa wafupi walikuwa wakilala nao kama kawaida. Kwa hapo hotelini, kwa kila msichana ambaye alikuwa akitaka kuanza kazi katika hoteli ile ilikuwa ni lazima alale nae na kisha kumpa kazi katika hoteli hiyo.

Katika siku ambayo aliambiwa na Bwana Mbwana kwamba kijana wake, Kaposhoo alikuwa akimleta msichana wake kwa ajili ya kufanya kazi katika hoteli hiyo, Bwana Stewart wala hakuwa na uso wa tamaa, alichokuwa akikijua ni kwamba msichana huyo alikuwa ni wa kawaida tu, hivyo wala asingeweza kufanya jambo lolote lile kwani hakutaka kugombani mwanamke na mtu ambaye alionekana kuwa kama mtoto wake, Kaposhoo kisa mwanamke.

Katika kipindi ambacho Gloria alikuwa ameingia mahali hapo, Bwana Stewart akaonekana kutokwa na kijasho chembamba, hakuamini kama macho yake yalikuwa yamemuona msichana mzuri kama alivyokuwa Gloria, kila alipokuwa akimwangalia, aliona ni bora kugombana na Kaposhoo lakini si kumuacha msichana huyo apite katika mikono yake.

Hakuonyesha kipingamizi, tena kwa sababu Gloria alikuwa akihitaji kazi kwa udi na uvumba, akampa kazi na cheo juu cha kuwa msimamizi wa mambo ya usafi ndani ya hoteli ile.

Suala lile likaonekana kuwashangaza wafanyakazi wengine lakini wakawa wamekwishajua kulikuwa na kitu gani ambacho kiliendelea moyoni mwa Bwana Stewart, wakakubaliana nae.

Katika kipindi chote hicho, Bwana Stwewart alikuwa akimwangalia Gloria tu, umbo lake pamoja na sura yake ya kitoto vilikuwa vitu ambavyo vilimchanganya sana jambo ambalo lilimpelekea kujiapiza kwamba piga ua ilikuwa ni lazima kutembea na msichana Gloria.

Katika siku ya kuandika mkataba wa kufanya kazi ndani ya hoteli hiyo, mshahara wa Gloria ulikuwa ni mara mbili zaidi ya mishahara ya wafanyakazi wengine ndani ya hoteli ile. Gloria hakujua kama alikuwa amepewa ofa kubwa ya mshahara mpaka pale alipoambiwa na mzee huyo.

“Huu mshahara ni mara mbili juu zaidi ya mishahara ya wafanyakazi wengine” Bwana Stewart alimwambia Gloria katika kipindi ambacho alikuwa akisaini mkataba ndani ya ofisi yake.

“Asante sana. Ila kwa nini umeamua kufanya hivyo?” Gloria aliuliza huku akionekana kushangaa.
“Kwa muonekano tu, unaonekana kuwa msichana muaminifu sana kuliko wafanyakazi wa hapa.

Ukifanya kazi kwa kuniridhisha zaidi, utakuwa sekretari wangu, huyo mwingine nitampeleka sehemu nyingine na mshahara wako utakuwa juu zaidi” Bwana Stewart alimwambia Gloria ambaye alionekana kuwa na furaha zaidi.

“Asante sana” Gloria alimwambia Bwana Stewart ambaye akasimama kutoka kitini.

“Usijali. Unajua unapokuwa na mamlaka sehemu fulani ni lazima uonyeshe kwamba una mamlaka. Hilo usitie shaka, onyesha ushirikiano kwa wenzako pamoja na mimi kila kitu kitakuwa sawa. Kuhusu hili la mshahara naomba usiwaambie wenzako” Bwana Stewart alimwambia Gloria.
“Sitowaambia” Gloria aliitikia na kisha kuruhusiwa kuondoka ofisini hapo.

Bwana Stewart akarudi kitini na kuweka mguu juu, hakuamini kama kweli msichana Gloria angeweza kumkatalia mara pale atakapoanza kupiga ndogondogo. Kwake, Gloria alionekana kuwa msichana mwepesi sana ambaye kama ungetumia silaha ya fedha basi wala asingeweza kuteteleka hata mara moja, angefanya kila kitu ambacho ungetaka akifanye, likiwepo suala la kufanya mapenzi.

“Hanisumbui huyu. Nitatembea nae na sitohitaji lawama kwa mtu yeyote yule. Kama mtu anahitaji kulaumu, amlaumu yule aliyetengeneza fedha” Bwana Stewart alisema huku akionekana kuwa na furaha pamoja na uhakika wa kumpata Gloria bila kujua kwamba hata Kaposhoo nae alikuwa si msichana wake bali alikuwa amemuibia rafiki yake wa karibu, Peter.

*Je, nini kitandelea?
 
Back
Top Bottom