Song of Solomon

JF-Expert Member
Aug 5, 2021
2,725
5,472
DRC: Jumuiya ya Afrika Mashariki yakaribisha mgeni mpya baada ya kuwasili kwa DRC, anakuja na mazuri gani?

Mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yana kila sababu ya kusherehekea, yakiikaribisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kuwa mwanachama mpya wakati viongozi wake watakapokutana Machi 29.

DRC taifa kubwa lilojaa utajiri wa maliasili litakuwa mwanachama wa saba. Ni katika nia ya kutanua ushirikiano wa kikanda.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ilifufuliwa tena 1999 na mataifa matatu waasisi Tanzania, Kenya na Uganda baada ya ile ya awali kuvunjika 1977 kwa sababu za kisiasa. Burundi na Rwanda zilijiunga 2007 na Sudan Kusini 2016. Kongo inapakana na nchi zote hizo sita.

Bila shaka kwa kuzingatia ukubwa wa taifa hilo, lililoko katikati mwa Afrika ambalo limebatizwa jina la "moyo wa Afrika" na lenye wakazi milioni 90, idadi kubwa kuliko mataifa hayo mengine, kujiunga kwake itakuwa ni fursa kwa kila nchi kunufaika katika sekta mbali mbali za kiuchumi zikiwemo kilimo, biashara na usafiri.

Usalama ni ufunguo
Wakati kujiunga kwa DRC katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kutakuwa na tija kibiashara kwa mataifa yote wanachama, lakini kwa Uganda kuna la ziada. Hilo ni suala la usalama. Uganda kwa miongo zaidi ya miwili imekabiliwa na hali ngumu katika kupambana na waasi wa kundi la itikadi ya kiislamu Allied Democratic Forces (ADF) wanaoendesha harakti zao kutokea ardhi ya Congo.

ADF wamekuwa pia wakifanya vitendo vya mauaji katika eneo la Mshariki mwa Kongo, ukiwemo mji wa Beni wakisababisha taharuki kwa wakazi wa mji huo. Majeshi ya Uganda yaliingia Kongo Desemba 2021 kupambana na waasi hao wakishirikiana na wanajeshi wa Kongo.

Miaka ya nyuma DRC imekuwa na historia ya kuingiliwa katika nyakati mbali mbali na majirani zake Uganda, Rwanda na Burundi, kwa madai ya kupambana na makund tofauti ya waasi yaliopiga kambi mashariki ya Kongo na ambayo yamekuwa yakihatarisha usalama wao.

Utulivu na usalama katika ukanda huo mzima, kutafanikisha juhudi za kuboresha hali za kimaisha za wakazi wake, kutokana na utajiri wa kilimo,maliasili na nguvu kazi ya nchi zote kwa pamoja. DRC isiyo na bandari, upande wa mashariki, kupitia bandari kuu za Mombasa na Dar es Salaam kutakuwa na fursa adhimu ya kuongeza usafirishaji wa bidhaa zake huku ikinufaika kwa kuondolewa masharti ya awali ilipokuwa nje ya jumuiya.

DRC yenye wakazi milioni 90 ina uchumi wa karibu dola za Marekani bilioni 50. Inakadiriwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ina wakazi 177 milioni na uchumi wa dola bilioni 193.7. Kwa hiyo kuna kila sababu ya kujivunia ushirikiano wa pamoja, ambao utaongeza wigo wa kibiashara na kulitanua soko la Jumuiya.

Tshisekedi na jiihada za mabadiliko
Kuna matumaini kwamba kujiunga kwa Kongo na Jumuiya ya Afrika Mashariki kutasaidia kuipa kisogo historia yake ya misukosuko ya kisiasa na vita, iliyoiandama tangu uhuru kutoka kwa Ubeligiji Juni 1960. Tangu kuingia madarakani Rais Felix Tshisekedi 2019 kufuatia uchaguzi uliomaliza utawala wa miaka 18 wa mtangulizi wake, Joseph Kabila, Tshisekedi amefanikiwa kuigeuza sura ya Kongo.

Mafanikio hayo ni pamoja na jitihada za kupambana na tatizo sugu la rushwa kwa kiwango kikubwa, licha ya kuwa kibarua hicho kingali ni kigumu katika taifa ambalo rushwa iliota mizizi na kugeuka jambo la kawaida kwa miongo mingi licha ya jitihada za serikali kuikabili hali hiyo. Mageuzi katika taasisi za dola yamemsaidia kupata imani ya mataifa ya kanda na nje ya kanda hiyo.

Hata hivyo, badoTshisekedi atakuwa na kazi ngumu ya kubadili mtazamo wa wakazi wa eneo la magharibi mwa Kongo ukiwemo mji mkuu, Kinshasa na kuondokana na utamaduni wa kujihisi wanamafungamano zaidi na ulimwengu wa wanaozungumza lugha ya Kifaransa. Tatizo hilo haliko upande wa mashariki unaozungumza zaidi Kiswahili.

Ingawa tatizo hilo linaikumba pia Sudan Kusini, lakini mbali ya Kiarabu lugha ya Kiingereza ndiyo lugha rasmi. Mwaka 2017. Serikali ya Sudan Kusini ilitangaza azma yake ya kuanzisha mpango wa Kiswahili kufundishwa shuleni, ikiwa ni hatua ya kuelekea kuwa lugha rasmi siku za usoni. Rais Salva Kirr aliomba rasmi msaada wa walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania.

Jumuiya na uimarishwaji wa taasisi zake
Uimarishwaji wa taasisi za Jumuiya ni suala jengine muhimu linalohitaji kipaumbele na kupigania kuondoshwa kwa tafauti za kisiasa zilizosababisha kuzorota kwa taasisi hizo miaka ya karibuni. Itakumbukwa Jumuiya ilikuwa na azma ya kufikia hatua ya Shirikisho la kisiasa ifikapo 2012, lakini ilikwama kwa sababu mbalimbali ikiwemo mivutano na migogoro kati wanachama.

Miongoni mwa mivutano hiyo ni kati ya Rwanda na Burundi na Rwanda na Uganda, ingawa kwa kiwango fulani Rwanda na Uganda zimejongeleana kuondoa tafauti zao, lakini hatua hiyo haijafikiwa panapohusika na Rwanda na Burundi pamoja na kuwa hali imetulia kiasi fulani.

Mivutano imezorotesha utendaji wa sekretarieti makao makuu mjini Arusha, ambayo imejikuta ikijizuia kuwa na uwazi wa kutaja kwamba kuna matatizo. Mkutano wa viongozi 2019 na 2020 uliahirishwa kwa sababu ya kukosekana akidi.

Kukosekana akidi kwa mujibu wa sheria nambari 11 kunazuia utoaji maamuzi kuhusu masuala ya Jumuiya kama inavyosisitizwa na kifungu cha12 cha mkataba.

Hamu ya wengine kujiunga na Jumuiya inazidi
Licha ya hayo, kwa muda mrefu Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa kivutio si tu kwa DRC Kongo, bali pia kwa Somalia. Somalia vile vile iliomba kujiunga, lakini baada ya kikao cha Februari 21, 2021, viongozi wa nchi wanachama bado hawajalizingatia ombi lake.

Ombi la Somalia lilikataliwa 2016, pale viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliposisitiza kwamba ukosefu wa usalama nchini humo umeinyima sifa ya kuweza kuzingatiwa. Somalia iliupinga uamuzi huo na kujaribu kuomba tena uanachama miaka 5 baadaye. Inaelekea sababu ya awali ingali bado kikwazo.

Katika wakati ambapo wapiganaji wa kundi la itikadi kali ya Kiislamu wa Al Shabab bado ni tatizo si kwa usalama wa Somalia bali hata nchi jirani ya Kenya, moja ya nchi waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki kumekamilisha safari yake ya muda mrefu. Imepiga hodi na kukaribishwa. Na sasa ni kusonga mbele kufaidi tunu zilimo ndani ya Jumuiya huku nayo ikichangia tunu za kwake kwa manufaa ya nchi nyingine wanachama.
 
DRC: Jumuiya ya Afrika Mashariki yakaribisha mgeni mpya baada ya kuwasili kwa DRC, anakuja na mazuri gani?

Mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yana kila sababu ya kusherehekea, yakiikaribisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kuwa mwanachama mpya wakati viongozi wake watakapokutana Machi 29...
Analysis nzuri, ubarikiwe.
 
Eti wakuu sana, DRC kuwa mwanachama wa EAC inamaanisha nini kwa nchi yetu na jumuia kwa ujumla? Binafsi nimependa sana hili jambo.

Kwa muda mrefu Tz amekuwa mkwamishaji mkubwa wa mipango ya EAC akijivunia wingi wa watu na ukubwa wa ardhi.

siku zote akidai memba wengine wanataka kunyakua ardhi yake. Amekuja DRC ambaye ana ardhi nzuri kuliko TZ na kubwa kuliko memba wengine wote wakiwekwa pamoja.

Wana idadi kubwa ya watu na rasilimali nyingi sana. Tanzania siyo darling tena wa EAC.

Wewe unaonaje ujio wa DRC kwenye EAC?
 
Hii jumuiya ipo slow sana kwenye mambo ya muhimu kama biashara, ulinzi na usalama, uwekezaji wa wananchi wa jumuiya, demokrasia, sheria, nk.

Kila mmoja anataka kukumbatia vidubwasha vyake kwa tamaa za kijinga huku tukiacha fursa kubwa kubwa waje wachukue wachina na wazungu.

Mungu atusamehe sana kwa kuwa tunajidhalilisha sana mbele ya dunia.
 
As a noble citizen sijaona manufaa yake mpaka sasa, tunavutana vutana sana kwa mambo ya kidiplomasia na biashara tuache unafiki huu.
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom