GE2025 Uhuru wa Habari upo shakani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025

GE2025 Uhuru wa Habari upo shakani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

DodomaTZ

Senior Member
Joined
May 20, 2022
Posts
161
Reaction score
200
Malalamiko kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania yameongezeka tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu Agosti 28, 2025. Vyombo vya habari vimekuwa vikikabiliwa na vikwazo vingi, ikiwamo kupewa maonyo, kuamriwa kushusha maudhui yasiyoifurahisha Serikali, na hata kufungiwa.

Mfano mkubwa ni kusitishwa kwa leseni ya JamiiForums kwa siku 90 kuanzia Septemba 6, 2025, tukio linaloelezwa kuwa ishara ya ukandamizaji wa uhuru wa habari wakati wa uchaguzi. Wakati huohuo, taarifa za watu kutekwa au kupotezwa zimeongezeka, zikiwahusisha wakosoaji wa Serikali, waandishi wa habari na wahamasishaji wa mitandaoni, huku vyombo vya ulinzi vikihusishwa.

Ripoti ya Freedom House (2025) imepunguza hadhi ya Tanzania katika kipimo cha Freedom in the World kutoka “Huru kwa kiasi” hadi “Sio Huru,” kutokana na kudorora kwa haki za kiraia na utawala wa sheria.

Hayo yanajiri wakati kukiwa na sharia zinazolalamikiwa kukwaza uhuru wa habari nchini. Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari (2016) na Sheria ya Uhalifu wa Mtandao (2015). Sheria hizi zinampa Waziri mamlaka ya kusitisha magazeti au vyombo vya habari vinavyoonekana “kuhatarisha amani” na kudhibiti maudhui mtandaoni. Watetezi wa haki wanasema zinatumika kimabavu kukandamiza sauti za upinzani na ukosoaji wa Serikali.

Vyombo vya Habari Viko Njia Panda
Mwanahabari mkongwe Absalom Kibanda anasema mwaka huu vyombo vya habari “vimewekwa njia panda,” kwani baadhi vinaunga mkono Serikali huku vingine vikiwa havina uhuru wa kufanya kazi kwa uwazi.
Kibanda anasema matukio kama kesi ya Tundu Lissu na kauli za Augustino Polepole kuhusu uchaguzi, yamefunika habari za kampeni. “CHADEMA hawashiriki uchaguzi, lakini mshindani mkubwa wa CCM anaonekana kuwa Lissu, wakati hayupo kwenye karatasi za kura,” alisema.

Kwa mujibu wake, vyombo vingi vilivyo huru ni vile vya mtandaoni vilivyosajiliwa nje ya nchi kama Mange Kimambi, Sauti Kubwa na Mwanzo TV, huku vilivyosajiliwa nchini vikiwa chini ya udhibiti mkubwa. Kibanda ametoa mifano ya maudhui yaliyoshushwa, ikiwemo mahojiano ya The Chanzo na Maxence Melo, na yale ya Tido Mhando na Rostam Aziz yaliyocheleweshwa na mamlaka.

Ameeleza pia kuwa utekelezaji wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) umeacha waandishi wengi nje ya mfumo, akiwataja John Marwa (Jambo TV), Masoud Kipanya (Clouds TV) na Prisca Kishamba miongoni mwa waliokosa ithibati.

Kibanda anaamini Rais Samia Suluhu Hassan anaweza kurekebisha hali hii iwapo ataamua kuunda Tume ya Maridhiano itakayoshughulikia malalamiko ya uhuru wa habari.

Kufungiwa JamiiForums
Septemba 6, TCRA ilisimamisha leseni ya JamiiForums kwa siku 90, ikidai jukwaa hilo lilisambaza taarifa “zisizo sahihi” na zinazodhoofisha umoja wa taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Africa, Maxence Melo, alisema katika mahojiano na The Chanzo kwamba kufungiwa huko kulitokana na wananchi kulalamika kuhusu huduma za kijamii.

“Niliwaambia kuna changamoto za wananchi, wakasema ondoa, ukishindwa tunajua namna ya kuja, na kweli walikuja,” alisema. Aliongeza kuwa amepokea vitisho kutoka kwa watu “wanaojulikana lakini wasiojulikana rasmi,” akisema mmoja aliwahi kumpigia simu na kutishia maisha yake.

Vitisho kwa Vyombo Vingine
Baadhi ya vyombo vya habari vimesema vimepewa maonyo makali na kuamriwa kushusha maudhui yasiyo na “mizania.” Miongoni mwao ni The Chanzo, ambao walilazimishwa kuondoa mahojiano yao na Maxence Melo.

Mkurugenzi wa The Chanzo, Khalifa Said, alisema sababu zinazotolewa ni “ukosefu wa mizania,” jambo analoliona kuwa kisingizio cha udhibiti.

“Hali ya uhuru wa habari ni mbaya hata kabla ya uchaguzi. Tuliwahi kufungiwa kabla ya uchaguzi huu, kama ilivyotokea kwa gazeti la The Citizen lililofungiwa mwezi mmoja,” alisema.
Khalifa anaeleza kuwa taasisi kama Jukwaa la Wahariri (TEF) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) hazina nguvu za kulinda vyombo vya habari. “Hata ukilalamika hawana wanachoweza kufanya. Tunachofanya ni kupambana tu,” alisema.

Jambo TV: Maonyo na Hukumu
Mkurugenzi wa Jambo TV, John Marwa, alisema amepokea maonyo manne na hukumu moja kutoka TCRA tangu kuanza kwa kampeni. “Wanadai habari zetu hazina mizania, lakini kutoa sauti za wakosoaji wa Serikali si kosa,” alisema.

Anasema hali imekuwa ngumu zaidi wakati wa kampeni, akiongeza, “Hiki ni kipindi kigumu mno, natamani tu uchaguzi uishe.” Hata hivyo, Marwa alisisitiza kwamba vyombo vyake havikabiliwi na changamoto za kifedha, kwani “waandishi wote wanaofanya kazi kwenye kampeni nalipa vizuri.”

TEF Yatetea Uhuru wa Habari
Wakati waandishi wengine wakilalamikia udhibiti, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema “uhuru upo,” akidai tatizo ni uchumi wa vyombo vya habari, si udhibiti wa Serikali.

“Tatizo ni vyama vya siasa kuchukua waandishi kwa kampeni zao. Hapo ndipo uhuru unapotea. Lakini sisi hatujapokea malalamiko rasmi kutoka kwa vyombo vya habari vilivyodai kudhibitiwa,” alisema Balile, na kuongeza, “isije ikawa ni umbea wa mitandaoni kama wa Mange Kimambi.”

Hitimisho
Kadri uchaguzi mkuu wa 2025 unavyokaribia, dalili za kudorora kwa uhuru wa habari zinaonekana wazi kupitia kufungiwa kwa vyombo, vitisho kwa waandishi na udhibiti wa maudhui.

Wakati taasisi rasmi zikikanusha kuwepo kwa ukandamizaji, hali halisi inaonyesha mazingira ya uandishi kuwa magumu zaidi, huku vyombo vya habari vikihangaika kusawazisha majukumu yao kati ya uadilifu wa kitaaluma na shinikizo za kisiasa.
 
Back
Top Bottom